• Nairobi
  • Last Updated December 6th, 2023 9:00 PM
DINI: Aghalabu matatizo ni ishara ya uhai

DINI: Aghalabu matatizo ni ishara ya uhai

NA PADRE FAUSTINE KAMUGISHA

MTOTO akiwa analia anahitaji kubembelezwa.

Sio kila wimbo unaweza kumbembeleza mtoto. Wimbo mzuri ndio unambembeleza mtoto. Kauli nzuri ndizo zinambembeleza mtu. Kauli nzuri zinavutia mtu. Maneno matamu humtoa nyoka pangoni. Maneno ya upole na kuelewana hutatua tatizo sugu.

Maneno makali yanakata ini. Maneno makali yanauudhi kama mtu hajatenda kosa lolote.

Katika vitabu vitakatifu kuna maneno ya kutia moyo, maneno ya “kumbembeleza” aliyekata tamaa. Maneno hayo ni wimbo mzuri. Kwa mtu aliyeachishwa kazi au kushindwa jambo fulani tumia maneno ya mtunga mithali.

“Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, wala usizitegemee akili zako mwenyewe; katika njia zako zote mkiri yeye, naye atayanyosha mapito yako” (Mithali 3: 5). Maneno haya ni kama wimbo mzuri “unaombembeleza.”

Mungu ananyosha mapito. Mungu ananyosha njia.

Nathaniel Hawthorne alipopoteza kazi serikalini alirudi nyumbani akiwa na huzuni mkubwa amekata tamaa. Mke wake alipomtazama badala ya kumlalamikia alimpa kalamu na kumwekea wino mezani na kumwashia taa na kumwambia kuwa anaweza kutumia muda huu kuandika kitabu. Jamaa huyo akaandika kitabu kizuri kinachoitwa The Scarlet Letter. Mke wake alikuwa Mwana wa Faraja. Wito wangu uwe Mwana wa faraja.

Wimbo mbaya haumbembelezi mtoto. Mtu aliyefanya mambo mazuri mtie moyo. Yesu alipohubiri vizuri mwanamke mmoja katika mkutano alipaza sauti yake, “Heri tumbo lililokuzaa, na matiti uliyonyonya” (Luka 11:27). Yesu alitiwa moyo.

Dkt. Paul Tournier alipokea pongezi kubwa sana siku moja rafiki yake alipomtembelea nyumbani kwake. Rafiki yake alimletea ujumbe toka kwa mtu mwingine ambaye hakuwahi kukutana na Dkt. Paul Tournier lakini alisaidiwa sana na maandishi yake. Ujumbe ulisomeka hivi: “Unaenda kumuona Dkt. Paul Tournier huko Uswisi. Hakuna mashaka sitaweza kumuona katika dunia hii, lakini mwambie kuwa atakuwa mtu wa kwanza nitakayemtafuta kumuona huko mbinguni.” Alitoa pongezi wakati Dkt. Paul Tournier akiwa hai.

Tuwapongeze watu wakiwa hai. tusingoje kusoma historia ya marehemu na kumpongeza akiwa anazikwa. Pongezi hizo wakizisikia zitawatia faraja. Wimbo mbaya haumbembelezi mtoto.

Mtu aliyekata tamaa asome maneno haya, “Ulimwenguni mnayo dhiki, lakini jipeni moyo mimi nimeushinda ulimwengu” (Yohana 16:33).

“Yesu hasingeshinda ulimwengu na ulimwengu ukawashinda wanachama wake,” alisema Mt. Augustino wa Hippo Afrika ya Kaskazini.

“Bwana anaposhinda, wafuasi hawapaswi kuvunjika moyo,” alisema Mt. John Kyrisostomu aliyezaliwa Antiokia Syria (347-407).

Yesu ni mfano wa kuigwa wa kushinda ulimwengu.

Katika kitabu nilichokiandika MATATIZO SI TATIZO: MATATIZO NI DARAJA ninawatia moyo waliokata tamaa kwa kauli hizi: Matatizo hayana kauli ya mwisho. Matatizo ni alama ya mkato si nukta. Matatizo ni fursa zenye miiba. Usiziache fursa hata kama ziko kwenye miiba. Matatizo ni changamoto, zishinde. Matatizo ni ufunguo wa mafanikio.

Matatizo huwafanya baadhi ya watu kuvunjika moyo na wengine kuvunja rekodi. Kinacholeta baa la njaa ndicho kinakuonesha chakula kipatikanapo.

Matatizo ni giza la kukusaidia kuona nyota. Vitu vingi vimevumbuliwa kutokana na matatizo. Matatizo ni mwisho wa sura si mwisho wa kitabu. Matatizo ni weusi ulioko nyuma mbele ni kweupe.

Matatizo ni sumaku inayokuvuta uwe karibu na Mungu. Matatizo ni mapito. Matatizo ni ishara ya uhai.

Kuna watu ambao hawana tatizo lolote. Hawana madeni. Hawana wasiwasi. Hawana huzuni. Hawana msongo wa mawazo. Hawana mateso. Watu wa namna hii wako makaburini wamelala.

Wewe unayesoma makala haya hata kama una matatizo, matatizo ni ishara ya uhai. Kitabu ambacho nimetoa nukuu hizi ni wimbo mzuri unaombembeleza mwana. Yote yakiisha semwa, WIMBO MBAYA HAUMBEMBELEZI MTOTO.

You can share this post!

Nyong’o apiga marufuku mikutano ya injili kupunguza...

Ebola: Museveni hataweka ‘lockdown’ kote UG

T L