• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:55 AM
Ebola: Museveni hataweka ‘lockdown’ kote UG

Ebola: Museveni hataweka ‘lockdown’ kote UG

NA AFP

KAMPALA, Uganda

RAIS wa Uganda Yoweri Museveni amekariri kuwa hataamuru ‘lockdown’ kote nchini humo kuzuia kuenea kwa Ebola licha ya kuongezeka kwa visa vya maambukizi ya ugonjwa huo.

Tangu wizara ya afya ilitangaza mlipuko wa ugonjwa huo katika wilaya ya Mubende, ugonjwa huo umeenea maeneo mbalimbali nchini Uganda ikiwemo jiji kuu Kampala.

Lakini Museveni alishikilia kuwa hana mpango wa kuweka amri ya watu kutosafiri maeneo mbalimbali nchini humo, badala yake akiwataka wananchi kuwa “waangalifu zaidi” na wazingatie masharti ya kuzuia msambao wa Ebola.

“Hakutakuwa na ‘Lockdown’. Kwa hivyo, watu waendelee na shughuli zao za kawaida bila wasiwasi wowote,” akasema kupitia Twitter Ijumaa.

Idadi ya watu ambao wamekufa kutokana na ugonjwa huo, unaoenea kwa njia ya mtagusano, ni 49 kulingana na takwimu za serikali.

Lakini mnamo Alhamisi Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) lilisema Uganda imethibitisha visa 150 na vifo 64.

Ebola huenea pale majimaji kutoka kwa mgonjwa yanapopitishwa hadi mtu mwingine. Dalili zake ni ongezeko la joto mwilini, kutapika, kutokwa na damu sehemu mbalimbali za mwili na kuendesha.

Ni vigumu kudhibiti milipuko ya ugonjwa huo, haswa katika maeneo ya mijini ambako kuna misongamano ya watu.

Watu walioambukizwa, hawawezi kuwaambukiza wengine hadi dalili zitakapoanza kujitokeza baada muda wa kati ya siku mbili na 21.

Mlipuko wa Ebola Uganda ulitangazwa kwa mara ya kwanza mnamo Septemba 20.

Lakini siku 20 baadaye Rais Museveni alisema kuwa “hakukuwa na haja kwa serikali kuamuru kusitishwa kwa shughuli za kawaida kote nchini.”

Hata hivyo, mnamo Oktoba alitangaza amri ya kutotoka nje nyakati za usiku katika miji ya Mubende na Kassanda, akazima usafiri na kuamuru kufungwa kwa masoko, baa na makanisa kwa siku 21.

Aidha, Rais Museveni aliamuru kukamatwa kwa mtu yeyote aliyeambukizwa Ebola na akakataa kujitenga.

Mnamo Alhamisi, WHO ilionya kuhusu uwezekano wa Ebola kuenea zaidi na ikatoa wito kwa mataifa jirani kuweka mikakati ya kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo.

Mara ya mwisho mlipuko wa Ebola kuripotiwa nchini Uganda ilikuwa mnamo 2019.

Aina ya kirusi cha Ebola kinachosambaa wakati huu nchini Uganda inajukana kama Sudan Ebola.

Kufikia wakati huu chanjo ya kudhibiti aina hii ya kirusi cha Ebola haijapatikana, japo kuna chanjo nyingi zinazofanyiwa majaribio.

  • Tags

You can share this post!

DINI: Aghalabu matatizo ni ishara ya uhai

Mahakama kukamilisha kesi 50 za watoto

T L