• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 1:24 PM
DINI: Tufuate nyayo za Mungu aliyetupa ‘Zawadi’

DINI: Tufuate nyayo za Mungu aliyetupa ‘Zawadi’

Na PADRE FAUSTINE KAMUGISHA

KRISMASI inapambwa na zawadi.

Krismasi inapambwa na ukarimu.

Demetri Martin alisema, “Nilifunga zawadi zangu za Krismasi kwenye karatasi za kufungia zawadi lakini nilitumia karatasi ambazo si sahihi zilikuwa na meneno: Heri ya Kuzaliwa. Sikutaka kuzipoteza nikaongeza neno Yesu.”

Kwenye zawadi ya Krismasi, ongeza neno Yesu. Hakuna Krismasi bila Yesu Kristu. Yesu ni zawadi ya Mungu Baba kwetu. Mungu ametupa zawadi ya mwanawe: Yesu Kristo. Hii ni zawadi ya Krismasi.

“Mungu hatoi kamwe zawadi kwa watu ambayo hawana uwezo wa kuipokea. Kama anatupa zawadi ya Krismasi, ni kwa sababu nyote mna uwezo wa kuielewa na kuipokea,” (Papa Fransisko). Tusichoke kumpokea Yesu.

Tufuate nyayo za Mungu Baba aliyemtoa zawadi mwanawe. Mungu ni mtoa zawadi tujifunze kwake.

“Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amsadikiye asipotee, bali awe na uzima wa milele” (Yohane 3: 18).

Zawadi si zawadi kama haipokelewi. Tusichoke kumpokea Yesu. Kardinali Hume alihuburi Krismasi moja. Aliwashangaza waumini katika parokia ndogo huko London ya Kaskazini. Kwa mshangao wa wengi, hakutaja kuzaliwa kwa Bwana wetu Yesu Kristu.

Badala yake aliwaambia waamini juu ya hadithi ya kweli ya kilichotokea katika kambi za kutesea watu wakati wa vita ya pili ya dunia. Watu walipiga mstari wakingojea zamu zao za kuingia kwenye chumba cha kifo.

Milango ilipofungwa wakati uliwadia wa msichana mdogo wa kiyahudi kuingia kwenye chumba. Alikuwa amesimama peke yake akitetemeka kwa hofu, akilia na akiwa uchi.

Alikuwa ameshikilia kifuani mwanasesere, mali pekee aliyokuwa nayo. Waliokuwa pale kila mmoja alikuwa anafikiria hofu zake. Hakuna aliyemuona anatetemeka, ila askari wa Kijerumani ambaye kazi yake ilikuwa ni kuhakikisha anawapeleka kwenye kifo chao.

Kulia kwa mtoto kulimgusa askari huyo. Naye alivua nguo zake mwenye akaingia kwenye chumba cha mauti akishika mkono wa mtoto huyo. Uso wa mtoto ulikuwa na nuru.

Ghafla aliacha kulia. Milango ya chumba cha mauti ilipofunguka waliingia pamoja wakishikana mikono. Hilo ndilo Yesu Kristu alifanya miaka 2,000 iliyopita. Aliingia kwenye ubinadamu wetu kutusaidia na kutuondolea hofu.

Krismasi inatokea mara moja kwa mwaka. Ni tarehe 25 Desemba kila mwaka. “Krismasi ni kipindi cha kuwasha moto wa ukarimu katika ukumbi, na miale ya joto la ukarimu moyoni,” alisema Washington Irving.

 

You can share this post!

Museveni afungua uchumi, japo kwa masharti makali

Ruto atoboa siri yake na Mudavadi

T L