• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Ruto atoboa siri yake na Mudavadi

Ruto atoboa siri yake na Mudavadi

Na CHARLES WASONGA

HATIMAYE Naibu Rais William Ruto ametoboa siri kuhusu mipango yake ya kumnyakua kiongozi wa ANC, Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya, Moses Wetang’ula ili kuimarisha nafasi yake ya kuingia Ikulu.

Akiongea mjini Mumias Ijumaa, Dkt Ruto alidokeza kuwa amekuwa akizungumza na wawili hao na kwamba hivi karibuni atawasiliana nao yeye binafsi ili wafanye uamuzi. Wawili hao ni vinara washirika katika muungano wa One Kenya Alliance (OKA) unaojumuisha kiongozi wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka na Gideon Moi wa Kanu.

Dkt Ruto aliwataja kama “matapeli” viongozi wengine wa eneo la Magharibi wanaounga mkono vuguvugu la Azimio la Umoja, la kiongozi wa ODM, Raila Odinga, akisema wanapanga kunadi jamii ya Waluhya kwa matajiri.

“Hii ndiyo maana ninaendelea kuongea na Mudavadi na Wetang’ula ili tuunde serikali pamoja. Na hii ninaomba kwa unyenyekevu mkubwa zaidi,” Dkt Ruto akasema alipohudhuria fainali ya dimba la Malala Super Cup katika uwanja wa Mumias Complex, Kaunti ya Kakamega.

“Jambo muhimu wakati huu ni kwamba tunapaswa kufanya kazi pamoja ili tushinde uchaguzi mkuu ujao. Kwa hivyo, binafsi nitawatafuta Mudavadi na Wetang’ula ili kwa pamoja tufanye uamuzi wa mwisho,” akaongeza.

Dkt Ruto alisema si lazima awe mgombeaji wa urais wa muungano atakaobuni pamoja na vinara wenzao hao wa One Kenya Alliance (OKA).

Alisema, “Hata Mudavadi anaweza kuwa mgombeaji wetu wa urais mradi atushawishi kwamba atatupa ushindi.”

Dkt Ruto alisema jamii ya Waluhya imemuunga mkono Bw Odinga tangu 2007 lakini hajaifanyia lolote la kuwashukuru watu wake kwa hisani hiyo.

Huku akionekana kumtambua Bw Mudavadi kama kigogo wa siasa katika eneo hilo, alisema: “Mimi hutafuta idhini kutoka kwa Mudavadi pekee kabla ya kuja hapa Magharibi wala si mtu mwingine. Wale wanaojidai kuwa wakombozi mumewaunga mkono kwa miaka 30 iliyopita lakini wakawasaliti viongozi wenu.”

Imekuwapo minong’ono kwamba mazungumzo yanaendelea kati ya kambi ya Dkt Ruto, kwa upande mmoja, na ile ya Bw Mudavadi na Wetang’ula, kwa upande mwingine, kwa lengo la kushirikiana kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo katika mahojiano kwenye runinga ya Citizen wiki hii, Bw Mudavadi alisema kama mwanasiasa yeye yuko tayari kufanya kazi na yeyote, mradi asishurutishwe.

“Watu wasijitwike wajibu wa kuwachagulia wengine marafiki. Nitafanya uamuzi wangu na hakuna kisichowezekana, mradi hakitakiuka katiba,” akasema.

“Nitafanya uamuzi kuhusu ni nani nifanye kazi naye, wakati wa kufanya hivyo ukitimu,” Bw Mudavadi akaongeza alipoulizwa ni nani kati ya Dkt Ruto na Bw Odinga, yu tayari kushirikiana naye.

Huenda hii ndiyo maana kiongozi huyo wa ANC, akaamua dakika za mwisho kutohudhuria fainali ya Malala Super Cup, Mumias baada ya kung’amua kuwa Dkt Ruto alialikwa. Hii ni licha ya kwamba Bw Mudavadi alikuwa amealikwa kama mgeni mheshimiwa katika mchezo huo na akathibitisha kuwa angehudhuria.

Duru ziliambia Taifa Jumapili mwenzake wa Ford Kenya, Bw Wetang’ula, pia alikwepa kufika licha ya kuratibiwa kama naibu mgeni mheshimiwa, kutokana na sababu hiyo hiyo.

“Ni siri iliyo wazi kwamba viongozi hawa wawili wamekuwa wakifanya mazungumzo ya kisiri na Ruto kuhusu suala zima la wao kushirikiana katika uchaguzi mkuu ujao,” akasema mbunge mmoja wa ANC ambaye aliomba tulibane jina lake.

“Wawili hao wanahisi ni mapema mno kwa wao kufanya uamuzi kama huo.”

Naye mchanganuzi wa siasa za Magharibi mwa Kenya Martin Andati pia alichangia katika mjadala huu.

“Ni baada ya Mudavadi na Wetang’ula kufeli kufika uwanjani humo, kinyume na mipango ya Dkt Ruto na Bw Malala, ambapo naibu huyo wa rais aliamua kupasua mbarika kuhusu nia yake ya kushirikiana na viongozi hao,” akaongeza Bw Andati.

  • Tags

You can share this post!

DINI: Tufuate nyayo za Mungu aliyetupa ‘Zawadi’

Spurs wakomoa Watford na kuweka hai matumaini ya kuingia...

T L