• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
DINI: Ulimi kiungo cha ajabu sana; ni dawa ya kutuliza, na pia sumu kali inayoua

DINI: Ulimi kiungo cha ajabu sana; ni dawa ya kutuliza, na pia sumu kali inayoua

Na FAUSTIN KAMUGISHA

ULIMI ni dawa, ulimi ni sumu.

Ndiposa Mungu alijua hatari ya ulimi akauwekea kuta mbili: ukuta wa meno na wa mdomo.

“Ulimi una nguvu ya kuua na kufanya hai.” (Methali 18:21).

Neno la kutia moyo ni dawa. Neno la kuliwaza ni dawa. Neno la kutuliza ni dawa.

Maneno ya kisasi ni sumu. Msalabani Yesu walimwambia maneno saba. Sita yalikuwa ni sumu.

Neno la kwanza kwa Yesu msalabani lilikuwa la kejeli.

“Watu waliopita njiani walimtukana, wakatikisa vichwa vyao na kusema, “Ewe uwezaye kulibomoa hekalu na kulijenga upya kwa siku tatu, ujisalimishe mwenyewe. Ukiwa Mwana wa Mungu, shuka msalabani.” (Mathayo 27: 39 – 40).

Kejeli ya wapitanjia ni sumu ya ulimi. Bwana Yesu alidhihakiwa kwa sababu alifanya vitu tofauti kwa mtazamo tofauti. Ukifanya vitu vizuri tofauti utavuna kejeli. Usikate tamaa.

Neno la pili kwa Yesu msalabani ni neno la matusi.

“Mmoja wa wale wahalifu waliotundikwa alimtukana akisema, “Je, wewe si Kristo? Basi, jiokoe mwenyewe na sisi pia” (Luka 23: 39).

Naye asiyeweza hudharau; yasema methali moja ya Tanzania.

“Lugha ya matusi ni silaha ya watu dhaifu,” alikariri Joseph Appasway. Wewe si mtu dhaifu usitumie matusi.

Neno la tatu kwa Yesu msalabani ni neno la matumaini.

Matumaini ni dawa kwamba kesho itapendeza. Ni jambo lililodhihirishwa na mwizi wa upande wa kulia wa Yesu pale msalabani, ambaye katika mapokeo ya Kanisa Katoliki anaitwa Dismas.

Dismas alitumainia maisha baada ya kifo. Akamwambia Yesu, “Ee Yesu, unikumbuke utakapoingia katika ufalme wako” (Luka 23: 42).

Neno la nne kwa Yesu msalabani ni simango.

“Kadhalika, makuhani wakuu pamoja na waandishi na wazee wakamdhihaki wakisema, “Aliwaokoa wengine, kujiokoa mwenyewe hawezi. Kama ni mfalme wa Israeli basi (Mungu) amwokoe sasa kama anampenda kwa maana alisema, ‘Mimi ni Mwana wa Mungu” (Mathayo 27: 41 – 43).

Yesu alisimangwa. Alivumilia, akatufundisha kuvumilia masimango.

Neno la tano ni mkanganyiko.

Baadhi ya wale waliosimama pale na kusikia walisema, “Tazama, anamwita Eliya.” Mmoja akaenda haraka, akajaza sifongo siki, akaitia juu ya mwanzi na kumpa anywe akisema, “Acheni, na tuone kama Eliya atakuja kumteremsha” (Marko 15: 35 -36).

Changamoto ni kuweka maneno mdomoni mwa Yesu. Maneno ya kuwekewa mdomoni yanaudhi.

Neno la sita ni dhihaka.

Askari pia walimdhihaki. Walimjongea na kumletea siki wakisema, “Kama wewe ni mfalme wa Wayahudi jisalimishe mwenyewe” (Luka 23: 36 -37).

Mungu hadhihakiwi. Kwa askari hao, waliona kuwa Mungu wa Wayahudi alikuwa dhaifu. Hakuweza kujitoa msalabani.

Lakini Mungu hadhihakiwi; acha Mungu aitwe Mungu. Yesu alikuwa na mpango “B.” Alifufuka.

Neno la saba ni neno la imani.

“Akida aliyesimama mbele yake alipoona jinsi alivyokata roho alisema, “Hakika, mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu” (Marko 15: 39).

Huu ndio mustakabali unaoongoza mtu kwenye imani ya kweli.

Askari huyu anawakilisha watu wote wanaopata imani kwa Yesu; kwamba kuongoka kwao si matokeo ya kuona miujiza na maajabu, bali ni kwa kutambua maana ya upendo wa Kristo kama anayetoa maisha yake kwa wote katika upendo.

Hiki ndicho kiini cha imani ya kweli na wanadamu kumkubali Kristo.

Jambo kubwa tunajifunza kutokana na kifo cha Yesu msalabani ni kwamba; hata ukisemwa vibaya kwa kuonewa wivu, usikate tamaa.

Yesu yupo katika mateso na uchungu mwingi, lakini hakukata tamaa.

Ni mtumishi anayeshikilia wajibu wake mkuu aliokuja kutimiza hapa duniani; kujitwika dhambi za ulimwengu ili kuleta wokovu.

Wanazipigania nguo zake. Shtaka la “Mfalme wa Wayahudi” lipo juu ya kichwa chake.

Wanamdhihaki huku wakuu wa dini wakimfyolea.

Nao wahalifu wawili waliosulubiwa pamoja naye wanamtukana.

Lakini katika haya yote Yesu hakutamka neno baya, alijua zawadi iliyokuwa ikimsubiri kutoka kwa Mungu Baba.

  • Tags

You can share this post!

JAMVI: ODM imekoroga ngome yake kwa kumvua Malala wadhifa...

Utata magavana waliobwagwa wakipanga kuwania