• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Utata magavana waliobwagwa wakipanga kuwania

Utata magavana waliobwagwa wakipanga kuwania

Na JUSTUS WANGA

UTATA umeibuka kuhusu iwapo magavana ambao walipoteza viti vyao baada ya kuhudumu kwa muhula mmoja wanaweza kuwania wadhifa huo tena kaunti tofauti za walizosimamia na kuhudumu kwa miaka 10 wakichaguliwa 2022.

Haya yanajiri wakati miongoni mwa magavana waliobwagwa katika uchaguzi mkuu wa 2017 wametangaza kwamba watawania viti hivyo tena mwaka ujao.

Baadhi yao, kama aliyekuwa Gavana wa Nairobi, Evans Kidero, wameamua kuwania katika kaunti tofauti na walikohudumu kwa miaka mitano kuanzia 2013 hadi 2017.

Vile vile, kuna kizungumkuti kuhusu hatima ya magavana ambao watakuwa wamekamilisha mihula yao miwili lakini wanataka kuwania kiti hicho katika kaunti tofauti.

Ingawa Katiba inasema gavana atahudumu kwa mihula miwili (ya miaka mitano kila mmoja), wataalamu wa kisheria wametofautiana kuhusu fasiri yake, haswa kuhusiana na hali ambapo gavana anataka kuhamia kaunti nyingine baada ya kushindwa katika awamu ya kwanza.

Kwa mfano, baada ya kuhudumu muhula mmoja na kushindwa na Mike Sonko katika uchaguzi mkuu wa 2017, Dkt Kidero ametangaza kuwa atawania tena katika kaunti ya Homa Bay.

Swali ni je, endapo atawania na kushinda kiti hicho, atahudumu kwa muhula mmoja au miwili ikizingatiwa kuwa amehudumu kwa miaka mitano kama gavana wa Nairobi?

Dkt Mutakha Kangu, ambaye alihudumu kama mwenyekiti wa Jopokazi la Ugatuzi kuhusu katiba ya sasa, anasema kuwa wale ambao waliwahi kuhudumu kwa muhula mmoja wanaweza kuhudumu kwa mihula miwili wakichaguliwa katika kaunti zingine.

“Hitaji la kikatiba la kwamba gavana hawezi kuhudumu zaidi ya mihula miwili linatumika kwa ajili ya kaunti moja mahsusi. Hii ina maana kuwa Kidero, kwa mfano, anaweza kuhudumu kwa mihula wiki endapo atashinda katika chaguzi,” akasema Dkt Kangu.

“Hii ina maana kuwa mtu kama Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya, ambaye katiba imemzuia kuwania tena, anaweza kuhamia kaunti jirani kama ya Busia na kuwania ugavana,” mtaalamu huyo anaeleza.

Kulingana na Dkt Kangu hakuna kipengele cha sheria kinachomfungia mtu kuwania ugavana katika kaunti fulani pekee.

“Sheria kuhusu mihula ya ugavana inatumika tu katika kaunti mahsusi,” akasema.

Kwa upande wake, mwanasheria Peter Wanyama, anasema hakuna kipengele cha sheria kinachomzuia gavana kuwania kiti hicho katika kaunti nyingine.

Hata hivyo, anasema, ufasiri wa kisheria mahakamani au bungeni unahitajika kutoa mwelekea kuhusu suala hilo. Anaeleza kuwa watalaamu walioandika katiba waliweka mihula miwili ya ugavana kuimarisha uwajibikaji katika utawala.

“Hawakulenga kumpa mtu nafasi ya kukamilisha mihula miwili katika kaunti moja kisha ahamie kaunti nyingine kuwania kiti hicho hicho,” Bw Wanyama anaeleza.

“Wanaweza kuwania viti vingine kama vya ubunge na useneta,” anapendekeza akiongeza kuwa nchini Nigeria magavana waliokamilisha mihula yao miwili katika jimbo moja hawaruhusiwi kuwania wadhifa huo katika jimbo lingine.

Lakini wakili wa masuala ya kikatiba Paul Mwangi anaonya kuwa kuwaruhusu wanasiasa kuwania ugavana kwingineko baada ya kukamilisha mihula yake miwili itatoa mfano mbaya wa “ukiukaji wa sheria.”

“Sheria kuhusu mihula miwili inafaa kuzingatia na wanasiasa hao hata ikiwa watahamia kaunti zingine; kwa sababu sheria inahusu mtu binafsi,” anasema Mwangi.

Naye wakili wa serikali Kennedy Ogeto anashikilia kuwa hitaji la katiba kwamba mtu ahudumu kama gavana kwa mihula miwili pekee sharti lizingatiwe hata kama gavana atahamia kaunti nyingine.

You can share this post!

DINI: Ulimi kiungo cha ajabu sana; ni dawa ya kutuliza, na...

Harambee Stars yafika Togo salama salmini