• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 7:50 AM
JAMVI: ODM imekoroga ngome yake kwa kumvua Malala wadhifa Seneti

JAMVI: ODM imekoroga ngome yake kwa kumvua Malala wadhifa Seneti

Na BENSON MATHEKA

HATUA ya chama cha ODM ya kumpokonya Seneta wa Kakamega Cleophas Malala wadhifa wa naibu kiongozi wa wachache katika Seneti huenda ikanyima chama hicho cha chungwa uungwaji mkono ambao kimekuwa kikifurahia eneo la Magharibi mwa Kenya kwa miaka mingi.

Bw Malala wa chama cha Amani National Congress (ANC) kinachoongozwa na Musalia Mudavadi, alivuliwa wadhifa huo siku chache baada uchaguzi mdogo wa eneobunge la Matungu, Kakamega ambao alipigia debe mwaniaji wa chama hicho Oscar Nabulindo aliyemshinda David Were wa ODM.

Viongozi wa ANC wanahisi kwamba masaibu ya Bw Malala yalitokana na mchango wake katika uchaguzi huo mdogo ambao waliungana na vyama vya Wiper, Kanu, Ford Kenya na Jubilee kushinda ODM ambacho kimekuwa kikifurahia umaarufu mkubwa eneo la Magharibi.

Wadadisi wa siasa wanasema kwamba kwa kumtimua Bw Malala, ODM kinajiweka katika hatari ya kufifia eneo hilo hasa baada ya kutofautiana na washirika wake katika muungano wa NASA.

Hatua hii inajiri miaka mitatu baada ya kumvua kinara mwenza wa NASA, Moses Wetangula wadhifa wa kiongozi wa wachache katika seneti.

Bw Wetangula, kiongozi wa chama cha Ford Kenya anatoka eneo la Magharibi na ameshirikiana na Bw Mudavadi kuunganisha jamii ya Waluhya jambo ambalo wadadisi wa kisiasa wanasema halifurahishi ODM.

“ODM hakifurahishwi na ukuruba wa kisiasa wa Bw Mudavadi na Wetangula na kwa kumvua Malala wadhifa huo kilirudia makosa yaliyokifanya kutofautiana na vigogo hao wa kisiasa wa jamii ya Mulembe. Hii inakiweka katika hatari ya kupoteza umaarufu ambao kimekuwa kikifurahia eneo hili ikizingatiwa kwamba ushirikiano wa ANC na Ford Kenya umeanza kushika kasi,” asema mdadisi wa siasa Patrick Wafula.

ODM hakifurahishwi na ushirikiano wa ANC na Wetangula wanaoutaja kama wa kikabila.

Duru zinasema kwamba hatua ya kumpokonya Bw Malala wadhifa wa uongozi katika seneti ilinuiwa kutisha vyama tanzu vya NASA ambavyo vimekuwa vikilaumu ODM kwa kukiuka mkataba wa muungano huo na ambavyo sasa vimeungana chini ya mwavuli wa One Kenya Alliance.

“Hatutakubali siasa za utapeli na vitisho ambavyo wenzetu wanashiriki,” alisema Bw Mudavadi na kuongeza kuwa ODM hakikufurahishwa na mchango wa Malala katika uchaguzi mdogo wa Matungu.

Kulingana na Bw Wafula, huenda ODM ikajutia hatua yake ikizingatiwa kuwa Bw Malala ana ushawishi mkubwa sana miongoni mwa vijana wa eneo la Magharibi hasa kaunti ya Kakamega iliyo na idadi kubwa ya wapigakura.

“Mikakati ya ODM ya kumpokonya Bw Malala wadhifa wa uongozi katika seneti itakuwa pigo kwa chama hicho. Kimekoroga ngome yake ya kisiasa ya magharibi wakati ambao inashuhudia mwamko mpya wa kisiasa kupitia ushirikiano wa vigogo wa kisiasa,” asema.

Seneta wa Kilifi

Nafasi ya Malala katika seneti, ilikabidhiwa seneta wa Kilifi Stewart Madzayo katika kile ambacho wadadisi wanasema ODM ililenga kuzima uasi eneo la Pwani.

Viongozi wa eneo hilo ambalo pia ni ngome ya ODM, wamekuwa wakitaka kuanzisha chama chao cha kisiasa. Kiongozi wa ODM, Raila Odinga amekuwa akipinga hatua hiyo akisema Kenya hahiitaji vyama vya kisiasa vya kikabila.

Duru zinasema kwamba viongozi wa eneo la Pwani wanatarajiwa kuzindua chama chao kipya wiki ijayo wakiongozwa na Gavana wa Kilifi Amason Kingi.

Inasemekana kwa kumkabidhi seneta Madzayo wadhifa wa Malala katika seneti, ODM ilinuia kuvuruga mipango ya viongozi wa pwani na hasa Kilifi kuungana kuzindua chama cha kisiasa cha eneo hilo.

Baadhi ya viongozi wa Pwani wamekuwa wakimlaumu Bw Odinga kwa kupuuza eneo lao wakati wa kugawa nyadhifa za uongozi bungeni.

Wakati mmoja Malala alikuwa mshirika wa Bw Odinga kabla ya kupatana na kiongozi wa chama chake cha ANC, Musalia Mudavadi.

“Yaliyompata Malala ni baadhi ya kafara ambazo wanasiasa hufanya kwa kushikilia wanachoamini. Tunasimama na Malala,” alisema Bw Mudavadi.

Kulingana na wadadisi wa siasa, hatua ya ODM ya kumvua Malala wadhifa alioshikilia kwa hisani ya NASA, huenda ikafifisha umaarufu wa chama hicho eneo la Magharibi na ngome za vyama tanzu vya muungano huo.

“Ni hatua ambayo haikufaa wakati huu uchaguzi mkuu unapokaribia ambao chama hicho kinahitaji kuwa na nguvu kinavyodai kinafanya. Kumpokonya Malala wadhifa wake katika seneti kunaweza kutia nguvu wapinzani wao katika Okoa Kenya Alliance,” asema mdadisi wa siasa, Geff Kamwanah.

Malala ni seneta wa tatu wa eneo la Magharibi kupokonywa wadhifa wa uongozi na ODM.

Mbali na Wetangula, ODM kilimvua seneta wa kuteuliwa wa ANC Petronilla Were wadhifa wa naibu kiranja wa wachache na kuukabidhi seneta wa kuteuliwa Beatrice Kwamboka.

You can share this post!

Uchungu wa ‘lockdown’

DINI: Ulimi kiungo cha ajabu sana; ni dawa ya kutuliza, na...