• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
GWIJI WA WIKI: Moji Shortbabaa

GWIJI WA WIKI: Moji Shortbabaa

Na CHRIS ADUNGO

JAMES Muhia almaarufu Moji Shortbabaa alianza safari ya elimu akitazamia kutia nanga katika madarasa ya kusomea taaluma ya uanasheria chuoni.

Hata hivyo, kipaji cha uanamuziki kilimteka nyara akiwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya upili ya Senior Chief Koinange iliyoko Kiambaa, Kaunti ya Kiambu.

Alishiriki mashindano mengi ya ngazi na viwango tofauti na akatambisha shule yake kwenye tamasha za kitaifa za muziki na drama. Alijizolea tuzo za haiba kubwa zilizomfanya maarufu miongoni mwa wanafunzi wenzake.

Tangu wakati huo, hakupoteza dira wala kurudi nyuma katika fani ya uimbaji.Shortbabaa alishirikiana na aliyekuwa mwanafunzi mwenzake katika shule ya upili – Silvanus Otieno almaarufu Didi Man – kuanzisha kikundi cha Kelele Takatifu kilichowakuza zaidi kisanaa.

‘Itakuwa Ngori’, ‘Bamba Mbaya’ na ‘Haina Noma’ ni baadhi ya nyimbo walizofyatua wakiwa katika kundi hilo lililodumu kati ya 2010 na 2017.

“Walimu walijitolea kupalilia kipaji changu na shule ikanipa majukwaa tele ya kukitononoa. Wazazi walinitandikia zulia murua lililochochea maono yangu kuwa ndoto zenye thamani. Kufaulisha azma hiyo kulihitaji subira, bidii, nidhamu na ukakamavu,” anasema.

Kufikia mwanzo wa 2022, Shortbabaa alikuwa amekwea ngazi ya muziki wa injili kiasi cha kujivunia albamu mbili – ‘Yesu Mtaani’ (2018) na ‘Cheza Gospel’ (2021).

Aliungana na msanii Kevin Amenge Okoth almaarufu Jabidii kutoa kibao ‘Vimbada’ kabla ya kushirikiana na DJ Kwenye Beat na Guardian Angel kusuka wimbo ‘Hajawahi Niangusha’ ambao pia waliuachilia 2018.

Mbali na wimbo ‘Dance ya Kanisa’ aliocharaza 2019, kazi yake nyingine maarufu zaidi ni kibao ‘Roho Mbaya’ alichokitoa Julai 2022, miezi minne baada ya kushirikiana na Eunice Njeri kufyatua wimbo ‘Utukuke’.

‘Mazuri’, ‘Shuka Usitumane’, ‘Sitadanganya’, ‘Mtoto’, ‘Mitumba’, ‘Imani’ na ‘Mungu wa Musa’ ni baadhi ya nyimbo nyinginezo ambazo amezisana kwa Kiswahili.

Tangu 2016, Shortbabaa amekuwa akipata mialiko ya kupiga shoo katika majimbo mbalimbali nchini Amerika kila mwaka.

Aliwahi pia kuburudisha mashabiki jijini Kampala, Uganda, akiwa na kikundi cha Kelele Takatifu mnamo 2014.

Kubwa zaidi katika maazimio yake ni kuendelea kuachilia kazi zinazokubalika kimataifa huku akitambua, kukuza na kulea vipaji vya wanamuziki chipukizi.

Anapania pia kushirikiana na Roy Smith ‘Rufftone’ Mwita, Mercy Masika na Evelyn Wanjiru kutumia uimbaji kueneza Ukristo, kukuza maadili na kuipa jamii mwelekeo. Hawa ni miongoni mwa wasanii waliomchochea zaidi kujitosa katika tasnia ya muziki.

Upekee wa Shortbabaa ulingoni ni upevu wa masimulizi, ukwasi wa msamiati, ufundi wa kufumbata ujumbe wa muziki kupitia mtindo wa ‘Afro-pop’ pamoja na ujuzi wa kusuka na kuremba maneno.

Amewahi kupata fursa adhimu za kuwa mshereheshaji katika hafla muhimu za mashirika, kampuni na watu binafsi kutokana na kipaji chake cha ulumbi, ubunifu wa kiwango cha juu na weledi wa kukisarifu Kiswahili.

Shortbabaa alizaliwa katika mtaa wa Kawangware na akalelewa katika eneo la Ngando, Nairobi.

Ndiye mwanambee katika familia ya watoto watatu wa Bw Paul Wachira na marehemu Bi Esther Waithera.

Alisomea katika shule ya msingi ya Ngong Forest, Nairobi (1998-2005) kabla ya kujiunga na Senior Chief Koinange (2006-2009).

Ana diploma ya uanahabari kutoka chuo cha East African School of Media Studies (EASMS), Nairobi (2011-2013).

Anamstahi sana mkewe, Bi Nyawira Gachugi, anayezidi kuiwekea taaluma yake mshabaha.

  • Tags

You can share this post!

KINYUA BIN KING’ORI: Katiba ina utaratibu namna...

VYAMA: Chama cha Kiswahili katika shule ya msingi ya...

T L