• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
VYAMA: Chama cha Kiswahili katika shule ya msingi ya Garissa Progressive Academy

VYAMA: Chama cha Kiswahili katika shule ya msingi ya Garissa Progressive Academy

NA CHRIS ADUNGO

CHAMA cha Kiswahili katika shule ya msingi ya Garissa Progressive Academy (CHAKIGAPA) kiliasisiwa Januari 20, 2009 kwa lengo la kuwaamshia wanafunzi hamu ya kuchapukia masomo ya lugha.

Chama hiki kinafadhiliwa na wakurugenzi wa shule – Bw Abdiaziz Abdi na Bw Said Abdi. Mbali na Bw Khalid Abdirizak ambaye ni mlezi wa chama, shughuli za CHAKIGAPA husimamiwa na Mwalimu Mkuu Bw David Munyelele kwa ushirikiano na naibu wake Bw Vincent Ouma.

“Chama hiki ni chombo madhubuti kinacholea vipaji vya wanafunzi katika sanaa mbalimbali na kuwakuza pia kimaadili. Wengi wao tayari wameamshiwa hamu ya kuwa wanahabari, walimu, waandishi na wahariri wa kazi za Kiswahili,” anasema Bw Abdirizak.

Uanachama wa CHAKIGAPA unalenga wanafunzi wote na unajumuisha pia walimu wa Kiswahili shuleni pamoja na wenzao walio na ari ya kujifunza na kubobea katika lugha hii.

Mbali na kuboresha matokeo ya Kiswahili katika KCPE, chama pia kimekuwa jukwaa mwafaka kwa wanafunzi kukuza talanta zao katika uigizaji, utunzi wa mashairi, uandishi wa kazi bunilizi, utambaji wa hadithi, ulumbi, uimbaji na uchoraji.

Zaidi ya kuweka wazi umuhimu wa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi, madhumuni mengine ya CHAKIGAPA ni kustawisha makuzi ya lugha na kuzidisha maarifa ya utafiti katika fani zinazofungamana na Kiswahili.

Baadhi ya shughuli za wanachama ni kukusanya habari na kuziwasilisha gwarideni kila Ijumaa.

Wao hukutana mara kwa mara baada ya vipindi vya mchana kutwa ili kujadili mikakati ya kuimarisha chama na kuzamia mada za somo la Kiswahili zinazowatatiza madarasani.

Chama kinaongozwa na Omar Abdullahi, Faiza Yunis, Amran Ali, Aisha Aden, Fatuma Ali, Ismail Abdiwahab, Hared Abdi na Shamsa Abdille.

  • Tags

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: Moji Shortbabaa

NGUVU ZA HOJA: Hili swali ni gumu na vilevile rahisi, Je...

T L