• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 5:50 AM
Hamiliki nyumba wala shamba Nairobi, lakini anazalisha mboga kwa wingi na kuuzia wakazi

Hamiliki nyumba wala shamba Nairobi, lakini anazalisha mboga kwa wingi na kuuzia wakazi

NA FRIDAH OKACHI

WATU husema Nairobi ni shamba la mawe, na ili kujimudu kimaisha, ni sharti mtu anoe bongo na kutafuta mbinu za kumwezesha kukidhi mahitaji ya jiji.

Katika eneo la Kawangware, Jane Changawa alielewa vyema ushauri huo. Japokuwa yeye hana nyumba wala shamba jijini, maarifa yake yamemwezesha kuuzia wakazi mboga kutoka shambani mwake.

Akiwa mpangaji, sawa na mamilioni ya wakazi wa Nairobi wasiomiliki nyumba, Bi Changawa anamudu vyema kuwalisha na kuwasomesha wajukuu wake wanne kwa kutumia sehemu ya paa la nyumba aliyokodisha, kufanya kilimo cha mboga. Kupitia kilimo hicho, amepiga hatua katika kukabiliana na gharama ya juu ya maisha.

Bi Changawa alibadilisha paa la nyumba ‘Top-roof’ kuwa shamba kwa kutumia mtindo wa kilimo mjini. Sehemu hiyo yenye upana wa mita 50 na 20, imepandwa kila aina ya mboga jambo, ambalo anasema mumewe ameweza kukumbatia.

“Wakati nilianza kupanda mboga, nilikuwa nimefanya tu kitalu cha kuniwezesha kuwa na mboga zangu za kula na familia yangu. Lakini ilifikia wakati zikawa nyingi. Wauzaji mboga barabarani wakaanza kuja kuzinunua,” anasema Bi Changawa.

Pesa anazopata kwenye biashara ya kilimo hicho, zimemwezesha kuongeza hisa zake katika chama kimoja ambapo yeye ni mwanachama.

Si mambo ya chama pekee. Kitalu hicho juu ya nyumba ya wenyewe kimempa ajira kamili, kwa kuwa pesa anazopata huzitumia kulipa karo ya shule ya wajukuu wake.

“Huwa nauza Sh100, naweka mahali. Zikifika Sh2,000-Sh3,000 kwa wiki moja nalipa karo au kuwekeza,” anasema.

Mama huyo mwenye umri wa miaka 57, anasema alipata ujuzi wa kupanda mimea mbalimbali baada ya shirika moja kutoa mafunzo na kumpa gunia moja la mchanga.

“Nilianza na gunia moja lakini ikafika hatua nikaongeza hadi yakawa magunia 10, kutokana na sehemu pana ya paa lile,” anaeleza Bi Changawa.

Ukulima huo wa kisasa umefanya mpagaji huyo kuepuka mambo mengi. Hutumia muda wake mwingi kuhakikisha anapata mapato yake ya kila siku.

“Ugonjwa wa kisukari umefanya nitie bidii kuongeza sehemu nyingine ya kilimo. Naugua ugonjwa wa kisukari. Daktari aliniambia nile mboga kwa wingi. Imenilazimu nimuombe mwenye nyumba mwingine nafasi ya paa lake. Nazidi kupanda mboga na mimea mingine. Nikitumia mboga hizo inakuwa bora kwa afya yangu,” anasema.

Katika kilimo hicho, Bi Changawa anasema hutumia mbinu za kiasili kuhakikisha anapata mavuno yanayofaa. Anajitengenezea mbolea na dawa ya kunyunyuzia mimea yake.

“Ni vyema wakulima wajue harufu ya dania hutorosha wadudu kwenye mboga. Mimi huwa sinunui mbolea au dawa. Ule uchafu unaotoka jikoni; kuanzia mboga, ugali, maganda ya kila aina ya matunda, matawi ambayo sihitaji na kadhalika. Mimi huweka kwenye karatasi la plastiki nafunga na unaanza kuoza. Baada ya siku utaanza kutoa maji meusi. Maji yenyewe huwa hayavutii macho,” anasema.

Anaongeza, “Nitatoboa karatasi ile na kuweka katika kikombe. Nitaongeza maji kikombe kimoja na hiyo ni dawa tosha kwa mimea. Wadudu hawapendi harufu mbaya.”

Anaongeza kuwa changamoto yao kubwa ni maji ambayo wanalazimika kugharimia.

Mmiliki wa nyumba hizo Bw Geoffrey Mongare, aliambia Taifa Leo kwamba nia ya mpagaji wake ilimruhusu kumpa nafasi hiyo, ili kuendeleza kilimo.

Hata hivyo, alimweleza awe akitumia karatasi ya plastiki ili kuzuia maji hayo kuingia kwenye simiti na kisha kumpa fursa ya kuweka mifereji inayomwaga maji kutoka juu

  • Tags

You can share this post!

Mume wangu hana ustadi wa kucheza mechi chumbani, nifanyeje?

Jinsi mradi wa magazeti shuleni ulivyoipa shule Eldoret...

T L