• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:47 PM
Himizo wakulima wazalishe mazao salama kuwahi soko la kimataifa

Himizo wakulima wazalishe mazao salama kuwahi soko la kimataifa

Na SAMMY WAWERU

WAKULIMA nchini wametakiwa kuhakikisha wanazingatia mifumo bora kitaalamu ili kuzalisha chakula salama.

Meneja Msimamizi wa Mikakati katika Ubalozi wa Denmark Kenya, Bw Charles Wasike amesema soko la mazao yanayouzwa nje ya nchi litanoga endapo wakulima wataafikia vigezo vya kimataifa katika usalama wa chakula. Akizungumza jijini Nairobi, afisa huyo alisisitiza haja ya wakulima kuhakikisha wanaepuka matumizi ya dawa zenye kemikali katika ukuzaji na uzalishaji.

Alisema lango la soko la kimataifa linaamuliwa na ubora wa mazao, usalama ukipewa kipau mbele. “Soko bora na lenye ushindani mkuu, humu nchini na katika ngazi ya kimaitafa linaingiwa kupitia uzalishaji wa mazao salama,” Bw Wasike akasema, akihimiza wakulima kumakinika katika utendakazi wao.

“Tuhakikishe kinachotufikie mezani ni salama. Hiyo ndiyo siri pekee kuwahi soko bora la kimataifa.” Mapema mwaka huu, kampuni ya kimataifa yenye mikahawa kuchoma kuku na kukaanga vibanzi – chipsi nchini (KFC) ilijipata kwenye kikaangio moto Wakenya kuivamia mitandaoni, kufuatia msimamo wake wa kukosa kununua viazi vinavyokuzwa nchini.

Kwenye majukwaa ya mitandao wakionyesha hasira na hamaki, waliikashifu wengine wakiitaka “iuzie chakula chake wanunuzi wa kimataifa – nje ya nchi”. Walionya endapo haitakuwa ikinunulia wakulima wa Kenya viazi, watagoma kula bidhaa zake.

Bw Charles Wasike, ambaye Meneja Msimamizi Mikakati katika Ubalozi wa Denmark Kenya, anahimiza wakulima kuzalisha mazao salama ili kuwahi soko la kimataifa…Picha/ SAMMY WAWERU

KFC hata hivyo kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, ilijitetea ikihoji wakulima humu hawazingatii usalama wa mazao, baadhi ya dawa zinazotumika kukabili wadudu na magonjwa zikiwa zilizopigwa marufuku. Kulingana na Waziri wa Kilimo, Bw Peter Munya, idara yake inaendelea kufanya majadiliano na kampuni hiyo ili iwe inanunua viazi vinavyolimwa humu nchini.

Aidha, KFC inadaiwa kununua kuku kutoka Uturuki na viazi kutoka Misri, kati ya mataifa mengine. Licha ya Kenya kuwa muuzaji mkuu wa maua, kahawa, majanichai na matunda soko la kimataifa, Bw Wasike anahimiza haja ya hamasisho miongoni mwa wakulima kufanywa.

“Serikali na wadauhusika katika sekta pana ya zaraa, tujitume kuhamasisha wakulima umuhimu wa kuzalisha chakula kwa njia salama,” akasisitiza. Kwa mujibu wa takwimu za Fairtrade Africa, mazao mabichi ya shambani hususan yanayochukua muda mfupi kukomaa kama vile mboga na matunda, Kenya inaendelea kufanya bora katika soko la kimaifa.

Data za kampuni hiyo yenye washirika wa kilimo na kuwatafutia mianya ya soko ng’ambo zilizotolewa mwaka uliopita, 2021, pia zinaonyesha bidhaa zilizoongezwa thamani zina mapato ya kuridhisha. “Tunasihi wakulima wakumbatie mifumo ya kuongeza mazao thamani. Bidhaa zilizosindikwa zimeonyesha dalili kuteka soko bora,” akasema Kate Nkatha, Msimamkzi wa Mauzo Fairtrade Africa.

Kufuatia mkurupuko wa ugonjwa wa Covid-19 Kenya Machi 2020, idadi ya watu wanaoendeleza shughuli za kilimo imetajwa kuongezeka. “Tumeshuhudia ongezeko la Wakenya wanaofanya kilimo baada ya virusi vya corona kutua nchini, licha ya kuwa sekta hii imekuwa ikifanya bora,” akasema Bw Wasike ambaye pia husimamia kilimo-biashara na bunifu kuangazia mabadiliko ya tabia nchi, katika Ubalozi wa Denmark Kenya.

Mamia na maelfu ya watu walipoteza nafasi za ajira kufuatia athari za Covid, ugonjwa ambao ni janga la kimataifa.

You can share this post!

Tiba asili

Popcaan aahirisha shoo yake Nairobi kwa mara nyingine, hadi...

T L