• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 12:56 PM
Arati kwenye kinywa cha mamba Naibu wake akiungana na mahasimu

Arati kwenye kinywa cha mamba Naibu wake akiungana na mahasimu

NA WYCLIFFE NYABERI

Huenda msimamo mgumu wa Gavana wa Kisii Simba Arati wa kutowalipa wanakandarasi mabilioni ya pesa wanayodai serikali ya kaunti ukawa chanzo cha mgogoro baina yake na naibu wake, Dkt Robert Monda.

Deni hilo ni la zaidi ya Sh1.2 bilioni lakini kulingana na Arati, ni Sh235 milioni pekee zilizo halali na amedokeza hizo ndizo atakazolipa.

Hatua hiyo imeibua joto kali la kisiasa Kisii na wanakandarasi ambao wameambiwa walifanya “kazi hewa” wamejiunga na upande wa Dkt Monda wakitishia kufadhili hoja itakayolenga kumng’atua afisini Gavana Arati.

Tangu wachaguliwe kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka jana, wawili hao wamekuwa wakifanya kazi kwa pamoja. Watu wengi wamekuwa wakiwatolea mfano wa gavana na naibu wake bora ambao wana uhusiano mzuri wa kikazi.

Lakini hali sasa imebadilika haraka na viongozi hao hawaonani uso kwa macho.

Mambo yalianza kufichuka Jumamosi iliyopita, mnamo Novemba 25, 2023, baada ya Dkt Monda kuwakaribisha nyumbani kwake wakosoaji wakubwa wa Bw Arati, katika makazi yake yaliyoko kijijini Rigena, eneobunge la Nyaribari Chache.

Wakosoaji hao walijumuisha mbunge wa Mugirango Kusini na Kiranja wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Silvanus Osoro, Seneta wa Kisii Richard Momoima, Mwakilishi wa Kike wa Kisii Dorice Aburi, wabunge Japheth Nyakundi (Kitutu Chache Kaskazini), Daniel Manduku ( Nyaribari Masaba) na madiwani kadhaa.

Mkutano huo ulijiri saa chache baada ya wakosoaji hao kuhudhuria hafla ya shukrani katika kanisa katoliki la Nyabururu, ambapo Spika Moses Wetang’ula alikuwa mgeni wa heshima.

Kanisani Nyabururu, Seneta Onyonka, wabunge Manduku na Bi Aburi walimjia juu Gavana Arati kwa msimamo huo wake mkali wa kutowalipa wanakandarasi pesa.

“Nimejaribu kuwashauri lakini wana vichwa vigumu. Tumejaribu kuwarai waweke pesa kwa kina mama, wakarabati barabara, wajenge madarasa ya ECDE na kuwalipa walimu wao, tumejaribu kuwaeleza wawalipe wanakandarasi pesa zao lakini hakuna wanachokifanya,” Seneta Onyonka alisema, huku kauli zake zikiungwa mkono na Dkt Manduku na Bi Aburi.

Baadhi ya wanakandarasi wanaolilia pesa zao walikuwa kwenye hafla hiyo ambayo viongozi wa kisiasa waliohudhuria walikuwa wale wanaoegemea serikali.

Hafla hiyo ya Nyabururu ilipotamatika, wakosoaji hao wa Arati pamoja na baadhi ya wanakandarasi wanaoidai kaunti walifululiza moja kwa moja hadi kwa Dkt Monda aliyekuwa akiwasubiri.

Baada ya kushiriki chajio, wabunge hao ambao ni mwiba kwa gavana walijikita katika kikao cha faragha kwa zaidi ya saa nne.

Walipomaliza kikao hicho cha usiku, Bw Osoro ambaye aliwaongoza wakosoaji aliwaambia wanahabari kuwa Dkt Monda alikuwa ameonyesha hofu kuwa kaunti ya Kisii ilikuwa imewekewa vigezo kuwa haitapokea mgao zaidi kutoka kwa serikali kuu iwapo haingelipa madeni yake.

“Kwa hakika, tumezungumza mengi. Naibu Gavana alituita hapa na kutueleza kuwa hakuna mradi hata mmoja wa maendeleo ambao wameanzisha kinyume na walivyoahidi raia kwenye kampeni. Amedokeza pia kwamba hafurahii jinsi fedha za maendeleo zinatumika Kisii kwa hivyo tumekuja kutafuta suluhu,” Bw Osoro alisema na kisha akakataa kuulizwa maswali yoyote na wanahabari. Naibu gavana hakuzungumza hata kidogo kuhusu mkutano wao.

Mkutano huo katika makazi ya Dkt Monda ulijiri siku tano tu baada ya Mkaguzi Mkuu wa Bajeti (CoB) Dkt Margaret Nyakang’o kuiandikia serikali ya Kisii waraka kuhusu madeni ambayo hayajalipwa.

Barua ya Dkt Nyakang’o ilimwendea waziri wa Fedha wa Kisii Kennedy Abincha ikitaka kujua ni mpango upi uliopo wa kulipa madeni hayo.

Bw Abincha alitakiwa kueleza mbinu iliyotumika kusema kuwa baadhi ya madeni hayakuwa halali. Serikali ya gatuzi hilo ilipewa hadi Desemba 10 ili kutoa maelezo kabla ya kupewa mgao zaidi wa fedha.

Huku vita kati ya gavana na naibu wake vikishamiri, tayari makundi mawili yamejitokeza, kila kundi likitetea mtu wao.

Cha kushangazwa ni kuwa makundi hayo yanatoka katika ukoo wa Abanyaribari, anakotoka Dkt Monda.

Kundi la kwanza lilimkashifu Dkt Monda kwa kuwakumbatia wakosoaji wa Gavana Arati ilhali la pili lililodai kuwa wao ndio Abanyaribari halisi wakamtetea naibu gavana.

  • Tags

You can share this post!

Riggy G akemewa kupeleka siasa za Mungiki hafla ya heshima...

Kizaazaa babu aliyeenda kununua mahaba kugundua mtumbuizaji...

T L