• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Riggy G akemewa kupeleka siasa za Mungiki hafla ya heshima ya mwimbaji Samidoh

Riggy G akemewa kupeleka siasa za Mungiki hafla ya heshima ya mwimbaji Samidoh

Na JOHN NJOROGE

Wakazi wa Molo katika Kaunti ya Nakuru wamekashifu hatua ya Naibu Rais Rigathi Gachagua kugeuza jukwaa la hadhi ya juu la msanii Samidoh kuwa uwanja wa kupiga siasa kuhusu kundi haramu la Mungiki. 

Wakiongea na Taifa Leo, wananchi hao wamesema kuwa maongezi hayo hayakuambatana na hafla ya mwanamuziki mashuhuri Samidoh, jina halisi Samuel Muchoki Alhamisi, Novemba 30, 2023 katika Parklands Sports Club ambapo Naibu Rais alikuwa mgeni wa heshima.

“Hii ilikuwa sherehe tofauti na ile ya wanasiasa ambapo Gachagua hangefaa kuongea maneno hayo kwani haikuwa mkutano wa kisiasa,” David Kibe, mkazi wa Elburgon alisema na kuongeza kuwa matamshi kama hayo yanaweza kuzua balaa nchini na kufanya vijana wasio na hatia kutiwa baroni na kushtakiwa kwa mashtaka yasio halali.

Kama kiongozi wa wanaoishi mlima Kenya na sehemu zingine za nchi hasa za jamii ya Wakikuyu, Bw Kibe alisema kuwa Naibu Rais alifaa kuunganisha vijana.

Matamshi ya Bw Gachagua yanajiri wiki moja baada ya wabunge wa kike kutoka eneo la Mlima Kenya kuibua wasiwasi kuhusu kuzuka upya kwa kundi hilo haramu.

Hata hivyo, kumekuwa na ukosoaji kuhusu hatua ya Bw Gachagua kuzungumzia kuhusu kundi hilo wakati baada ya uchaguzi ilhali wakati wa kampeni, hakukuwa na matamshi yoyote kuhusu maovu ya kundi hilo, jambo lililofanya gumzo kuhusu Mungiki kufasiriwa kuwa la kisiasa.

Mkazi mwingine, Kienje Kihara anasema kuwa wakati wa kampeni, vijana walijulikana na kutambulika kama “jeshi” ambapo lilimaanisha vijana.

“Kama mwananchi mzalendo, sikusikia kijana yeyote aliyeshikwa kwa utumizi wa jina hilo lililomaanisha “Army” kwa kimombo. Ifikapo kwa jina Mungiki likitajwa, huonekana kama ni kundi haramu lakini kwa jamii ya Wakikuyu, ni jina la wingi wa watu,” akasema Kihara na kuongeza kuwa kila kabila huwa na jina na utamaduni wao linalofaa kuheshimiwa.

Katika hafla hiyo, Naibu Rais aliwaomba wasanii kutotumiwa vibaya.

“Nataka kuwasihi wasanii wetu kuwa makini sana. Msikubali kutumiwa vibaya na kazi zenu kutekwa nyara na watu wenye tabia mbaya na historia mbaya. Wanawatisha wanawake kutokana na shughuli zenu,” akasema Naibu Rais wakati wa uzinduzi wa Wakfu wa Samidoh Alhamisi usiku katika Parklands Sports Club, Nairobi.

Shirika la hisani lisilo la kiserikali linamilikiwa na mwanamuziki wa Kikuyu Muchoki Samidoh.

“Naomba msinyanyaswe na watu wenye tabia zenye mashaka, watu wanaojaribu kukutumia sasa mnajua walichokifanya kwa vijana wetu na kilichotokea kwa watoto wetu,” aliwaambia wasanii hao.

Naibu Rais alisema kuwa watu wanaohusishwa na kundi lililoharamishwa wanajaribu kurejea kwa umma kupitia hafla zinazoandaliwa na wasanii na kuteka nyara shughuli hizo ili kuhutubia umati.

Aliwataka wasanii kuhakikisha matukio yao yanakuwa na heshima kwa kuwanyima watu wachafu jukwaa la kuzungumza na hadhira.

 

  • Tags

You can share this post!

Mbunge Milly Odhiambo atumai hata yeye atapata mtoto uzeeni...

Arati kwenye kinywa cha mamba Naibu wake akiungana na...

T L