• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
JAMVI: Roho ya Uhuru iko kwa OKA au Raila?

JAMVI: Roho ya Uhuru iko kwa OKA au Raila?

Na CHARLES WASONGA

HUKU ikisalia miezi tisa pekee kabla ya Wakenya kwenda debeni kumchagua rais mpya, mrengo ambao Rais Uhuru Kenyatta ataunga mkono kukabiliana na Naibu wa Rais, Dkt William Ruto ungali kitendawili.

Ingawa inaaminika kuwa anamuunga mkono kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga katika kinyang’anyiro cha urais, uhusiano wake na baadhi ya vigogo wa One Kenya Alliance (OKA) huenda ukamfanya abadili nia.Vigogo wakuu katika muungano huo uliobuniwa mnamo Machi 25, 2021 wanajumuisha Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi (ANC), Moses Wetang’ula (Ford Kenya), Gideon Moi (KANU) na aliyekuwa Mbunge wa Lugari, Bw Cyrus Jirongo.

Rais Kenyatta amekuwa akiendesha juhudi za kuwashinikiza vinara wa OKA wamuunge mkono Bw Odinga katika kivumbi cha urais lakini hazijafua dafu.Hii ni kufuatia mikutano ambayo Rais Kenyatta amefanya na vinara hao katika Ikulu za Nairobi na Mombasa kuwarai wamuunge mkono waziri huyo mkuu wa zamani.

Vile vile, inadaiwa kuwa Rais Kenyatta amejaribu kutumia wanachama wa Wakfu wa Mlima Kenya (MKF) kujaribu kurai vinara hao waunge mkono Bw Odinga. Mnamo Oktoba 7, 2021 wanachama wa MKF walikutana na vinara wa OKA katika mkahawa wa Safari katika kile kilichodaiwa kuwa ni juhudi zao za kusaka mgombeaji urais anayefaa kumrithi Rais Kenyatta.

Lakini vinara wa OKA wameshikilia kuwa wataunga mkono mmoja wao katika kinyang’anyiro cha urais 2022 na kwamba, “wananchi ndio wenye mamlaka ya kuamua rais wao wala si watu wengine.Wadadisi wanasema juhudi hizi za Rais Kenyatta zinaonyesha kuwa bado hajafanya uamuzi wa mwisho kuhusu ni nani atakayemuunga mkono kuwa mrithi – Kwamba anakabiliwa na changuo mbili;

Bw Odinga au mmoja wa vinara wa OKA.“Kwa sababu ni wazi kwamba Rais Kenyatta na Naibu wake, Dkt Ruto hawawezi kupatana wakati huu, anaweza kuamua ni Raila au mmoja wa vinara wa OKA. Hii ni endapo juhudi za kuunganisha mirengo hii miwili zitaambulia patupu,” anasema Dismus Mokua ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya kisiasa.Kulingana naye, Rais Kenyatta amejipata katika njia-panda kuhusu suala hili kulingana na uhusiano wa karibu kati yake na Seneta Moi na kwa kiwango fulani, Bw Musyoka.

“Ni siri iliyo wazi kuwa kuna ukuruba mkubwa kati ya Rais Kenyatta na Seneta Moi kutokana na historia ya familia zao. Kwa mfano, ni baba yake Gideon (Rais wa zamani marehemu Daniel Moi) aliyemlea Uhuru kisiasa,” Bw Mokua anaongeza.Isitoshe, urafiki kati ya Seneta Moi na Rais Kenyatta unasemekana kuanza utotoni, wawili hao walipokuwa wanafunzi katika Shule ya St Mary’s Nairobi ambayo ilikuwa mojawapo ya shule za kifahari katika miaka ya ‘70.

Mnamo Julai 6, 2020 Rais Kenyatta alimtuma Seneta Moi nchini Malawi ambapo alimwakilisha katika hafla ya kuapishwa kwa Rais mpya wa nchi hiyo, Lazarus Chakwera. Uhusiano huu wa karibu kati ya Seneta Moi na Rais Kenyatta haujafurahisha mrengo wa ANC ndani ya OKA ambao sasa unamsawiri kuwa kibaraka cha Rais Kenyatta na Bw Odinga.

Seneta wa Kakamega Cleophas Malala pia amemtaja Seneta Moi kama “jasusi wa Raila” ndani ya muungano huo kutokana msimamo wake kwamba OKA ishirikiane na Bw Odinga kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

You can share this post!

Marufuku ndege za Afrika Ulaya

Aliyetekwa arudi nyumbani baada ya miezi mitano

T L