• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
SHINA LA UHAI: Je, bora mitishamba?

SHINA LA UHAI: Je, bora mitishamba?

NA WINNIE ATIENO

ALIPOKUWA akitumia vidonge vya kupanga uzazi, Josephine Karisa, 45, anasema aliugua mara kwa mara na hata kuvuja damu zaidi wakati wa hedhi.

Dawa hizo pia zilimfanya akose ari ya kushiriki tendo la ndoa. Lakini ni baada ya kushika mimba mara tatu ilhali alikuwa anatumia sindano ya kupanga uzazi, ndipo mumewe alibaini kuwa hali si shwari.

“Mume wangu alidhani nilimdanganya kwamba nimedungwa dawa ya kupanga uzazi baada ya kushika mimba nyingine. Ilibidi tuandamane hadi hospitalini kusaka majibu,” asema Bi Karisa.

Lakini walishtuka walipoambiwa na daktari kwamba dawa alizokuwa amedungwa zilikuwa zimepita muda wa matumizi ndio maana hazikufanya kazi ilivyokusudiwa.

Bi Karisa, mkazi wa eneo la Arabuko Sokoke, Kaunti ya Kilifi, anasema mumewe alimsihi baada ya hapo asiendelee kuzitumia na akaahidi kumtafutia dawa mbadala.

Baada ya chunguza chunguza zake, Karisa Dakawale, 60, ambaye ni karani wa kundi la wadau wa mitishamba eneo hilo, aligundua mbegu maalum ambayo jamii ya Waatha walikuwa wakitumia walipokuwa wakiishi msituni maeneo ya Pwani.

Bi Josephine Karisa, 45, akiwa na mumewe Karisa Dakawale, 60, wakithibitisha tembe za mturi turi ni muhimu katika upangaji wa uzazi. PICHA | WACHIRA MWANGI

“Nilitafuna tembe tano za mbegu za mturi turi miaka mitano iliyopita na sijawahi kupata ujauzito wala kuvuja damu tena. Tembe hizo zimenisaidia sana maanake siumwi tena na tumbo, kichwa wala maradhi mengine yanayoletwa na vidonge vya kupanga uzazi. Hazina athari yoyote kwangu,” akasema mama huyo wa watoto sita.

Bw Dakawale asema ilibidi amsaidie mke wake kukabiliana na athari za kutumia dawa za kisasa za kupanga uzazi.

“Ilibidi nimshauri aachane na dawa hizo tuanze kukumbatia dawa za kiasili ambazo hazina madhara yoyote. Lakini wasiwasi wangu ni kwamba mke wangu hapati hedhi tena,” akasema.

Aidha anasema nyumbani kwake hakuna dawa za kisasa zinazotumika isipokuwa za mitishamba.

“Tunatumia mitishamba kutibu magonjwa. Pia tunakula vyakula vyenye nyuzinyuzi hasa matunda kama ndizi na maembe na kunywa maji mengi sana ili tuepukane na maradhi. Damu yako ikiwa safi huwezi ugua. Nina umri wa miaka 60 lakini mwonekano ni mtu wa miaka 40,” aongeza.

Naye Tabu Batula, 50, kutoka jamii ya Waatha asimulia jinsi mbegu za mturi turi zilivyomwokoa baada ya kudhurika na vidonge vya kupanga uzazi.

“Kama si mbegu hizi, leo ningekuwa na watoto 20 kama wenzangu,” asema Bi Batula, mama wa watoto tisa huku akisisitiza hazina madhara yotote.

Kwa miaka na mikaka jamii ya Waatha wamekuwa wakiishi kwenye misitu maeneo ya Pwani hasa Boni na Arabuko Sokoke, lakini Kenya ilipojinyakulia uhuru 1963, walianza kutangamana na Wakenya wengine.

Hata hivyo, Waatha hawakuacha mila zao za jadi hasa kuhusu chakula na mitishamba kutibu magonjwa.

Mbegu za mturi turi zimekuwa zikitumiwa na jamii hiyo kupanga uzazi tangu jadi, na sasa Serikali imeagiza wanasayansi na watafiti kufanya uchunguzi zaidi.

Kulingana na watafiti wa Makavazi ya Kitaifa wakishirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Matibabu nchini (Kemri) , matokeo ya utafiti huo ulioanza Julai 2021, yanaonyesha matumaini.

Wanasema wamegundua kuwa mbegu hizo zimekuwa zikitumiwa na jamii za Asia hasa nchini India kupanga uzazi.

Dkt Amos Lewa, ambaye ni mtafiti wa mitishamba kutoka Kemri, anasema tembe moja huwa inazuia mwanamke kushika mimba kwa miezi mitatu, tembe mbili miaka miwili na tembe tatu kwa miaka mitano.

Katika Institute of Primate Research, taasisi ambayo hutumia wanyama kufanya utafiti wa matibabu ya binadamu, mtafiti mkuu, Dkt Atunga Nyachieo, anasema wanaendeleza utafiti wa mbegu hizo wakitumia nyani ili kutathmini kikamilifu zinavyofanya kazi na ikiwa zina madhara.

Dkt Nyachieo ameipongeza serikali kwa kukumbatia dawa za kiasili kukabiliana na magonjwa nchini kwani dawa hizo zinazidi kukumbatiwa na mataifa mengine ulimwenguni. Alitoa mfano wa China ambayo imewekeza sana kwa mitishamba iliyogunduliwa inatibu malaria.

“Walipogundua waganga wa mitishamba wanatumia mti maalum kutibu malaria, walishirikiana nao. Serikali ikafanya utafiti ambao ulionyesha dawa hiyo inatibu malaria. Hii leo wanaedelea kuwekeza kwa waganga. Duniani watu wananunua dawa za malaria kutoka China. Kenya pia inalenga mkondo huo kwenye utafiti wa mturi turi,” akasema Dkt Nyachieo.

Anaongeza kuwa, watafiti na kampuni za kutengeneza dawa ulimwenguni, wanasaka dawa ya kupanga uzazi ambayo haina madhara kwa mwanamke.

Naye mwenzake Dkt Evans Taracha anasema nyani 12 wanaendelea kufanyiwa uchunguzi ambapo awamu ya kwanza imewapa matumani makubwa kwamba tembe za mturi turi zinaweza kutumika kupanga uzazbila madhara.

Dkt Evans Taracha wa Makavazi ya Kitaifa, anasema awamu ya kwanza ya uchunguzi imewapa matumaini makubwa kwamba tembe za mturi turi zaweza zikatumika kupanga uzazi. PICHA | WACHIRA MWANGI

Hata hivyo, Dkt Taracha anasema kwamba tembe hizo zinapokatizwa, wanawake wanaweza kushika mimba baada ya miezi miwili au tatu.

Anaongeza kuwa katika kipindi cha miezi sita ijayo watakuwa wamemaliza utafiti kwa nyani na waanze kufanya utafiti kwa wanawake.

Haya yanajiri huku serikali ikinuia kuhalalisha waganga na wakunga wa kienyeji ili kuimarisha sekta ya afya nchini.

“Mpango wa kuhalalisha tiba ya kiasili umeshika kasi. Wizara inaweka mikakati ya kuunda mswada wa tiba ya kiasili. Mswada huu ukipitishwa, itakuwa ni halali kwa hata wakunga wa kienyeji kusaidia kina mama kujifungua,” asema Waziri Msaidizi wa Afya, Dkt Rashid Aman.

Kando na Pwani, mmea wa mturi turi hupatikana maeneo ya Bonde la Ufa na Magharibi mwa Kenya ijapokuwa matumizi yake ni tofauti kwa jamii tofauti. Jamii zingine hutumia mbegu za mturi turi kukabiliana na kisukari.

You can share this post!

Raila ajitahidi kudhibiti kaunti telezi ya Pwani

DKT FLO: Kwa miezi 3 sasa koo yanisumbua

T L