• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Jinsi kamanda wa polisi Maragua alivyokataa Sh40,000 ambazo inadaiwa wazazi wa mshukiwa wa kitendo cha kunajisi mwanafunzi, wakiwa na rafiki yao, walijaribu kumkabidhi

Jinsi kamanda wa polisi Maragua alivyokataa Sh40,000 ambazo inadaiwa wazazi wa mshukiwa wa kitendo cha kunajisi mwanafunzi, wakiwa na rafiki yao, walijaribu kumkabidhi

Na MWANGI MUIRURI

SHERIA iko aghalabu kuhakikisha kuna usawa na haki, lakini binadamu na ujeuri wao pia hulenga kukiuka utaratibu ili kuwafaa baadhi, na kuwanyanyasa wengine.

Wakati waliopewa wajibu wa kuhakikisha sheria inadumishwa na haki kupatikana wamelaumiwa kwa kiwango kikuu kwa kuchochea ufisadi ndani ya mkondo wa haki, la kujivunia limetokea katika katika kituo cha polisi Maragua katika Kaunti ya Murang’a ambapo Jumatatu watu watatu walitiwa mbaroni wakiwa katika harakati za kukiuka lile la wahenga kuwa “uchungu wa mwana aujuaye ni mzazi.”

Watatu hao ni mume na mkewe na rafiki wa familia ambao walijitokeza katika kituo hicho cha polisi wakiwa wamebeba Sh40,000 za kumhonga Kamanda Cleophas Mangut ili amwachilie kijana wao ambaye alikuwa amenaswa kwa madai ya kumnajisi msichana wa shule.

Kwa mujibu wa kamanda wa Polisi wa kaunti ndogo ya Muranga Kusini Bw Anthony Keter, watatu hao ni mwanamke na mumewe na ambao ni wazazi wa kijana mhudumu wa uchukuzi wa bodaboda anayetuhumiwa kumnajisi mwanafunzi wa shule mojawapo ya upili Maragua.

“Wazazi wa mshukiwa wakiandamana na rafiki wa kifamilia kwa jina Bernard Irungu wa miaka 50 walikusanyika katika mkutano wa njama na hila kwao nyumbani na wakaamua mtoto wao ni spesheli, uchungu wao wa mwana ni spesheli pia, na katika hali hiyo, wakajipa imani kwamba hongo ya Sh40,000 kwa afisa wa polisi ingeweza kuzika uchungu wa mwana wa wazazi wa mwathiriwa wa kitendo hicho kupitia kununua haki isimpe ridhaa,” akasema Bw Keter.

Sasa kumhusu afisa huyu wa polisi kwa jina Mangut ambaye kwa jina maarufu anafahamika kama Bw Juma, katika huduma yake ya polisi kwa mujibu wa faili yake katika makao makuu ya polisi, amejipa nembo ya uadilifu kazini, ukakamavu unaofaa wa kulinda sheria na ambaye mwongozo wake ni kuboresha mazingira katika jamii akilinda maisha na mali. Ni nguzo muhimu katika ile kaulimbiu ya ‘Utumishi kwa Wote’.

Ingawa Bw Mangut alikataa katakata kuongea na mwandishi huyu akisisitiza kuwa mwongozo wa kikazi ni kuwa hana ruhusa ya kuongea na waandishi wa habari, Bw Mohammed Barre akiwa ndiye Kamishna wa Kaunti ya Murang’a alimtaja kama “risasi yetu ya mwisho katika ukosaji wa nidhamu katika mji wa Maragua.”

Bw Barre alikariri jinsi ambavyo mji huo umekuwa ukimtatiza katika shughuli za kudumisha usalama.

“Magenge ya kila aina yalikuwa yamechipuka yakilenga kuthibiti mitaa ya mji kupitia mihadarati na pombe haramu, ghasia na wizi wa kimabavu,” akasema Bw Barre.

Akaongeza: “Ni katika hali hiyo ambapo kwa kipindi cha miezi mitatu tulikuwa tunatapatapa tukisaka suluhu ambapo tulimleta Kamanda Bi Francisca Mbinda na ambaye kwa muda mfupi akaonekana kutokuwa na jibu la kero hiyo, tukamleta Bw Gikunda Mbaya na ambaye pia kwa kipindi cha wiki mbili ilibainika hakuwa na suluhu na ndipo tukamleta Bw Mangut ambaye kwa kipindi cha wiki moja pekee, ilikuwa wazi kuwa ndiye dawa ya mji huu.”

Huyo ndiye Bw Mangut ambaye watatu wale walifika katika kituo chake Jumatatu wakitaka kumwona na walipopishwa katika afisi yake, baada ya kuamkuana na kupiga gumzo kuhusu hili na lile kuunda urafiki, wakatwaa mabunda ya pesa kama ‘chai’ ili mshukiwa aponyoke na aliyetendewa unyama aende labda akajitulize na msemo hasi na “mwenye nguvu mpishe.”

“Noti hizo zilikuwa Sh30,000 zikiwa katika noti moja moja za Sh1,000, ujumla wa Sh7,000 ukiwa noti za Sh500 nazo Sh1,800 zikiwa katika ujumla wa noti za Sh200 na hatimaye Sh1,200 zikiwa za ujumla wa noti za Sh100,” akasema Bw Keter.

Bw Mangut aliwasikiliza na akaigiza kufurahikia jambo hilo na akawaambia wasubiri awaitie afisa aliyekuwa akihusika na kesi hiyo “aipokee sehemu hiyo ya shukrani”.

“Afisa huyo wa kesi aliishia kuwa ni maafisa wa Uchunguzi wa Jinai ambao walifika na kuwatia mbaroni na kisha wakaandikisha taarifa yao kuhusu suala hilo na hatimaye wakafungiwa ndani ya seli. Ikawa mwana yuko ndani ya seli za kituo hicho, wazazi wake wakiwa ndani ya seli hizo kwa madai ya kushabikia uhalifu huo kiasi cha kupanga njama ya kuhonga afisa wa polisi ndio waelekee nyumbani pamoja wakashabikie unyanyasaji wa haki za mwathiriwa,” akasema Bw Keter.

Wote wanawasilishwa mahakamani leo Jumatano kwa mujibu wa Bw Keter.

  • Tags

You can share this post!

AFCON: Atawika nani kati ya Olunga na Mo’ Salah?

CHAWAKAMA KENYA: Kiswahili kwa maendeleo endelevu