• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
CHAWAKAMA KENYA: Kiswahili kwa maendeleo endelevu

CHAWAKAMA KENYA: Kiswahili kwa maendeleo endelevu

Na CHRIS ADUNGO

CHAMA cha Wanafunzi wa Kiswahili katika Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (CHAWAKAMA), kilianzishwa mnamo 2004 kwa lengo la kukuza na kueneza Kiswahili katika eneo la Afrika Mashariki.

Wanachama wa chama hiki ni wale wanaosomea Kiswahili, japo wapenzi wa Kiswahili wanaosomea taaluma nyinginezo vyuoni wanaweza kujiunga nacho.

Mara kwa mara, CHAWAKAMA huandaa makongamano kwa nia ya kuwapa wanachama fursa za kujadili, kuimarisha, kuendeleza na kukuza vipawa vyao vya lugha na fasihi ya Kiswahili, kuamsha ari ya mapinduzi ya utamaduni wa Kiswahili na kueneza Kiswahili ndani na nje ya nchi.

Wao hushirikiana na vyama vingine na asasi mbalimbali zinazojihusisha na ukuzaji na uenezaji wa Kiswahili katika juhudi za kuendeleza Kiswahili na kuwaunganisha wanafunzi wanaosomea Kiswahili hapa Afrika Mashariki na Kati.

CHAKAMA-KENYA ambalo ni tawi la CHAWAKAMA, huchapisha jarida la chama na machapisho mengine ili kusaidia kueneza taaluma za Kiswahili. Aidha, huhifadhi kumbukumbu za wataalamu wa Kiswahili na kuratibu makongamano na mijadala mbalimbali inayohusiana na taaluma za Kiswahili.

Chama huandaa makongamano kila mwaka kwa lengo la kukutanisha wanachama wote katika vyuo mbalimbali nchini. Katika makongamano haya, mada mbalimbali zinazohusu Kiswahili na mustakabali wake hujadiliwa na maazimio mbalimbali kuchukuliwa kuhusu maendeleo ya chama.

Makala mbalimbali huandikwa, huwasilishwa na kuchapishwa kwa minajili ya kusomwa na watu mbalimbali.

Ni miaka 16 sasa ya uhai wa CHAWAKAMA-KENYA. Kwa mujibu wa Paul ‘Bin Bakari’ Baker (Mhariri Mkuu), mnara wa chama umeimarishwa na nguzo tatu kuu: ulezi, kamati tendaji na wanachama kwa jumla.

Kwa sasa Kamati Tendaji Shikilizi ya CHAWAKAMA-KENYA inawajumuisha Josiah Omukuti (Mwenyekiti), Kananu Ruth (Naibu Mwenyekiti), Dominic Oigo (Katibu Mkuu), Emma Njeru Mukami (Naibu Katibu), Bin Bakari (Mhariri Mkuu), Dancan Obwocha (Naibu Mhariri Mkuu) na Alfan Mwatime (Mhazini).

Wengine ni Kevin Wafula (Afisa wa Uhusiano Mwema), Barng’etuny Kemboi (Afisa Mwenezi), Rafael Okoth (Katibu Mtendaji) pamoja na Miriam Shianyisa, Chrispus Mwaponda, Sr Evalin Kimani na Rolvin Nyabiba (wahariri).

Kitengo cha Nidhamu kinasimamiwa na Kevin Juma na Ismael Nandwa.

Chuo Kishiriki cha Turkana, Chuo Kishirikishi cha Bomet, Chuo cha Kiufundi cha Eldoret, Chuo cha Mount Kenya, Chuo Kishirikishi cha Kaimosi ni miongoni mwa vyuo tanzu takriban thelathini vya humu nchini vinavyojivuniwa wanafunzi ambao ni wanachama wa CHAWAKAMA-KENYA chini ya ulezi wa Dkt Sheila Wandera-Simwa wa Chuo Kikuu cha Laikipia.

Licha ya changamoto tele za kila sampuli, Jopo la Uhariri la CHAWAKAMA-KENYA kwa sasa linapiga hatua katika kuhariri hadithi fupi ambazo tayari zimewasilishwa na wanachama kwa minajili ya kuchapishwa kwa hisani ya chama.

Dhamira ya mradi huu ni kulea vipaji vya wanachama hasa katika ulingo wa uandishi wa kazi bunilizi. Mbali na mradi huo, chama pia kina mikakati ya kujipatia Makao Makuu/Afisi Kuu mjini Nakuru.

Kongamano lililokuwa liandaliwe na chama katika Chuo Kikuu cha Embu mnamo Machi 14, 2020 lilitibuliwa na janga la korona baada ya kisa cha kwanza cha maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 kuripotiwa humu nchini mnamo Machi 13, 2020. Tangu wakati huo, chama hakijaandaa warsha au kongomano lolote jingine la kanda au kimataifa.

  • Tags

You can share this post!

Jinsi kamanda wa polisi Maragua alivyokataa Sh40,000 ambazo...

Mechi ya UEFA kati ya Real Madrid na Liverpool kuchezewa...