• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 1:24 PM
Jinsi ustawishaji wa maua na mimea ya kuvutia unavyompa kipato, utulivu wa moyo

Jinsi ustawishaji wa maua na mimea ya kuvutia unavyompa kipato, utulivu wa moyo

Na MAGDALENE WANJA

MNAMO Machi 2019, Bi Marlene Mweru, aliamua kugawa mimea na maua ambayo alikuwa amepanda hapo awali nyumbani kwao ili kuongeza idadi ya mimea hiyo.

Baada ya kazi hiyo, aligundua kwamba mimea hiyo ina uwezo wa kuongezeka hata maradufu iwapo angetilia maanani kazi hiyo.

Mimea hii ilinawiri na baada ya muda mfupi, ilikuwa kivutio kikuu na alipenda kutembelea bustani yake mara kwa mara.

Mmojawapo wa majirani wao nyumbani kwao katika eneo la Kitengela alipowatembelea alifurahishwa sana na baadhi ya mimea ambayo alikuwa nayo na akamuomba amuuzie.

Baadhi ya maua na mimea ya kuvutia ambayo Marlene Mweru anapanda nyumbani kwao. PICHA | MAGDALENE WANJA

Japokuwa Bi Mweru hakua na nia ya kuifanya biashara, aliona hili kuwa wazo zuri na aliamua kuuza huku akivumisha biashara kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.

“Wakati huo nilikuwa nafanya kazi hiyo kama mojawapo ya njia za kujifurahisha tu bila kuwazia kuwa inaweza kuwa nafasi ya kujipa riziki,” alisema Mweru.

Alipata wateja wengi waliokuwa wanahitaji mimea ya aina mbali mbali ya kuweka katika nyumba zao.

Bi Mweru anasema kuwa babake ambaye ni mjuzi katika sekta ya maua (floriculture), alichangia sana katika kuchochea hamu yake ya kukuza mimea na maua.

Baadhi ya maua na mimea ya kuvutia ambayo Marlene Mweru anapanda nyumbani kwao. PICHA | MAGDALENE WANJA

Kazi hii imeweza kumpa faida pamoja na kujifunza zaidi kuhusu mimea.

Kwa mimea midogo, bei yake huwa ni Sh500 huku mimea mikubwa akiuza kwa kati ya Sh4,000 na Sh15,000.

Yeye hununua mimea kutoka kwa wakulima ambao huuza kando ya barabara katika maeneo ya Limuru Road, Ngong Road na Namanga Road.

“Miezi michache iliyopita, nimeweza kupanda mimea yangu mwenyewe kwa kutumia ujuzi nilioupata kutoka kwa shamba langu dogo,” anaeleza.

Bei ya mimea hiyo hutegemea aina ya mmea, chombo alichokitumia kupanda na ukubwa wa mmea.

Marlene Mweru atabasamu akiwa ameshika mkononi chombo chekundu chenye mmea wenye maua ya kuvutia. PICHA | MAGDALENE WANJA

Anasema kuwa anauza mimia kati ya saba na 10 kila mwezi huku akiongeza kuwa idadi hii inaongezeka kila mwezi.

Wateja wake ni pamoja na wamiliki wa hoteli, ofisi mbalimbali na wanaopenda kuweka mimea nyumbani.

Anaongeza kuwa kinachomfurahisha sana na kazi hii ni kuona mimea ikinawiri kila siku kila anapoongeza.

Hata hivyo anasema kuwa changamoto kuu katika kukuza mimea hii ni wadudu wanaoivamia pamoja na magonjwa ya mimea.

Anaongeza kuwa kutokana na utafiti alioufanya, kuwa na mimea nyumbani husaidia sana katika kutuliza mawazo na huleta pia hewa safi na mazingira ya kuvutia.

  • Tags

You can share this post!

Fataki City wakialika Spurs EPL

IEBC: Chebukati atifua kivumbi aking’atuka

T L