• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Julai 7: Siku ya Kiswahili Duniani

Julai 7: Siku ya Kiswahili Duniani

NA CHRIS ADUNGO

KILELE cha kusherehekea Siku ya Kiswahili Duniani katika Chuo Kikuu cha Moi kitashuhudiwa leo Alhamisi mjini Eldoret, wadau watakapodhihirisha umuhimu wa lugha hii kama chombo cha mawasiliano kilichokita katika tamaduni mbalimbali na taratibu za maisha ya kila siku ya Waafrika.

Maadhimisho hayo yanayodhaminiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Chama cha Kiswahili cha Taifa (CHAKITA), Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki (CHAKAMA), Wizara ya Utamaduni na Serikali ya Kaunti ya Uasin Gishu, yalianza jana katika Chuo Kikuu cha Moi (Ukumbi wa PDN).

“Kiswahili kimekua na kupiga hatua kubwa kimaendeleo hadi kufikia kilele cha kutambuliwa na kusherehekewa kimataifa. Juhudi hizi za kukuza na kueneza lugha hii ulimwenguni zilianza Afrika Mashariki zikichangiwa na watu wengi, kila mmoja akiwa na lengo lake,” anasema Prof Evans Mbuthia ambaye ni mwanachama wa CHAKITA.

“Maadhimisho haya yatatoa fursa kwa wapenzi wa lugha kujadiliana zaidi kuhusu mikakati ya kuboresha Kiswahili na wito kutolewa kwa vyuo vikuu kuweka misingi ya kufundisha lugha hii kwa hadhi na viwango vitakavyokabiliana na kasi ya ukuaji wake,” akaongeza Mhariri Mkuu wa CHAKAMA, Prof Mosol Kandagor.

Hafla ya leo itaanza kwa matembezi ya saa moja kutoka nje ya ofisi za Kaunti ya Uasin Gishu hadi Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi (MTRH).

Wakazi wa Eldoret watahamasishwa kuhusu jinsi ya kubidhaaisha kwa Kiswahili na nafasi ya lugha hii katika soko la ajira duniani. Wataburudishwa kwa nyimbo kutoka kwa bendi na kwaya ya Chuo Kikuu cha Moi huku washiriki wakibeba mabango yenye jumbe zinazofungamana na mada kuu ya siku: ‘Kiswahili kwa Amani na Ustawi’.

Zaidi ya wajumbe 200 watakongamana baadaye katika Ukumbi wa PDN kwa ajili ya mawasilisho kutoka kwa wadau mbalimbali wa Kiswahili, akiwemo Prof Ngugi wa Thiong’o. Kikao hicho kitakachohudhuriwa pia na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Moi, Prof Isaac Kosgey, kitafunguliwa rasmi na Gavana wa Uasin Gishu, Bw Jackson Mandago.

“Lengo letu ni kueleza taifa na ulimwengu kuhusu hatua kubwa ambazo Kiswahili kimepiga katika sekta nyingi. Zaidi ya kufundishwa kimataifa, ndiyo lugha ya kwanza ya Kiafrika kutambuliwa na Umoja wa Mataifa (UN) na kutengewa siku maalum ya kuadhimishwa,” akasema Kandagor kwa kusisitiza kuwa huenda hatua hiyo ya UNESCO ikazindua na kuchochea Serikali ya Kenya kuanza mchakato wa kuunda Baraza la Kiswahili.

“Katika siku hii, ni muhimu tuketi pamoja na kukichapukia Kiswahili si kwa maandishi na mazungumzo tu, bali kupitia utajiri wa utamaduni wetu – vyakula, mavazi, mashairi, maigizo, nyimbo, ngoma, densi, hotuba na kumbukumbu za matendo ya magwiji waliotutangulia ili sauti zao na zetu zitande kote ulimwenguni,” akaongeza Dkt Leonard Chacha katika kauli iliyotiliwa mkazo na Katibu wa CHAKITA, Prof Nyehita Maitaria.

  • Tags

You can share this post!

Azma ya Nyamweya yapata pigo baada ya mwenza wake kutoroka

Chimbuko na Asili ya lugha ya Kiswahili

T L