• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
JUMA NAMLOLA: Marufuku yasitumike kuumiza mwananchi wa chini

JUMA NAMLOLA: Marufuku yasitumike kuumiza mwananchi wa chini

Na JUMA NAMLOLA

TANGU serikali itangaze marufuku ya usafiri kutoka eneo moja la nchi hadi jingine, mambo mengi yamebadilika.

Ukiongeza na amri ya kila mtu kuingia ndani ya nyumba kufikia saa mbili za usiku katika kaunti za Nairobi, Kiambu, Kajiado, Machakos na Nakuru, maisha ya Wakenya wengi yamekuwa ya kubahatisha.

Kufunga Nairobi ambacho ni kitovu cha shughuli za nchi ni sawa na kufunga nusu ya nchi. Wamiliki wengi wa mabasi na matatu za masafa marefu husafiri kati ya miji mingine na Nairobi.Mabasi ya kutoka Mombasa kama vile Coast Bus, Mash, Modern Coast, Dreamline, Crown na Tahmeed kati ya mengine yamelazwa kwenye maeneo ya maegesho.

Wale wa magari ya kutoka Migori, Kisumu, Kisii, Kakamega, Bungoma, Mandera, Garissa na kwengine, wanaendelea kukadiria hasara huku maelfu ya watu wakiteseka na familia zao bila ajira.Mabasi hayo huajiri mamia ya watu na kutegemewa na familia nyingi.

Kuyasimamisha yasiendelee na safari bila ya kuwapa wamiliki njia ya kuepuka hasara ni kuumiza uchumi.Baadhi ya wenye magari hayo waliyanunua kwa mikopo na wanatarajiwa wayalipie kila mwezi.

Wapo wafanyibiashara wengine wa kuuza magurudumu, vipuri vingine vya magari, mafuta ya dizeli na petroli, mekanika na wadau wengine walioathiriwa moja kwa moja na hatua hiyo.

Hatusemi kwamba serikali haina haki ya kuwalinda raia wake dhidi ya corona. Inaweza kufanya hivyo kwa njia ambayo haitaathiri maisha ya wananchi.Kama lengo la kuifunga miji kadhaa ukiwemo wa Nairobi lilikuwa ni kupunguza viwango vya maambukizi, basi ni kwa nini serikali haijaongeza kasi ya kuwapima watu?

Hata nchi ikifungwa kwa miaka mingine mitano ijayo, kama hakuna mikakati ya kutambua walioambukizwa ili kuwatenga na walio salama, itakuwa ni kazi bure.

Kinachoshangaza zaidi ni uamuzi wa serikali kuendelea kuacha wazi mipaka na nchi jirani, ambazo hazijaweka mipango kama wetu wa kuagiza raia kuvaa barakoa au kuzingatia kanuni zozote za kupunguza maambukizi.

Isitoshe, ingawa serikali ilijua kuwa India inakumbwa na janga hatari zaid la corona, iliruhusu ndege kutoka Delhi na Mumbai ziendelee kuingia nchini hadi leo Jumamosi.

Kipindi cha saa 72 kinatosha kusambaza corona miongoni mwa wafanyikazi wa viwanja vya ndege na katika hoteli ambako wageni hao watawekwa karantini.Kenya inapoungana na ulimwengu leo kuadhimisha siku ya Wafanyikazi, serikali yapaswa kufikiria upya jinsi ya kufufua uchumi wetu.

You can share this post!

Kaunti yapewa siku 7 kujibu kesi ya wafanyabiashara

Bei ya majanichai imepungua kwa asilimia 12 – KTDA