• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 10:50 AM
Jumwa kupendelea wawaniaji  wa kiume kwaibua gumzo kali

Jumwa kupendelea wawaniaji wa kiume kwaibua gumzo kali

NA MAUREEN ONGALA

MTINDO ambao Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, anatumia kwa kampeni zake kuwania ugavana Kaunti ya Kilifi katika uchaguzi ujao, zimeibua kiwewe miongoni mwa baadhi ya wanasiasa wa kike kaunti hiyo.

Katika kampeni zake siku za hivi majuzi, Bi Jumwa ameonekana akijipigia debe kwa njia ambayo huenda ikashawishi wapigakura kupuuza wanawake wanaowania viti vingine vya kisiasa.

Bi Jumwa amekuwa akieneza hoja kwamba, wapigakura wachague mwanamke, ambaye ni yeye, kuwa gavana kisha viti vingine vya kaunti viendee wanaume isipokuwa kile cha Mbunge Mwakilishi wa Kaunti ambacho kimehifadhiwa wanawake.

Kulingana naye, mtindo wa kupiga kura kaunti hiyo unafaa kuchukua mkondo wa rais mwanamume (William Ruto), gavana wa kike (yeye binafsi), seneta kijana ambaye tayari amemtambua na ni mwanamume, na mbunge mwakilishi wa kike.

Bi Jumwa amekuwa akimpigia debe Bw Shukrani Mwamboje kuwa seneta wa Kilifi.

“UDA ni ya watu wote. Kina mama tuko ndani na vijana pia wamepewa nafasi kutafuta viti,” akasema katika mojawapo ya mikutano yake ya hadhara.

MIJADALA MIKALI

Kauli hizo ambazo zimeibua mijadala mikali baina ya wanasiasa na wakazi wa Kilifi, zimevutia malalamishi hasa kutoka kwa wanawake wanaotaka kuwania useneta.

Baadhi ya wanasiasa eneo hilo wamesema, kauli hizo zake huenda zikafanya wafuasi wake pia kukataa kuchagua wanawake kwenye viti vingine ikiwemo ubunge na udiwani ikizingatiwa kuwa kiti cha ugavana ni kikuu katika kaunti.

Akizungumza na Jamvi, Bi Carolyne Chilango anayepanga kuwania useneta alisema inasikitisha kuwa Bi Jumwa amekuwa akimpigia debe mpinzani wake wa kiume. Bi Chilango ni mwanachama wa UDA.

“Katika chama cha UDA tuko wawili tunaotaka tikiti ya kuwania kiti cha useneta. Lakini Bi Jumwa amekuwa akizunguka katika mikutano ya hadhara na kumpigia debe mpinzani wangu, Bw Shukrani Mwamboje, akidai kuwa ana mbinu ya UDA kushinda katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, ambayo ni kuwa gavana na seneta hawawezi kuwa wanawake,” akasema.

Alisema kuwa alishtushwa na hatua ya Bi Jumwa. Bi Chilango alikashifu kitendo hicho na kusema ni aibu kuwa inatoka kwa kiongozi wa tajiriba yake ambaye amekuwa mstari wa mbele kupigia upato uongozi wa wanawake.

“Ni swala ambalo halistahili kuchukuliwa kwa mzaha ikiwa tuna kiongozi mama ambaye anapinga wazi uongozi wa kina mama,” akasema.

Mwezi uliopita, Bi Chilango alilazimika kujitokeza kupinga madai kwamba alikuwa ameeka kando azimio lake kuwania useneta na badala yake anataka kuwa mbunge mwakilishi wa kike.

Alitoa wito kwa jamii kujitokeza na kupinga hatua ya Bi Jumwa inayotishia kuwafungia nje wanawake katika uongozi.

“Tunaangalia maswala ya uongozi bora na sio maswala ya kuwa mume au mke. Mwananchi wa kawaida ana hamu ya maendeleo na sio ajenda ya jinsia,” akasema.

WATOFAUTIANA KIMAWAZO

Baadhi ya wandani wa Bi Jumwa wamekuwa wakiunga mkono wazo lake, ila kuna wengine ambao waliambia Taifa Jumapili kisiri kwamba wanafanya hivyo tu kwa vile hawataki kukwaruzana na Chama cha UDA lakini wanatofautiana naye kimawazo.

Mmoja wa viongozi wanaoegemea UDA katika Kaunti ya Kilifiambaye aliombwa asitajwe kwa kuhofia kuleta uhasama kati yake na Bi Jumwa, alisema hali hiyo tayari imeanza kutishia nafasi ya wanawake wanaotaka udiwani.

“Tulifahamishwa kuwa wadi ya Kaloleni ina wagombeaji wawili, mwanamke na mwaname (wanoegemea UDA), lakini Bi Jumwa anampigia debe yule wa kiume,” akasema kiongozi huyo.

Aliendelea kusema kuwa baadhi ya viongozi wa chama hicho mashinani wamemuonya Bi Jumwa dhidi ya kuwabaagua wagombea viti kwa sababu za kibinafsi.

“Bi Jumwa hatatuchagulia viongozi. Tutampa kura zake za ugavana lakini aache tuchague viongozi wanaotufaa na sio ambao yeye anawataka,” akasema.

INGIA ODM

Bi Mufida Mohamed, aliyetaka kuwania udiwani Wadi ya Shimo la Tewa, alihama chama cha UDA na kujiunga na ODM kwa kile alichikitaja kuhofia kunyimwa tikiti ya chama.

Bi Mohamed alijulikana kuwa mwanachama sugu wa Jubilee na pia mwandani wa Naibu Rais William Ruto.

Baada ya naibu wa rais kuunda chama cha UDA, Bi Mohamed alianzisha zoezi la kusajili wanachama kupitia vuguvugu la ‘The Hustler Tent’.

Katika mahojiano na Taifa Jumapili, alisema alikufa moyo wakati mpinzani wake wa kiume alipoanza kupigiwa debe.

“Niliamua kutoka UDA kwa sababu nilijua kuwa nitanyimwa tikiti kwa sababu uongozi wa chama kaunti ya Kilifiulikuwa na mtu wake,” akasema.

Baadhi ya wachanganuzi wa kisiasa walisema migogoro inayoibuka kwa misingi ya masuala ya kijinsia huenda ikakomaa hadi kusambaratisha umaarufu ambao chama hicho kilikuwa kimeanza kupata kaunti hiyo.

Kulingana na mchanganuzi wa kisiasa, Bw Kazungu Katana, UDA itapoteza mambo mengi kwa sababu ya usimamizi mbaya unaotenga watu mashinani.

“Inavyoonekana, hakuna mtu mwingine anayeweza kutoa maoni mbadala katika chama wala kumfikja Ruto na viongozi wengine wa juu. Sasa watu wamekimbia,” akasema.

Aliendelea kusema kuwa baadhi ya wakazi wa Kilifiwalikuwa washashawishika kujitenga na ODM na kufanya uamuzi wa kujiunga na chama cha UDA lakini viongozi wa mashinani wameshindwa kuimarisha chama hicho.

“UDA ilikuwa katika nafasi nzuri ya kuchukua nafasi ya ODM kwa sababu hakuna chama kingine cha nguvu katika Kaunti ya Kilifi,” akasema Bw Kazungu.

Kulingana naye, ingekuwa vyema kama chama kingetafuta jinsi ya kufanya isionekane kwamba Bi Jumwa ndiye UDA na UDA ni yeye katika Kaunti ya Kilifi.

Hii ingesaidia kuondoa dhana ya kuwa chochote anachosema ndicho msimamo wa chama.

  • Tags

You can share this post!

Mchujo: ODM yazidi kujiponza

Tammy Abraham aweka rekodi ya ufungaji mabao Serie A

T L