• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Mchujo: ODM yazidi kujiponza

Mchujo: ODM yazidi kujiponza

NA CHARLES WASONGA

HATUA ya chama cha ODM kukumbatia mfumo wa uteuzi unaoipa uzito tafiti za kura za maoni ndio inachangia wanachama wakuu wa ODM kugura chama hicho na wengine kuogopa kujiunga nacho.

Wiki hii, chama hicho kimempoteza mwanachama mkongwe Sam Ongeri ambaye alihamia chama cha Democratic Action Party of Kenya (DAP-K). Hiki ni mojawapo ya vyama tanzu katika vuguvugu la Azimio la Umoja na linaunga mkono waziri mkuu wa zamani Raila Odinga, katika kinyang’anyiro cha urais Agosti 9.

Duru ziliambia safu hii kwamba Profesa Ongeri ambaye amekuwa akisaka tiketi ya ODM kusudi awanie kiti cha ugavana wa Kisii, alichukua hatua hiyo baada ya kupata habari kwamba chama hicho kimeamua kutoa tiketi hiyo kwa mpinzani wake, Simba Arati.

Inasemekana kuwa Bw Arati ambaye ni Mbunge wa Dagoretti Kaskazini ndiye aliibuka mwenye ushawishi mkubwa kulingana na matokeo ya kura ya maoni iliyoendeshwa na ODM mwezi jana.

Kwenye mahojiano na safu hii, mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi (NEB) ya chama cha ODM Catherine Mumma alisema chama hicho hakitaharibu rasilimali zake kwa kuandaa kura ya mchujo katika maeneo ambapo kura za maoni zimeonyesha kuwa mgombeaji fulani ndiye bora zaidi.

“Aidha, hatutaki wagombeaji fulani kupoteza fedha na rasilimali zao zingine kuendesha kampeni kisha kushiriki kura ya mchujo ilhali kura za maoni zinaonyesha kuwa hawana ushawishi tosha kuwawezesha kushinda,” Dkt Mummo akaeleza.

Mnamo Desemba mwaka jana, kiongozi wa ODM Raila Odinga alipendekeza kuwa kura ya maoni itatumika kama mbinu mbadala wa kuteua wagombeaji “ili kuzuia migongano wakati wa kura za mchujo.”

“Mbinu zingine ambazo tutatumia katika mchujo ni; maelewano, kutoa tiketi ya moja kwa moja na matumizi ya wajumbe. Kura ya mchujo itatumika endapo tutahisi kuwa mbinu hizi zingine zitafeli,” Bw Odinga akasema katika makao makuu ya ODM Nairobi alipowapokea wanasiasa waliojiunga na chama hicho kutoka vyama vingine.

Lakini baadhi ya wafuasi wa ODM wanapinga mbinu hiyo ya kura ya maoni wakisema sio hauzingatii haki.

“Swali langu ni je, ni watu wangapi huhojiwa katika kura hizo za maoni? Pili, nini inaonyesha kuwa wale ambao walihojiwa ni wanachama halisi wa ODM,” akasema Bw John Mogaka ambaye ni mfuasi wa ODM kutoka Kisii.

“Ni ukosefu wa majibu ya maswali haya ambao umechangia mwanachama mkongwe kama Mzee Ongeri kuhama ODM na kujiunga na DAP-K ili kutimiza ndoto yake ya kuwa gavana wa Kisii,” akasema mwanasiasa huyo ambaye anawania udiwani katika Wadi ya Nyakoe.

Mwanasiasa mwingine kutoka ngome ya ODM ya Nyanza kujiunga na chama kingine cha kisiasa kwa kuhofia mfumo huo wa uteuzi kupi – tia kura za maoni ni aliyekuwa Mbunge wa Rongo, Dalmas Otieno.

Wiki jana, mwanasiasa huyo mwenye uzoefu mkubwa ambaye aliwahi kushikilia nyadhifa za uwaziri katika serikali zilizopita, aliamua kujiunga na chama cha Jubilee.

“Kwa heshima ya Rais Uhuru Kenyatta na kakake mkubwa Raila Odinga, leo nimeamua kujiunga na Azimio la Umoja kupitia chama ca Jubilee. Nitatumia tiketi ya chama hichi tawala kuwania ugavana wa Migori katika uchaguzi mkuu ujao,” akasema alipopokelewa rasmi na Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni.

Duru ziliambia Jamvi kwamba kando na Kisii, kura za maoni zilizoendeshwa katika kaunti ya Migori na Kisumu zilibaini kuwa Seneta Ochilo Ayacko na Gavana Anyang’ Nyong’o, mtawalia ndio wana umaarufu mkubwa. Inasemekana kuwa ni wao ambao watapewa tiketi za kuwania ugavana katika kaunti hizo.

  • Tags

You can share this post!

Huenda Uhuru asiweze kudhibiti ‘Rais Raila’

Jumwa kupendelea wawaniaji wa kiume kwaibua gumzo kali

T L