• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
KAMAU: Siasa zina uwezo mkuu wa kuijenga au kuibomoa jamii

KAMAU: Siasa zina uwezo mkuu wa kuijenga au kuibomoa jamii

Na WANDERI KAMAU

MSINGI kamili wa siasa huwa ni ushirikiano na mwingiliano wa idara mbalimbali za utawala katika usuluhishaji wa changamoto zinazoiathiri jamii.

Hilo ndilo lilidhihirika wakati mifumo tofauti ya kisiasa ilianza kujitokeza wazi na kutumika kwenye majukwaa ya kiusomi katikati mwa karne ya 15 nchini Ugiriki.

Ni mchipuko uliowachochea wasomi na wanafalsafa kama Aristotle kuanza kuandika vitabu kuhusu uhalisia, maana na fasiri kamili kuhusu maana ya siasa katika jamii.

Kando na Aristotle, midahalo hiyo pia iliwachipuza wasomi wengine kama Nicollo Machiavelli, ambao walijaribu kufafanua jinsi nchi zinaweza kustawisha mifumo yake ya kisiasa kwa manufaa ya raia.

Katika juhudi za kujaribu kujibu swali hilo, Aristotle aliandika kitabu ‘Politics’ (Siasa), mwenzake Plato akaandika ‘Republic’ (Taifa Huru) huku Machiavelli akiandika kitabu maarufu kiitwacho ‘The Prince’ (Mwanamfalme).

Juhudi hizo zilizua migawanyiko mikubwa ya kifalsafa na kiusomi.

Kuna wale walioamini demokrasia kama mfumo bora zaidi wa kukuza siasa, huku wengine wakiamini ukomunisti au ujamaa kama njia bora ya kuhakikisha usawa katika mataifa husika.

Mitazamo hiyo ilizua midahalo zaidi ya kiusomi. Wale walioshabikia ukomunisti waliendeleza mawazo yao, wakiusifia kama mfumo pekee ambao ungeziba tofauti za kitabaka na kimapato kati ya watu maskini na wale matajiri.

Miongoni mwa wasomi waliousifia mfumo huo ni Karl Marx na Friendrich Engels kupitia kitabu ‘The Communist Manifesto’ (Manifesto ya Ukomunisti/Ujamaa) kilichochapishwa mnamo 1848. Marx pia aliukashifu vikali mfumo wa kibepari kwenye kitabu ‘Das Kapital’ (Ubepari).

Bila shaka, midahalo hiyo yote inaonyesha kuwa siasa ni kigezo na nguzo kuu ya ustawi wa jamii yoyote ile.

Ni kutokana na umuhimu huo ambapo ilizua hisia na midahalo mizito, kiasi cha wasomi na watu maarufu kuweka mawazo yao kwenye vitabu na majarida.

Vivyo hivyo, siasa zinaweza kugeuka kuwa mkasa na mkosi mkubwa katika jamii, ikiwa viongozi husika watakosa kuzingatia na kuziendeleza ifaavyo.

Midahalo hiyo inapaswa kuwafungua macho wananchi na viongozi kuwa, taifa halistawi kwa msingi wa mfumo wa kisiasa linaloegemea, bali kuhusu namna viongozi husika wanavyouendesha.

Hivyo, haijalishi ikiwa tunazingatia demokrasia, ubepari ama ukomunisti—kilicho muhimu ni aina ya viongozi tulio nao.

Ni wakweli ama ni wanafiki? Wanatii sheria ama wafisadi?

Ni mahayawani ama ni wenye utu? Hilo ndilo jibu kuu kwa uwepo wa siasa endelevu.

[email protected]

You can share this post!

Kibwana, spika kupokea maoni kuhusu BBI

MUTUA: Valentino: Tutahadhari tunapoiga mila za kigeni