• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 3:16 PM
MUTUA: Valentino: Tutahadhari tunapoiga mila za kigeni

MUTUA: Valentino: Tutahadhari tunapoiga mila za kigeni

Na DOUGLAS MUTUA

UKITAKA ithibati kwamba dunia imekuwa kijiji kimoja, tazama jinsi watu wanavyojiandalia ‘Siku ya Wapendanao’ ambayo inaadhimishwa kesho kote duniani.

Ithibati ya kwanza kabisa jinsi biashara ya maua ilivyoshika kasi Kenya na kwingineko Afrika, wapenzi wakionyeshana wanavyopendana.

Hiyo haikuwa desturi ya Mwafrika miongo michache tu iliyopita, wala haukuwa utamaduni wake kwenda njiani akiwatangazia watu kwamba anapendwa au anampenda mtu.

Ni desturi ya kigeni iliyoingia Afrika na kubadilisha maisha yetu kimchezo tu na sioni ikiondoka, hivyo ni sharti tujifunze kuishi nayo.

Haina maana kwamba awali hatukujua kupenda, la hasha! Tulipenda kimyakimya, zaidi kwa vitendo.

Leo ndoa ya Mwafrika ikiingia msukosuko unaweza kusikia mtu akilalamika kwamba hapendwi! Inachekesha kidogo.

Zamani hata lilikuwa jambo tukizi mno kumsikia mzazi akimwambia mwanawe anampenda.

Ajabu iliyoje kwamba leo utamsikia mtu mzima akilalamika eti babake au mamake hakuwahi kumwambia waziwazi anampenda.

Kwanza enzi hizo eti baba akwambie anakupenda? Huko ni kuota mchana, ndoto ikashindikana kuagulika. Au kukosa mambo muhimu ya kufikiria.

Enzi hizo ishara ya mapenzi ilikuwa zawadi zisizo ghali sana kati ya wapendanao, mume kuyakidhi mahitaji ya mkewe, kuwalisha na kuwavisha watoto wao, nao wakimtii, wala haikutengewa siku.

Kisa kinahadithiwa cha Mwafrika aliyehamia uzunguni kabla ya ‘Siku ya Wapendanao’ kupata umaarufu Afrika.

Aliposikia kuihusu akadhani ni kitu kizuri kumuonyesha mapenzi mchumba wake wa kizungu kwa kumnunulia maua.

Muuzaji alipomwambia ni kiasi gani, yule bwana alidhani ni ghali mno, akajaribu kupiga bei kwa kusema ‘haya ukienda kwetu Afrika hayauzwi, yanajiotea ovyo porini’.

Mwafrika wa watu alitukanwa vibaya na kuambia akayachume porini kwao na kumletea mpenzi wake, ‘huku ni uzunguni, si Afrika!’

Kisa kingine kinahadithiwa cha Mwafrika aliyelazwa hospitalini uzunguni, mpenzi wake wa kizungu akampelekea shada la maua na kuliweka mezani kimyakimya.

Baada ya kumuuguza mgonjwa wake na kupiga soga naye kuhusu mambo mengi tu, yule mpenzi wa kizungu aliondoka bila kusema chochote kuhusu maua aliyoleta. Ndiyo desturi yao wazungu, huelezwi maua ni ya nini kwa sababu unapaswa kujua.

Siku iliyofuata alipokwenda kumwona mpenzi wake tena hospitalini, Mwafrika wa watu alinyanyuka kitandani alipomwona akiingia mlangoni akamwambia: Samahani sana, ulisahau maua yako hapa nami sikukukumbusha’!

Hayo yalitokea mbele ya watu. Kisichana cha kizungu kilimpa tabasamu tu kwa kuwa kilijua ni tofauti ya tamaduni zao.

Sasa mambo yamebadilika sana. Mwafrika, hasa anayeishi mjini, ameiga tabia za kizungu hivi kwamba, japo hazielewi vyanzo vyake, huwezi kumsadikisha aachane nazo.

Kwa mfano, Krismasi inavyoadhimishwa siku hizi sivyo ilivyoadhimishwa miongo kadhaa iliyopita.

Ni Waafrika wachache mno walioutambua ‘Mti wa Krismasi’ na maana yake kwa sababu hautajwi popote kwenye Biblia takatifu.

Wala hawakuijua hekaya ya babu wa kizungu kwa jina Santa Claus anayesawiriwa akibebwa kwa kigari kinachobururwa na swara, eti akiwapelekea watu zawadi.

Leo Mwafrika ananunua ‘Mti wa Krismasi’ na kuupamba kweli kweli akisubiri siku yenyewe.

Sawa na anavyofanya mzungu, mzazi wa kiafrika ameanza kudanganya wanawe kwamba wasipokuwa na nidhamu, basi Santa Claus hatawaletea zawadi. Inachekesha!

Wakenya wameanza hata kusherehekea ‘Siku ya Halloween’ ambapo Wamarekani huvaa mavazi ya kuogofya eti kumshtua shetani, nao Wamexico husherehekea pepo za wafu!

Kuiga si kubaya, lakini mwenzangu ukiiga tumia akili. Mathalan, kuiga mahanjam ya wapendanao uzunguni ni kitu kizuri.

Kuna vinyago vya kuogofya vilivyozuiwa na Mamlaka ya Ushuru Nchini (KRA) vikiingizwa Kenya mnamo 2013 kisha vikatoweka kimyakimya. Vilikuwa vya sherehe ya Halloween iliyopangiwa kufanyika eneo la Village Market, Nairobi.

Nasikia siku hizi hata baa za mashoga ni nyingi jijini Nairobi, Mombasa na Kisumu, sikwambii nyingine ambako watu hukaa uchi na wateja hulipia kuwaona na kuwapapasa!

Hivi tutaiga mpaka lini? Kuiga si kubaya, lakini mwenzangu ukiiga tumia akili. Mathalan, kuiga mahanjam ya wapendanao uzunguni ni kitu kizuri.

[email protected]

You can share this post!

KAMAU: Siasa zina uwezo mkuu wa kuijenga au kuibomoa jamii

TAHARIRI: Yafaa tuwaruhusu mashabiki viwanjani