• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
KAULI YA WALLAH BIN WALLAH: Tanzania yaadhimisha siku ya Kiswahili Duniani kwa namna ya kipekee Afrika Mashariki

KAULI YA WALLAH BIN WALLAH: Tanzania yaadhimisha siku ya Kiswahili Duniani kwa namna ya kipekee Afrika Mashariki

NA WALLAH BIN WALLAH

LEO Alhamisi ninapoyaandika makala haya nipo jijini Darisalama Tanzania kwa mwaliko rasmi niliotumiwa na Dkt Consolata Mushi, Katibu wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKIZA) nijumuike na ndugu Watanzania kuadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani.

Katika ualishi wake, Dkt Mushi alinidokezea kwamba kwenye kilele cha maadhimisho haya leo katika Ukumbi wa Mikutano ya Kimataifa wa Julius Nyerere kutakuwa na shamrashamra za maonesho ya Kiswahili. Kutakuwa na ngoma, mashairi, ngonjera, hotuba za wadau wa Kiswahili wa taasisi mbalimbali na serikali. Aidha, watu mbalimbali waliojitolea kidedea kukitetea Kiswahili nchini Tanzania na katika nchi nyinginezo watatuzwa.

Wazalendo wa Watanzania bara na visiwani walizindua shamrashamra za kujiandaa kuikaribisha siku ya Kiswahili tangu tarehe 3 Julai ambapo matembezi ya shangwe na nderemo yalirindima jijini Darisalama. Matembezi haya yalianzia Temeke na kupokelewa na Waziri wa Katiba na Sheria kwenye uwanja wa Uhuru.

Usiku wa kuamkia tarehe 4 kulikuwa na burudani ya tamasha za Mkesha wa Utamaduni wa Taarabu. Hafla hii ilipeperushwa hewani mubashara kupitia televisheni ya Shirika la Habari Tanzania TBC usiku kucha!

Ndugu wapendwa, nahitimisha kwa kuwapongeza kwa dhati wapenzi wote wa Kiswahili duniani, mashirika, vyama vya Kiswahili, nchi zinazotumia Kiswahili pamoja na kila mtu aliyeonyesha nia au aliyesherehekea Siku ya Kiswahili Duniani.

Ninatumaini kwa neema zake Mungu, siku zijazo maadhimisho yatakuwa makubwa zaidi kote ulimwenguni! Amina.

  • Tags

You can share this post!

SIKU YA KISWAHILI DUNIANI: Maadhimisho ya hafla ya...

Saba saba: Maadhimisho ya ‘Siku ya Kiswahili...

T L