• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 11:53 AM
SIKU YA KISWAHILI DUNIANI: Maadhimisho ya hafla ya Kiswahili janibu mbalimbali ughaibuni

SIKU YA KISWAHILI DUNIANI: Maadhimisho ya hafla ya Kiswahili janibu mbalimbali ughaibuni

NA WANDERI KAMAU

ULIMWENGU mzima unapoungana leo kuadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani, itakuwa hatua muhimu sana katika historia ya lugha hii.

Ni mara ya kwanza kwa Kiswahili kusherehekewa duniani tangu kutengewa siku yake maalum na Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) mnamo Novemba 23, 2021.

Maadhimisho hayo yatakuwa ya kipekee nchini Canada, baada ya jimbo moja kutenga Julai 2 hadi Julai 9 kuwa “Juma la Jamii ya Waswahili.”

Kwenye notisi, gavana wa jimbo la British of Columbia, Canada, alisema kuwa sherehe hizo zitakuwa na lengo la “kupiga jeki juhudi za UN kukitambua Kiswahili.”

Nchini Amerika, ambayo ni moja ya mataifa ambako Kiswahili hufunzwa pakubwa katika vyuo vikuu vyake, wasomi wanasema wataandaa sherehe za kufana kusherehekea ufanisi huo.

Baadhi ya vyuo hivyo ni Chuo Kikuu cha California (Los Angeles), Wisconsin-Madison, Pennysylvania kati ya vingine vingi.

CHAUKIDU

Kwa mujibu wa Bw Hezekiel Gikambi ambaye ni mwanachama wa Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU), vyuo vingi barani Afrika, Ulaya na kwingineko vitakuwa vikiendesha sherehe hizo kwa njia ya mtandao huku vingine vikiziendesha kwa njia ya ana kwa ana.

Katika mahojiano Jumatano, Bw Gikambi alieleza kwamba ijapokuwa taasisi nyingi zimekutwa zikiwa hazijajitayarisha vilivyo, bado kutakuwa na mikakati ya kuendeleza sherehe hizo hata baada ya leo Alhamisi.

“Vyuo vingi katika sehemu tofauti bila shaka vimeweka mikakati kuendeleza sherehe hizi. Huu ni ushindi mkubwa sana kwa juhudi ambazo zimekuwa zikiendelezwa kuinua hadhi ya Kiswahili kote duniani,” akasema Bw Gikambi.

Nchini Tanzania, asasi kuu ya kukuza Kiswahili huko – Chama cha Kitaifa cha Kiswahili (CHAKITA) – pia itakuwa kwenye mstari wa mbele kuendeleza maadhimisho hayo katika sehemu tofauti nchini humo, kama vile miji ya Dar es Salaam na Dodoma.

Profesa Ndirangu Wachanga, aliye mhadhiri wa Lugha za Kiafrika katika Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison, Amerika, anasema kuwa chuo hicho kitaandaa hafla za mtandaoni na ana kwa ana kuitambua lugha hiyo.

“Kwa jumuiya ya Waswahili duniani, siku hii inafanana na wakati mataifa ya Afrika yalipata uhuru wao kutoka kwa wakoloni. Ni ushindi mkubwa kwa Afrika,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Sababu za UNESCO kuteua siku ya Kiswahili duniani

KAULI YA WALLAH BIN WALLAH: Tanzania yaadhimisha siku ya...

T L