• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 2:07 PM
KAULI YA WALLAH: Ukitaka ufanikiwe zaidi sharti uwe mwanafunzi bora si bora mwanafunzi

KAULI YA WALLAH: Ukitaka ufanikiwe zaidi sharti uwe mwanafunzi bora si bora mwanafunzi

NA WALLAH BIN WALLAH

UKWELI ni kwamba kila mtu aliye tayari kujifunza mahali popote ni mwanafunzi.

Lakini kwa vijana wetu, mahali pao mahususi pa kujifunzia ni shuleni au vyuoni.

Kuitwa mwanafunzi ni kazi rahisi sana mradi tu uwe umekubali kufunzwa na kujifunza ili upate elimu na maarifa maishani!

Lakini ukitaka kuwa mwanafunzi bora wala si bora mwanafunzi, sharti upige hatua tofauti za kujihimu kuzingatia maadili yafuatavyo!

Kwanza, mwanafunzi bora anapaswa kujua madhumuni halisi ya kuwa shuleni badala ya kumangamanga tu shuleni!

Sharti awe mwenye nidhamu na kutii kanuni za shule pamoja na kuwaheshimu walimu wake, wazazi, wanafunzi wenzake na wafanyakazi wote shuleni!

Mwanafunzi bora hufanya kazi zote za darasani na za ziada kwa wakati unaofaa na huuliza maswali yanayomkanganya!

Kisha hushirikiana na walimu na wanafunzi wenza katika shughuli muhimu za shuleni bila uzembe.

Mwanafunzi bora husoma kwa mapana na marefu akirejelea kazi za darasani huku akiongezea mazoezi na marudio kwa kufuata ushauri na maelekezo ya mwalimu ili asipotoke na kusoma mambo ambayo hayaambatani na silabasi anayofunzwa!

Mwanafunzi bora huvaa vizuri kila mara; hapotezi muda; huwasikiliza walimu wake kwa makini; husema nao kwa nidhamu bila kiburi wala ujeuri! Na huomba msamaha akikokosea!

Aidha hujitahidi kusoma bila kukata tamaa ili afanikiwe katika mtihani na maishani!

Huyo ndiye mwanafunzi bora wala si bora mwanafunzi.

You can share this post!

FASIHI SIMULIZI: Fasili, sifa, dhima na aina za ngomezi

NDIVYO SIVYO: Ubashiri hautokani na anachokijua msomaji

T L