• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:46 PM
Kenya, Uholanzi kwenye ushirikiano wa kuboresha kilimo cha viazi mbatata nchini

Kenya, Uholanzi kwenye ushirikiano wa kuboresha kilimo cha viazi mbatata nchini

Na SAMMY WAWERU

KENYA ina aina 64 ya viazi mbatata, 34 kati yavyo vikitoka katika nchi ya Uholanzi.

Serikali ya Kenya inasema ongezeko hilo la viazi linatokana na ushirikiano wa karibu kati ya Kenya na Uholanzi katika sekta ya kilimo, kwa muda wa miaka 10 sasa.

Uholanzi ndiye mzalishaji mkuu wa mbegu za viazi mbatata ulimwenguni, ikikadiriwa asilimia 55 ya mbegu zilizoidhinishwa (sawa na tani 800,000 kwa mwaka) na asilimia 55 zilizoimarishwa, zinazotumika kote duniani zimetoka nchini humo.

“Kwa sababu ya ushirikiano wetu wa karibu na Uholanzi kwa muda wa miaka 10, hususan katika uzalishaji wa mbegu, Kenya sasa ina aina 64 ya viazi mbatata, 34 kati yavyo vikitoka nchini humo. Vinajumuisha vile vya kupika na kuongeza thamani,” akasema Katibu katika Wizara ya Kilimo, Mifugo na Samaki Prof Boga Hamadi katika hafla ya maadhimisho ya Sikukuu ya viazi mbatata Duniani 2021.

Huku viazi vikiorodheshwa kama mojawapo ya zao muhimu hasa uzalishaji wa chakula, ni vya pili bora kusheheni wanga baada ya mahindi.

Naibu Balozi wa Uholanzi nchini Kenya, Joris van Bommel (kushoto) na Katibu katika Wizara ya Kilimo, Mifugo na Samaki Prof Boga Hamadi katika hafla ya maadhimisho ya Siku ya viazi mbatata duniani 2021. Picha/ Sammy Waweru

Prof Boga alisisitiza haja ya Kenya kujiimarisha katika uzalishaji, kutokana na manufaa yake.

Akisifia ushirikiano wa Kenya na Uholanzi, Katibu alisema uzalishaji wa Kenya unawiana na mazao yanayotoka nchi jirani ya Tanzania.

“Mikakati tuliyoweka kama serikali, inalenga kuboresha na kuongeza kiwango cha mazao kupitia kuwepo kwa mbegu bora ili kujaza pengo dogo lililopo la uzalishaji,” akasema.

Uholanzi na serikali ya kitaifa, inashirikiana na serikali za kaunti kuzindua miradi inayolenga kuongeza uzalishaji, kupitia mifumo na teknolojia ya kisasa, Nakuru na Meru zikiwa za kwanza kunufaika.

Majuzi, Waziri wa Kilimo (CEC) Kaunti ya Nakuru, Dkt Immaculate Maina na Balozi wa Uholanzi hapa Kenya, Bw Maarten Brouwer walizindua tovuti ya Agrico Potato Service Africa.

Ni mtandao wa wakulima wa mapato ya chini na ya kadri katika sekta ya ukuzaji viazi, utakaowawezesha kuboresha biashara zao, kukutana na wanunuzi na pia kupata mafunzo ya kilimo bora bila kutozwa ada.

Tovuti hiyo iliasisiwa na Agrico East Africa mwaka wa 2012, na inayoenda sambamba na mikakati ya serikali kuimarisha usalama wa viazi nchini, Uholanzi ikiipiga jeki.

Huku mabadiliko ya tabianchi yakiathiri shughuli za kilimo, hali ya anga ikikosa kutabirika, Naibu Balozi wa Uholanzi hapa Kenya, Bw Joris van Bommel, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya viazi alisema vyuo vikuu vya Uholanzi vinashirikiana na watafiti wa Kenya kuibuka na mbegu za viazi zitakazostahimili athari za mabadiliko ya anga.

“Licha ya kuwa tunajaribu kuongeza kiwango cha mazao, vilevile tunaibuka na mbegu mpya na teknolojia za kisasa, ambazo zitastahimili athari za mabadiliko ya tabianchi kama vile kiangazi, mkurupuko wa wadudu na magonjwa,” Bw Bommel akaelezea, akidokeza wanashirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo cha Mimea na Uimarishaji Mifugo (Karlo) na ile ya Mbegu na Ustawishaji wa Mimea (Kephis).

Maadhimisho ya Siku ya viazi mbatata duniani hapa nchini, katika hafla iliyoandaliwa jijini Nairobi, kitabu chenye mwongozo na mafunzo ya ukuzaji kilizinduliwa.

Kitabu hicho ‘Potato Signals Africa, kinafafanua kimatendo safari nzima ya ukuzaji viazi, kuanzia mbegu, upanzi, utunzaji, mavuno na kuhifadhi mazao.

“Kinaelezea kwa njia ya kuvutia, picha na michoro, ambapo unatazama dalili za athari kwa viazi, unazitathmini na kuchukua hatua,” Bw Bommel akasema.

Balozi huyo alisema kilitungwa na kubuniwa na wataalamu wa Uholanzi pamoja na wa Kenya.

Kina nakala ya Kiingereza na Kiswahili, na pia kinapatikana mitandaoni.

You can share this post!

Lady Doves ya Uganda yaanza Cecafa kwa kulipua FAD ya...

West Ham wamtwaa beki Kurt Zouma kutoka Chelsea kwa Sh3.9...