• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 3:16 PM
WASONGA: Ni wazi, Ruto ndiye aliye na nafasi kubwa kumrithi Uhuru

WASONGA: Ni wazi, Ruto ndiye aliye na nafasi kubwa kumrithi Uhuru

Na CHARLES WASONGA

UKWELI ni kwamba miongoni mwa wanasiasa ambao wanatamani kuingia Ikulu baada ya Rais Uhuru Kenyatta kustaafu, Naibu Rais William Ruto ndiye aliye na nafasi bora ya kupata mamlaka hayo endapo uchaguzi ungeitishwa sasa.

Hii ni kulingana na darubini yangu binafsi kuhusu hali ya kisiasa nchini haswa wakati kama huu ambapo kuna dhana kwamba umaarufu wa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga umeshuka zaidi.

Sababu ni kwamba Wakenya wengi wanahisi kwamba mchakato wa mageuzi ya katiba jinsi ilivyopendekezwa kwenye ripoti ya mpango wa maridhiano ni njama ya wawili hao kumzima kisiasa Dkt Ruto kwa manufaa yao ya kibinafsi.

Kwa hivyo, amani na utulivu nchini, haswa katika ngome ya kisiasa Dkt Ruto ya Rift Valley, ni yenye faida kubwa zaidi kwa mwanasiasa huyu kwani itamwezesha kufanikisha ndoto yake ya kuwa Rais wa Kenya baada ya bosi wake kustaafu mwaka ujao. Hali hii pia itafaidia wanasiasa wandani wa Naibu Rais ambao watafaidi kwa kutunukiwa nyadhifa serikali endapo atashinda urais 2022.

Lakini matukio mawili ya utovu wa usalama yaliyoshuhudiwa wiki jana katika kaunti za Nandi na Uasin Gishu huenda yakavuruga mipango ya kisiasa ya Naibu Rais ikiwa hatachukua hatua za haraka kuyazima.

Kwanza ni kisa cha Jumamosi ambapo makundi ya vijana yalizua vurugu na kumzuia Seneta wa Baringo Gideon Moi kufika nyumbani kwa naibu mwenyekiti wa baraza la wazee wa Talai Christopher Koyogi, kijiji cha Kipsisiywa, kaunti ya Nandi ya kutawazwa kuwa msemaji wa jamii ya Kalenjin.

Pili, ni vijikaratasi vyenye jumbe ya kuchochea chuki na uhasama kwa kuwataka wakazi wasio wenyeji kuondoka Uasin Gishu kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022. Vijikaratasi vilisambazwa katika eneo la Kipkaren na watu wasiojulikana.

Lakini kilichonishangaza kuhusu kisa cha kwanza ni kwamba Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen alisema kitendo cha vijana hao kilikuwa sawa kwa sababu “Gideon pia aliwazuia watu kuona babake (marehemu Daniel Moi).”

Kauli ya Bw Murkomen ambaye ni mshirika wa karibu wa Dkt Ruto inaonyesha kuwa ni wao waliwakodi vijana hao kuvuruga mipango ya Seneta Moi ambaye pia ni mwenyekiti wa Kanu. Ina maana kuwa kama wandani wa Dkt Ruto walikuwa wakilipisha kisasi kisa cha Aprili 2019 ambapo jaribio lake (Ruto) la kukutana na marehemu Moi ziligonga mwamba licha ya kuwasili Kabarak.

Ikiwa ni kweli Naibu Rais anataka kuingia Ikulu 2022, anapasa kuondoa dhana kuwa ni kiongozi ambaye ni mwepesi wa kulipisha kisasi dhidi ya mahasidi wake wa kisiasa.

Kwa hivyo, anapasa kuwadhibiti wanafuasi wake kama vile Murkomen wenye ndimi za kuchochea chuki. Vile vile, ahakikishe kuwa amani na utulivu inadumu katika ngome yake ya Rift Valley.

You can share this post!

TAHARIRI: Walimu ndio kinga yetu dhidi ya corona shuleni

KIKOLEZO: Maji yazidi unga!