• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Kilio cha Wakenya waliobamizwa ukutani na bei ya juu ya mafuta

Kilio cha Wakenya waliobamizwa ukutani na bei ya juu ya mafuta

Na SAMMY WAWERU

HUKU viongozi na wanasiasa mbalimbali wakiendelea kutoa maoni kuhusu nyongeza ya bei ya mafuta wiki iliyopita, Wakenya wanazidi kulemewa na gharama ya maisha.

Mamlaka ya Kusimamia Sekta ya Kawi Nchini (Epra) ilitangaza ongezeko la Sh7.58 kwa petroli, mafuta ya dizeli na ya taa yakipanda kwa Sh7.94 na Sh12.97 mtawalia kwa kila lita .

Kufuatia kupanda huko kwa bei, petroli sasa inauzwa Sh134.72 kwa lita jijini Nairobi na viunga yake.

Lita moja ya dizeli jijini inagharimu Sh107.66 na mafuta taa ambayo hutegemewa na Wakenya wenye mapato ya chini ikiuzwa Sh110.82, kila lita.

Mfumuko wa bei ya bidhaa hiyo, umesababisha gharama ya maisha kupanda mara dufu, mwananchi wa mapato ya chini akiumia.

Bei ya bidhaa hasa za kula na nauli, imeanza kukwea mlima licha ya changamoto zilizopo kufuatia janga la Covid-19.

Wanaotegemea sekta ya juakali, na ambayo inawakilisha zaidi ya asilimia 75 ya nguvukazi nchini, nyongeza ya bei ya petroli imetishia utendakazi wao.

Simon Muchangi, mhudumu wa tuktuk eneo la Githurai 45, amesema sekta hiyo ya uchukuzi imeanza kupoteza wateja kutokana na jaribio la kutathmini nauli.

“Nyongeza ya Sh10 kwa kila mteja kuona iwapo tutagawana gharama ya mafuta imesukuma abiria kutafuta njia mbadala kuenda kazini na kurejea nyumbani,” Bw Muchangi akasema, akidokeza kwamba wengi wao wanaafadhalisha kutembea miguu.

Katika mahojiano na Taifa Leo, Bw Rustus Matia mfanyakazi wa vibarua vya ujenzi Zimmerman, Nairobi, alisema pindi nyongeza ya bei ya mafuta ilipotolewa ada ya usafiri anakoishi ilipanda mara moja.

Bw Rustus Matia ambaye ni mwashi anayetegemea kazi za ujenzi eneo la Zimmerman, Kaunti ya Nairobi. Aliambia Taifa Leo kwamba kupanda kwa bei ya mafuta kunaongeza mzigo kwa Mkenya wa kipato ya chini. Picha/ Sammy Waweru

“Iliongezeka kwa Sh20. Safari niliyokuwa nikilipa nauli ya Sh100 kuenda kazini, ikawa Sh120,” Bw Matia akasema.

Mkenya huyo anayetegemea vibarua vya ujenzi na anavyohoji havipatikani kwa urahisi, anasema mapato yake kwa siku ni Sh1, 500.

“Vinapatikana mara tatu kwa wiki. Mapato hayo ndiyo kodi ya nyumba, chakula, karo, matibabu, nauli na kukidhi familia mahitaji mengine muhimu ya kimsingi,” akasema baba huyo wa watoto sita, akilalamikia nyongeza ya bei ya mafuta wiki iliyopita.

“Nilikuwa nikitumia gesi kufanya mapishi, ila ilipoengezwa bei nikageukia makaa na mafuta ya taa. Mafuta yaliyokuwa nafuu sasa hayanunuliki,” akalia.

Perkins Agola, ambaye pia hufanya kazi ya mjengo Zimmerman analalamikia ugumu wa maisha, kufuatia ongezeko hilo.

“Sijui nitakavyoweza kukidhi familia yangu riziki na mahitaji mengine muhimu, kupitia ujira wa Sh600 kwa siku,” akateta, akiiomba serikali kutathmini bei ya petroli.

Ni baba wa watoto watatu, na hutegemea mafundi wa majengo kupata vibarua.

Baadhi ya wabunge wamedai wakirejelea vikao vya bunge juma hili, watajadili suala la ongezeko la bei ya mafuta.

Yalianza kutozwa ushuru 2018, baada ya wabunge haohao kupitisha mswada kuyaruhusu kulipiwa VAT.

Aidha, bei ya mafuta kwa kawaida hutathminiwa kila mwezi kuongezwa au kupunguzwa.

You can share this post!

WARUI: Tukumbatie changamoto za CBC ili utekelezaji uwe...

Maafisa wanne wa polisi wanaoshtakiwa kwa mauaji ya wakili...