• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Maafisa wanne wa polisi wanaoshtakiwa kwa mauaji ya wakili Willy Kimani

Maafisa wanne wa polisi wanaoshtakiwa kwa mauaji ya wakili Willy Kimani

Na RICHARD MUNGUTI

MAAFISA wanne wa polisi wa utawala wanaoshtakiwa pamoja na kachero kwa mauaji ya wakili Willy Kimani miaka mitano iliyopita wako na kesi ya kujibu.

Jaji Jessie Lessit alitoa uamuzi huo baada kupokea ushahidi wa watu 46.Jaji Lessit aliyekamilisha kupokea ushahidi Ijumaa wiki iliyopita alisema kila mmoja wa watano ataingia kwenye kisimba kujitetea.

Jaji Lessit aliamuru watano hao waanze kujitetea Septemba 27, 2021.Walioshtakiwa kwa mauaji ya Kimani , mteja wake Josephat Mwenda na dereva wa teksi Joseph Muiruri ni Inspekta Fredrick Lelimani, Koplo Stephen Cheburet Morogo, Konstebo Sylvia Wanjiku Wanjohi ,Koplo Leonard Maina Mwangi pamoja na Bw Peter Ngugi.

Katika uamuzi aliotoa jana Jaji Lessit alisema kuna ushahidi wa kutosha kuwezesha mahakama kuwaagiza watano hao kujitetea.“Baada ya kuchambua ushahidi wote uliowasilishwa na upande wa mashtaka hii mahakama imefikia uamuzi kila mmoja wenu yuko na kesi ya kujibu katika mauaji ya kimani , Mwenda na Muiruri,” Jaji Lessit alisema.

Kesi hiyo iliongozwa na wakili wa Serikali Bw Nicholas Mutuku.Leliman , Morogo, Mwangi , Wanjiku na Ngugi wanakabiliwa na mashtaka ya kuwaua Kimani , Mwenda na Muiruri  usiku wa Juni 23/24, 2016 katika eneo la Soweto Mlolongo kaunti ya Machakos.

Maiti za watatu hao zilipatikana zimetupwa katika mto Athi River eneo la Donyo Sabuk kaunti ya Machakos baada ya wiki moja.Walikuwa wameripotiwa wamepotea.Watatu hao walitekwa nyara wakitoka katika mahakama ya Mavoko ambapo Mwenda alikuwa ameshtakiwa kwa kupatikana na bangi na kuwabeba abiria zaidi kwa pikipiki yake.

Jaji Lessit alielezwa kulikuwa na uhasama kati ya Leliman na Mwenda kutokana kesi hizo mbili.Leliman ndiye alikuwa afisa mchunguzi wa kesi hizo.Pia jaji alielezwa Leliman alikuwa amempiga risasi mguuni Mwenda.

Mwenda alikuwa amemripoti Lelimani kwa mamlaka huru ya kusimamia idara ya polisi (IPOA) na alikuwa anachunguzwa.Kila mmoja wa washtakiwa hao, alieleza mahakama ataapishwa na kutoa ushahidi akiwa upande wa mashtaka.

Mashahidi 21 wataitwa na washtakiwa hao.Miongoni mwa mashahidi watakaofika kortini ni pamoja na maafisa wakuu wanaosimamia vituo vya Polisi vya Makindu na Mlolongo.

Jaji huyo aliwaamuru mawakili Cliff Ombeta , James Mochache na Kevin Michuki Wachira wamkabidhi msajili wa mahakama majina na anwani za mashahidi wao ndipo wapelekewe samanzi wafike kortini wiki ijayo.

Jaji huyo aliyeteuliwa kuwa Jaji wa mahakama ya rufaa kisha akapewa idhini na Jaji Mkuu Martha Koome asikize na kukamilisha kesi hiyo ya mauaji kabla ya kuanza majukumu yake mapya katika mahakamka hii ya pili kwa ukuu nchini.

  • Tags

You can share this post!

Kilio cha Wakenya waliobamizwa ukutani na bei ya juu ya...

NCIC yachunguza kisa cha Wanjigi kupigwa mawe alipozuru...