• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 5:50 AM
KIPWANI: Asema ‘views’ si hoja, bora muziki mzuri

KIPWANI: Asema ‘views’ si hoja, bora muziki mzuri

NA SINDA MATIKO

MWANADADA Laurriete Rota sio tu mwanamuziki anayetokea Pwani na hususan Mombasa, lakini pia yeye ni mwanasaikolojia.

Majina yake ya usanii ni Larota Africa na muziki anaoufanya sio wa Kipwani Pwani, ila ni Afro-Soul, Afro-Fusion na vitu kama hivyo.

Nafasi ilitokea ya sisi kupiga stori, nami nikaona isiwe kesi kuwapasha haya.

Toka umeanza muziki una miaka mingapi sasa ?

Minne sasa nikifanya muziki kitaaluma zaidi.

Kwako unafanya muziki kusaka riziki au kujibamba?

Riziki jambo la msingi kwa yeyote, kwa hiyo hilo lipo. Lakini pia kwa sababu napenda muziki, kujibamba inakuwa ni sehemu yake pia.

Nimegundua wasanii wengi Pwani hupiga shoo zao laivu hasa kwenye mahoteli, je, wewe utaratibu wako wa kutumbuiza upoje?

Ninapiga shoo za laivu vile vile ila sio mahotelini peke yake bali pia katika hafla au sherehe za kampuni tofauti tofauti.

Kingine kinachonisikitisha ni kuwa wasanii wengi wa Pwani hamwonekani mkichangamka sana kuzisukuma kazi zenu? Kwa mfano unakuta ngoma ni kali ila haina ‘views’ YouTube, tatizo nini?

Ujue kila msanii anao wasikilizaji na wakati wake, wawe wengi au wachache. Ni kama tu vile mwanamuziki kutoka Nigeria alivyowahi kusema, tunaimba muziki tofauti tofauti kwa hivyo huwezi tarajia mtu ambaye anapenda Jazz, asikilize sana Gengetone.

Umenizungusha sana ujue na sina uhakika kama umejibu swali.

Biashara matangazo ni jambo la muhimu sana kwenye karne hii ya utandawazi. Na ndio maana unawaona wasanii wakubwa bado wanasukuma nyimbo zao mpya kwa kuziweka kama matangazo ya YouTube ambayo ni gharama kubwa. Lakini kubwa zaidi, sio ishu ya ‘views’. Ni mara ngapi tumewaona wasanii wakishinda tuzo za Grammys wakati kazi zao hazina ‘views’ kibao?
La msingi ni kuendelea kupambana kuachia muziki mzuri.

Muziki ni gharama kuanzia na vikao vya studio hadi kushuti video. Ukizingatia wewe ni msanii unayeibukia, mtaji wako wa kusukuma muziki ni upi?

Mtaji wangu unatokana na zile zile shoo za hapa na pale ninazopata na pia mashabiki kupakuwa muziki wangu kutoka kwenye tovuti tofauti tofauti za kupakua na kupakia muziki.

Shoo sawa ila hiyo mitandao ya upakuaji nyimbo najua bado haijaanza kulipa vizuri Kenya, kwa hiyo kidogo nahisi umenizengua.

Hayo ya kwako. Lakini pia nina biashara kando na muziki kwa sababu sio kila wakati utapata pesa unavyotarajia kutoka kwa muziki wako.

Halafu staili yako ya muziki ni tofauti sana na wasanii wengine wa Kipwani, unachanganya staili tofauti tofauti, ndio mpango kazi wako au?

Staili yangu ni moja tu nayo ni Afro-Fusion. Lakini nachanganya wakati nina wazo nataka kupitisha kupitia muziki. Kwa mfano kama umegundua, nikiimba Reggae, basi ni nyimbo za afya ya kiakili ama za kuwapa watu motisha. Siwezi kusema ni mpango kazi, ila najua wasikilizaji nao pia wanapenda kusikiliza ladha tofauti.

Kwenye ‘Okay’ pale umefanya RnB, ukija kwenye ‘Uno’ kuna vionjo vya Singeli, Dala na Benga, sio wasanii wengi wapo hivi. Je, mtindo huu umekufaidi?

Eeeh! Tena pakubwa sana, sababu nikienda kwenye tamasha tofauti ninaweza kuimba kwa kutegemea na hadhira lengwa. Kwa mbinu hii nimefanikiwa kuifikia hadhira kubwa yenye tofauti kiumri na ladha ya muziki. Huku Mombasa, Uno ndio inapendwa sana ila Nairobi ni Okay na Dala.

Kwa staili hii unayoifanya, hivi umewazia kuhamia Nairobi kunako soko kubwa kama mastaa wengine kina Otile, Masauti, Jovial?

Kwa sasa hapana, maisha yangu yapo huku Mombasa nilikolelewa na kusomea. Kama ni kuuza muziki Nairobi na kwingineko, tutafanya hivyo tukiwa Mombasa. Isitoshe, Nairobi si ni ya muda wa saa moja tu kutoka hapa kwa usafiri wa pipa, presha ya nini sasa?

Kwa hiyo huoni haja ya kuwa karibu zaidi na soko lako (Nairobi) ambalo unasema unapokea shoo nyingi?

Haijalishi unakoishi kwani hata huku tunawasikiliza wasanii kutoka majuu, kama vile Marekani na wala hatujawahi kuwaona wakija huku kusukuma muziki wao.

Unahisi Larota anakwama wapi kwenye muziki wake, kwa sababu kama ni kuimba na kutunga mashairi, yupo vizuri sana?

Sioni kama nakwama. Naona nikipiga hatua. Ndio mwanzo najiandaa kuachia albamu yangu iitwayo Dala yenye nyimbo 11.

Lini?

Wakati wowote mwezi huu.

Haya mwana.

Poa poa!

  • Tags

You can share this post!

KIKOLEZO: Azidi kuchafua hewa Twitter

Gavana Sakaja aanza mbio kutekeleza agizo la mke wa Rais

T L