• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
KIKOLEZO: Azidi kuchafua hewa Twitter

KIKOLEZO: Azidi kuchafua hewa Twitter

NA SINDA MATIKO

TAJIRI nambari moja duniani Elon Musk ameendelea kuchafua hewa pale Twitter baada ya kukamilisha ununuzi wa App hiyo kwa dola 44 bilioni pesa taslimu.

Dola 13 bilioni ni mikopo kutoka kwa mabenki. Na ili kulipa mikopo hiyo anayotakiwa kuwa akilipa dola 1 bilioni kila mwaka, Musk katangaza tozo mpya Twitter ambayo ilianza kutekelezwa Jumatano wiki hii.

Tayari ameshasababisha baadhi ya watu maarufu kutangaza kuwa wataachana na App hiyo kufuatia mabadiliko aliyosema analenga kuleta kwenye Twitter.

Whoopi Goldberg, Toni Braxton, Shonda Rhimes, Gigi Hadid ni baadhi tu ya mastaa ambao tayari wamejiondoa Twitter toka Musk awe mmiliki.

Wote hao, wamemkashifu kwa kuleta udikteta kwenye App hiyo ikiwemo kutangaza kuwa sasa watumizi watatakiwa kulipia kuitumia.

“Nimefuta akaunti yangu ya Twitter leo. Kwa muda mrefu na haswa baada ya usimamizi mpya kushika hatamu, imekuwa dimbwi la chuki na ubaguzi na hivyo sitaki kuhusishwa nayo,” juzi kasema Gigi Hadid.

Huku wengi wakielezea kutofurahishwa na hatua hiyo, Musk kagandia pale pale akisisitiza kuwa ni lazima watu walipe. Anasema Twitter imekuwa ikipata hasara kwa miaka minane mfululizo na yeye anapania kubadilisha hilo.

Mabadiliko mengine aliyoahidi ambayo huenda yakawachukiza watu zaidi au yakawafurahisha ni kama vile;

Tozo ya dola 8 (Sh974)

Kwa sasa watumiaji wa Twitter Blue wanalipa dola 4.99 (Sh607) kila mwezi, kiasi ambacho anapania kukiongeza maradufu hadi dola 8 (Sh975).

Ingawaje ni watumiaji wa US ndio watatakiwa kulipa dola nane, Musk kasema maeneo mengine watatengenezewa bei zao kulingana na uchumi wa nchi husika.

Watumizi wa Twitter Blue wanafaidi mambo kadhaa kuliko wenzao wanaotumia Twitter ya kawaida. Twitter Blue haina usumbufu wa matangazo, pia mtumiaji ana uwezo wa kusahihisha posti akishaposti kinyume na ilivyo Twitter ya kawaida.

Aidha Twitter Blue ni thabiti hivyo kudukuliwa sio rahisi. Na kama akaunti ikiblockiwa, mtumiaji anapewa fursa ya kwanza kushughulikiwa. Vile vile watumiaji wa Twitter Blue wanaweza kuposti video ndefu zaidi hadi kufikia dakika 10 ikilinganishwa na dakika mbili ya watumiaji wa akaunti ya kawaida.

Blue tick kuja upya

Kutokana na kila mtumiaji kutaka kuwa na blue tick inayoashiria kuwa mhusika kathibtishwa – ‘verified’, raundi hii haitakuwa rahisi kama zamani.

Musk kasema kwa sasa timu yake inafanya ukarabati ili kuja na utaratibu mpya wa kuwapa watu blue tick hasa wale wenye akaunti za kawaida.

Kwa watumiaji wa Twitter Blue, kupata Blue Tick itakuwa rahisi. Mtumiaji yeyote atakayejisajilisha kutumia blue tick, moja kwa moja akaunti yake itakuwa ‘Verified’.

Na wale ambao tayari wanazo blue tick, watatakiwa kuingia kwenye mpango wa kulipia kila mwezi au wapokonywe beji hiyo muhimu sana inayotumiwa kuonyesha ushawishi na umaarufu wa mtu.

Mabadiliko Twitter Blue

Aidha kutakuwa na mabadiliko kwenye Twitter Blue. Watumiaji hawatakuwa wakikutana na matangazo kama ilivyo kwenye Twitter ya kawaida.

Aidha kuna mpango wa kuiwezesha Twitter Blue kupakia video ndefu zaidi kutoka dakika 10 za sasa hadi dakika 42. Twitter ya kawaida itasalia na video zake fupi zisizozidi dakika 2.

Kurefusha Twiti

Watumiaji wengi wa Twitter watakuambia utamu wa App hiyo ni uhuru mdogo wa kutwiti posti ndefu. Musk ameshaweka wazi kuwa hilo pia wanalifanyia kazi lengo likiwa ni kupanua uwezo wa kuposti twiti ndefu zaidi.

Majina halisi kutumika

Watumiaji watatakiwa kutumia majina yao kamili na ikiwa mtumiaji atanuia kutumia jina tofauti mbali na lake halisi, basi atatakiwa kuweka hilo wazi.

Kutokana na hilo, mtumiaji mwenye blue tick hatatakiwa kubadilisha jina, na kama akiamua kubadilisha jina, basi ataipoteza beji hiyo. Hivyo ili kuipata tena, atatakiwa kulipa upya.

You can share this post!

KASHESHE: Amwaga povu zito

KIPWANI: Asema ‘views’ si hoja, bora muziki mzuri

T L