• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:07 PM
KIPWANI: Eti katulia ila umkutapo studio, ni balaa!

KIPWANI: Eti katulia ila umkutapo studio, ni balaa!

NA SINDA MATIKO

SIJUI kama unamjua Sai Kenya. Nitakwambia baadhi ya watu maarufu wanaomfahamu.

Yupo Marioo yule Mtanzania mwenye hiti ya Mi Amor aliyomshirikisha Mkenya Jovial. Halafu yupo Mwasiti, staa mkubwa tu wa Bongo Flava. Kuna pia Babu Tale, meneja wake Diamond Platnumz na mbunge wa Morogoro Kijijini. Wapo wengine wetu tu, pia mimi namfahamu.

Sababu moja hadi imewapelekea hawa na wengine wengi kumfahamu Sai ni zile ‘cover’ nyingi za nyimbo kadhaa hiti alizofanya hasa za Bongo. Sio siri Sai ana sauti ya kuimba. Ndio sababu yupo chini ya mwavuli wake produsa Shirko. Ni kwa misingi hii, ilibidi nimtafute sista tupige stori. Utaniruhusu nikupe vipande tulipokuwa mkekani.

Hivi Sai una majina mengine?

Niite Grace Msafiri. Sai Kenya ni majina ya usanii. Nimezaliwa na kuelelewa Tudor, Mombasa, ndio nyumbani. Ndiko iliko amani yangu.

Kwenye Insta wajiita Maasai Empress, yule naye nani sasa?

Kila binadamu ana pande zake mbili. Msafiri na Maasai ni mtu mmoja lakini bado ni watu wawili tofauti. Msafiri ni yule binti wa nyumbani, katulia anapenda kuwa mwenyewe muda mwingi. Halafu sasa yupo huyo Maasai Empress, umkutapo studio ni balaa. Hanyamazi, ni mchangamfu, anapenda kuimba na kuongea sana. Hicho ndicho unachopata unapochanganya damu ya Mtaita na Maasai.

Halafu ‘cover’ nyingi ulizofanya mbona tu za Wabongo, Wakenya una nini nao?

Halafu usinichonganishe wewe! Wakati naanza kufanya ‘cover’ nilianza na ngoma za Bongo, sio kwamba nilikuwa nachagua mimi ila menejimenti yangu ndo ilikuwa inateua. Hili walifanya makusudi kwa sababu sikuwa na uimbaji mzuri na nyimbo za Bongo zilikuwa zinanitatiza hivyo ili kunifua, ikabidi ziwe hizo. Ila sasa hivi nipo vizuri sana, mwanzo nimerekodi kolabo na Mkenya. Ndio kolabo yangu ya kwanza sema bado hatujaiachia.

Hivi hizo ‘cover’ zimekusaidia?

Eeeh! Hivi hujanipata niliposema zimesaidia kuboresha uimbaji wangu? Lakini pia zimenisaidia kujulikana, kwa mfano kava yangu ya kwanza Raha, ambayo ni ngoma yake Marioo, sasa hivi inakaribia views milioni moja. Huo ndio wimbo ulionipa umaarufu kiasi cha haja, ukawafanya watu kama Diamond Platnumz, Ben Pol, Barnaba, Hamisa, kunitambua. Nimefanikiwa kuzungumza nao na hilo sio jambo dogo kwangu sababu lilinipa matumaini ya kutoboa kwenye gemu hii. Kumbuka nina miaka mitatu tu kwenye gemu.

Wanasema kufanya ‘cover’ ni rahisi kuliko tungo za mwenyewe?

Hao kina nani? Hivi ni wasanii? Sababu msanii yeyote atakwambia kuufanya wimbo wa mtu mwingine sio rahisi kama inavyoonekana. Ni lazima mwanzo ule wimbo uupokee kama wako na ujitahidi kuimba kwa kuzingatia kuwa haupotezi ule uhalisia wa kazi. Sasa kwenye wimbo wako, una uhuru wa kufanya chochote utakacho sababu wewe ndiye unayeelewa unachotaka kuimba.

Kwa miaka mitatu hiyo changamoto ulizokumbana nazo ni kama zipi?

Sio rahisi kusema kweli. Muziki ni mgumu sana na ishu kubwa ni fedha. Muziki unahitaji mtu kuwa na hela. Ndio maana nimekuwa kimya kwa sasa kwa muda na sio kwa sababu ninataka iwe hivyo ila ni kwa sababu mambo kwa sasa kimfuko hayapo vizuri. Ila tunapambana tu.

Aah! Basi ndio sababu kazi ya mwisho umeachia miezi tisa iliyopita?

Alehandro ndio ngoma yangu ya mwisho kutoa na kama nilivyokuambia, inanigharimu vitu vingi kuja kufanikisha kazi moja.

Kwa nini ukaamua Shirko na wala sio produsa mwingine?

Mwanzo ni produsa mkali sidhani kama hili lina pingamizi. Lakini pia napenda anavyoamini katika kipaji changu kuliko ninavyojiamini mimi. Huwa ananisukuma sana. Chini yake naona ubora wangu ukitanda.

Gemu imekufunza nini?

Kwenye tasnia hii usiwe mjeuri au kiburi sababu hujui unakutana na nani, na anaweza kuja kukufaa vipi. Usiwadharau watu wawe ni wasanii ibukia au mastaa sababu kila mtu anayo hadithi yake. Pia kuwa msikivu wa mawaidha ila yafanyie kazi yale chanya.

Muziki unafanya kama kazi au kujibamba?

Kwangu mimi muziki ni taaluma, kama kipaji ninacho siwezi kuepuka hivyo nachukulia sanaa hii kwa uzito na uzingatiifu mkubwa. Natagemeaa muziki kusukuma maisha.

Habel Kifoto mmoja wa waasisi wa bendi ya Maroon Commandos, una ukoo naye?

Kwa wajomba wangu wote niliojaliwa kupata, huyu ndiye nilimhusudu sana, Mwenyezi Mungu aendelee kuirehemu nafsi yake. Kila nikimkumbuka moyo wangu unapasuka. Tulitengeneza kumbukumbu za kutosha sababu kila tulipokuwa tukikutana ungedhani ni watoto vile. Tungepiga kelele sana, tungeimba sana, yani tulijua kufurahishana, natamani angelikuwa hai leo.

Moja ya mawaidha yake uliobeba?

Kwamba niwe mtu wa kujiamini, nisikubali kuzamishwa na chambo za watu na nipende kuomba sana. Sifa hizi zimenibeba.

Haya sista baadaye?

Sawa bwana, ila kwa maswali hayo bora uwe promota wangu sasa.

You can share this post!

Mgombea aahidi kufufua Mumias

KIKOLEZO: Walirejea baada ya kustaafu!

T L