• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Kituo cha afya kilichotelekezwa Nyeri

Kituo cha afya kilichotelekezwa Nyeri

Na SAMMY WAWERU

WAKAZI wa Wakamata, Karatina, Kaunti ya Nyeri wanalalamikia kuendelea kupuuzwa kwa kituo cha afya cha serikali kinachowahudumia eneo hilo.

Kituo cha afya cha Wakamata ndicho tegemeo kwa wenyeji kupata huduma za matibabu, ila hakina vifaa vya kutosha.

Kikiwa cha jengo moja pekee, kuna mengi yanayokosa kama vile maabara faafu ya kufanya vipimo, sehemu maalum ya wagonjwa kusubiri kuhudumiwa, chumba cha kupima virusi vya Ukimwi, kati ya mahitaji mengine muhimu ya kimatibabu.

Isitoshe, hakina chumba maalum cha dawa, jambo ambalo linazua wasiwasi kuhusu matibabu yanayofanyika.

Zahanati ya Wakamata iliyoko Kaunti ya Nyeri. Picha/ Sammy Waweru

“Hakina sehemu ya huduma za uzazi. Kina mama wanaohitaji huduma za dharura kujifungua aidha wapelekwe mji wa Nyeri au Karatina,” Bw Shimba Njohe akaambia Taifa Leo.

Mji wa Karatina na Nyeri, i kilomita kadhaa kutoka eneo hilo.

“Tukipata visa vya dharura, wakazi huhangaika,” mwenyeji huyo akalalamikia kutelekezwa kwa kituo hicho, akiiomba serikali kusaidia kukiimarisha.

Kando na kituo hicho kukosa vifaa na sehemu maalum, pia kinahitaji wahudumu wa kutosha, wakiwemo wauguzi, maafisa kliniki na madaktari.

Miundomsingi kama vile barabara vilevile inapaswa kuimarishwa, kutokana na hali yake mbovu.

“Serikali itusaidie kuboresha barabara zinazoelekea katika kituo cha afya cha Wakamata,” akaomba mkazi mwingine.

Aidha, kituo hicho ki mkabala mwa Shule ya Msingi ya Wakamata.

You can share this post!

Argentina na Chile waambulia sare ya 1-1 kwenye Copa America

Slovakia washangaza Poland kwa kuipokeza kichapo cha 2-1...