• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Argentina na Chile waambulia sare ya 1-1 kwenye Copa America

Argentina na Chile waambulia sare ya 1-1 kwenye Copa America

Na MASHIRIKA

LIONEL Messi alifunga bao kupitia mpira wa ikabu na kusaidia Argentina kusajili sare ya 1-1 dhidi ya majirani zao Chile kwenye makala ya 47 ya kipute cha Copa America mnamo Jumatatu usiku nchini Brazil.

Baada ya kufunga bao hilo katika dakika ya 33, Messi alitoa heshima zake kwa aliyekuwa jagina wa soka nchini Argentina, Diego Maradona ambaye aliaga dunia mnamo Novemba 2020 akiwa na umri wa miaka 60.

Hata hivyo, juhudi za Messi zilifutwa na fowadi mzoefu Eduardo Vargas aliyesawazishia Chile kwa kuelekeza langoni mpira uliokuwa umetemwa na kipa wa Argentina baada ya kupangua penalti ya Arturo Vidal katika dakika ya 57.

Kabla ya kipenga cha kuashiria mwanzo wa mechi hiyo kupulizwa, Maradona alikumbukwa kwa na wanasoka pamoja na benchi za kiufundi za vikosi vyote viwili huku taa za kisasa zenye rangi mbalimbali zikiwashwa na kutoa mwanga mkubwa ugani.

Aidha baadhi ya video fupifupi za Maradona akichezea Argentina wakati wa fainali za Kombe la Dunia za 1986 zilionyeshwa.

Bao la Messi dhidi ya Chile lilikuwa lake la 73 ndani ya jezi za Argentina.

Argentina walishuka dimbani wakijivunia rekodi ya kutoshindwa katika mchuano wowote tangu 2019. Hata hivyo, wanafainali hao wa Kombe la Dunia na Copa America mnamo 2014 na 2019 hawajawahi kutia kapuni taji la Copa America kwa takriban miaka 30 iliyopita. Miamba hao walitawazwa mabingwa wa kipute hicho kwa mara ya mwisho mnamo 1993.

Ingawa hivyo, Argentina wamejisuka upya na wanajivunia mwamko mpya chini ya mkufunzi Lionel Scaloni tangu wabanduliwe mapema na Ufaransa kwenye fainali za Kombe la Dunia za 2018 nchini Urusi. Mikoba yao ilikuwa ikidhibitiwa na kocha Jorge Sampaoli wakati huo.

Argentina almaarufu La Albiceleste, ndio wanaopigiwa upatu wa kuongoza kampeni za Copa America kutoka Kundi B ambalo pia linajumuisha Uruguay, Paraguay na Bolivia.

Kwa upande wao, Chile walijibwaga ulingoni wakilenga kuendeleza ubabe uliowashuhudia wakiwalazimishia Argentina sare ya 1-1 mnamo Juni 4 katika mchuano wa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar.

Sare nyingine ya 2-2 ambayo Argentina walilazimishiwa na Colombia mnamo Juni 9 katika mechi ya kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia ilimaanisha kwamba masogora hao wa kocha Scaloni walipepetana na Chile bila kushinda mchuano wowote mwaka huu wa 2021.

Chile kwa upande wao walikuwa na kiu ya kutia kibindoni taji la tatu la Copa America baada ya kutawazwa mabingwa mnamo 2015 na 2016.

Licha ya miaka mitano kupita tangu wanyanyue taji la mwisho la Copa America, kikosi cha kwanza cha Chile hakijabadilika pakubwa huku Alexis Sanchez wa Inter Milan nchini Italia na Vargas wa Atletico Mineiro nchini Brazil wakisalia tegemeo kubwa katika safu ya mbele.

Claudio Bravo wa Real Betis nchini Uhispania bado anatamba katikati ya michuma ya Chile wanaotegemea maarifa ya mabeki Gary Medel na Mauricio Isla kwenye idara ya ulinzi.

Licha ya ukubwa wa umri wa baadhi ya wanasoka wanaounga kikosi chake cha kwanza, kocha Martin Lasarte amesisitiza kuwa atazidi kuwawajibisha kwa sababu mashabiki wanaamini kuwa ndio walio na uwezo wa kupokonya Brazil ufalme wa Copa America mwaka huu wa 2021.

Baada ya kuambulia sare ya 1-1 dhidi ya Argentina mwanzoni mwa Juni 2021, Chile walisajili matokeo sawa na hayo dhidi ya Bolivia mnamo Juni 9 katika mchuano mwingine wa kufuzu kwa Kombe la Dunia.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Leicester City kuvunja benki ili kumsajili Coutinho kutoka...

Kituo cha afya kilichotelekezwa Nyeri