• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Kutimuliwa kwa kaimu Jaji Mkuu Philomena Mwilu kuna athari kadha

Kutimuliwa kwa kaimu Jaji Mkuu Philomena Mwilu kuna athari kadha

Na CHARLES WASONGA

AGIZO la Mahakama Kuu ya Meru kwamba Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu ni sharti akome kuhudumu kama Kaimu Jaji Mkuu kutasambaratisha mpango wa uajiri wa Jaji Mkuu mpya kuchukua pahala pa Jaji David Maraga ambaye alistaafu mnamo Januari 12, 2021, baada ya kutimu umri wa miaka 70.

Tume ya Huduma za Idara ya Mahakama (JSC) tayari imeanza mpango huo kwa kuwataka wanaohitimu kutuma maombi kabla ya Februari 10.

Kwenye notisi katika gazeti rasmi la serikali lililochapishwa mnamo Januari 18, Jaji Mwilu, katika wadhifa wake kama Kaimu Jaji Mkuu, alitangaza nafasi hiyo kuwa wazi na kutoa nafasi kwa wanasheria waliohitimu kuanza kutuma maombi.

Kando na wadhifa wa Jaji Mkuu, JSC pia iliwataka wanasheria kutuma maombi ya kujaza nafasi ya Jaji wa Mahakama ya Juu kuchukua pahala pa Prof Jackton Boma Ojwang aliyestaafu Februari 2020 baada ya kutimu umri wa miaka 70.

Wanasheria wanaotaka wadhifa huo wamepewa muda wa hadi Februari 10 kuwasilisha maombi na baadaye JSC itachukua muda wa siku 28 kuchambua maombi hayo.

Jaji Mwilu ndiye mwakilishi wa Mahakama ya Juu katika JSC na anatarajiwa kutekeleza wajibu mkubwa katika uamuzi wa ni nani atakayejaza nafasi hizo mbili; Jaji Mkuu na Jaji wa Mahakama ya Juu.

Endapo utekelezaji wa uamuzi wa Ijumaa uliotolewa na Jaji P. J. Otieno katika Mahakama Kuu ya Meru hautabatilishwa, utendakazi wa Mahakama ya Juu utaathirika kwa sababu itasalia na majaji wanne pekee.

Lakini Katiba inasema kuwa Mahakama hiyo sharti iwe na angalau majaji watano ili iweze kutekeleza majukumu na kutoa maamuzi yatakayokuwa na uhalali wa kisheria.

Kuondoka kwa Mwilu sasa kutamaanisha kuwa Mahakama ya Juu itasalia na majaji Mohammed Ibrahim, Smokin Wanjala, Isaac Lenaola na Njoki Ndung’u pekee.

Miongoni mwa kesi zitakazoathirika endapo Mwilu ataondolewa ni ombi ambalo liliwasilishwa na mabunge ya kaunti za Kericho na Nandi kuhusu uhalali wa mchakato wa marekebisho ya Katiba kupitia BBI.

Jaji Mwilu alihudumu kama wakili kwa miaka 32 kabla ya kuteuliwa kama Jaji wa Mahakama Kuu.

Baadaye alipandishwa cheo hadi kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa kabla ya kuteuliwa Naibu Jaji Mkuu kuchukua nafasi ya Kalpana Rawal.

You can share this post!

AC Milan wapepeta Bologna katika Serie A licha ya Zlatan...

Levante waduwaza Real Madrid kwa kuichapa 2-1 kwenye mechi...