• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 8:50 AM
LISHE: Faida za maziwa ya ngamia

LISHE: Faida za maziwa ya ngamia

NA MARGARET MAINA

[email protected]

KWA karne nyingi, maziwa ya ngamia yamekuwa chanzo muhimu cha lishe hasa miongoni mwa jamii za kuhamahama katika mazingira magumu kama jangwani.

Sasa maziwa hayo yanauzwa kibiashara katika nchi nyingi, na pia yanauzwa kama poda au yakiwa yamegandishwa.

Maziwa ya ngamia yana virutubisho vingi muhimu kwa afya kwa ujumla.

Linapokuja suala la kalori, protini, na wanga, maziwa ya ngamia yanalinganishwa na maziwa ya ng’ombe.

Hata hivyo, yana kiwango kidogo cha mafuta na hutoa vitamini C zaidi, vitamini B, kalsiamu, chuma na potasiamu.

Pia ni chanzo kizuri cha mafuta yenye afya, ambayo yanaweza kusaidia afya ya ubongo na moyo.

Ni chaguo bora kwa watu wasiostahimili maziwa ya ng’ombe. Baadhi ya watu wanapotumia bidhaa za maziwa ya ng’ombe hupata uvimbe, huendesha, na pia huhisi maumivu ya tumbo.

Zaidi ya hayo, maziwa ya ngamia yametumika kutibu shida ya tumbo inayosababishwa na virusi kwa mamia ya miaka.

Inaaminika kuwa maziwa hayo yana kingamwili zinazosaidia kutibu ugonjwa huu wa kuhara ambao huwapata watoto hasa.

Yanaweza kupunguza sukari ya damu na insulini.

Maziwa ya ngamia yanaaminika kupunguza sukari ya damu na kuboresha mchakato wa insulini kwa watu walio na aina ya 1 na aina ya 2 ya kisukari.

Insulini ni homoni inayosaidia kurekebisha viwango vya sukari kwenye damu.

Maziwa ya ngamia yana uwezo wa kupambana na virusi na bakteria mbalimbali zinazosababisha magonjwa, hivyo maziwa ya ngamia yana sifa zake za kuongeza kinga.

Maziwa haya ni rahisi kuongeza kwenye lishe yako.

Unaweza kunywa au utumie katika kahawa, chai, sharubati, bidhaa za kuoka, mchuzi au supu.

Kunaweza kuwa na tofauti ndogo katika ladha kulingana na mahali ambapo maziwa yanatoka.

Bidhaa za maziwa ya ngamia kama vile jibini laini, mtindi na siagi hazipatikani kwa wingi kutokana na changamoto katika usindikaji unaochangiwa na utungaji wa maziwa ya ngamia.

  • Tags

You can share this post!

KASHESHE: ‘Walinitilia sumu’

Wataalamu na wasomi wa Kiswahili watathmini maendeleo yake...

T L