• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:55 AM
‘Lockdown’ ya Aprili 2021 ilivyoyumbisha biashara yake ya madema ya kuku

‘Lockdown’ ya Aprili 2021 ilivyoyumbisha biashara yake ya madema ya kuku

Na SAMMY WAWERU

PETER Irungu amekuwa katika biashara ya uundaji wa madema kwa zaidi ya miaka 10.

Madema ni vizimba au makazi tamba kukinga ndege kama vile kuku, bata, njiwa na wengineo wanaofugwa nyumbani wasiliwe au kuhangaishwa na adui, hasa mwewe.

Kijana Irungu, huyatengeneza kwa nyaya na mabati. Aliingilia uundaji wa madema 2010.

Ni biashara ya juakali na ambayo imekuwa ikimsaidia kukithi familia yake riziki na mahitaji mengine muhimu ya kimsingi. Irungu, 36, ni mume na baba wa mtoto mmoja.

Huku akiwa mkazi wa Nairobi, mwaka uliopita, 2020 Kenya ilipothibitisha kuwa mwenyeji wa virusi vya corona, ugonjwa ambao sasa ni janga la kimataifa, Irungu anasema biashara ya vifaa vyake ilinoga.

Covid-19 ilianza kuathiri uchumi wa Kenya pindi ilipotua, mamia, maelfu na mamilioni ya watu wakapoteza ajira.

Aidha, biashara ziliyumba na zinaendelea kuyumbishwa, watu wakapoteza nafasi za ajira, ishara ya uchumi kuathirika kwa kiasi kikubwa.

Baadhi ya walioathirika, waliingilia shughuli za kilimo na ufugaji.

Ufugaji wa kuku ni kati ya miradi ambayo watu waliingilia, ili kujiendeleza kimaisha.

“Oda za madema ziliongezeka 2020 kwa sababu ya waliokumbatia ufugaji wa kuku,” Irungu anasema.

Kulingana na masimulizi yake, alipata mamia ya oda kutoka sehemu mbalimbali za nchi.

Huendeshea biashara hiyo eneo la Githurai 44, iliko karakana yake, kiungani mwa jiji la Nairobi.

‘Lockdown’ ya 2021

Mwaka huu, 2021, mambo hayakuwa tofauti. “Biashara ya madema inaendelea kunoga,” aeleza.

Hata hivyo, Irungu anasema amri ya ama kuingia au kutoka kaunti zilizotajwa kuwa hatari katika maambukizi ya corona nusra izime jitihada zake.

Serikali ilitangaza kutekelezwa kwa amri hiyo Kaunti ya Nairobi, Nakuru, Machakos, Kajiado na Kiambu, kati ya Machi 26, 2021 – Mei 1, 2021.

Huku Rais Uhuru Kenyatta akiiridhia kwa kupunguza kasi ya maambukizi kwa kiasi kikubwa, Irungu anaambia Taifa Leo kuwa hangeweza kufikia wateja wake kwa sababu ya vizuizi vya barabara vilivyowekwa.

“Vilikuwa kizingiti kikuu kufikia wateja wangu, ambao ni wafugaji wa kuku,” analalamika.

Mjasirimali huyo anasema amri hiyo ilitangazwa wakati ambapo alikuwa amewekeza fedha zake zote katika malighafi ya kutengeneza madema.

Huundwa kwa nyaya na mabati, vifaa anavyohoji bei yake inazidi kupanda kutokana na kuendelea kuongezeka kwa ushuru.

“Kwa sasa nina zaidi ya wateja 30 waliokuwa wamelipa arbuni (malipo ya kwanza kuzuia kitu kisiuzwe), wanaosubiri niwapelekee madema,” asema, akiongeza kuwa amelemewa kuwafikishia oda zao kwa sababu ya kukosa fedha.

Analia mapato yake yamelala kwenye vifaa vingi alivyotengeneza.

Peter Irungu, mtengenezaji wa madema katika mtaa wa Githurai 44, Nairobi. Picha/ Sammy Waweru

Hali aliyoshuhudia mwaka huu, haikuwa tofauti na ya 2020. Serikali ilikuwa imeweka amri ya ama kutoka au kuingia Kaunti ya Nairobi na Kiambu kati ya mwezi Aprili na Julai 2020, ili kusaidia kudhibiti maenezi zaidi ya corona.

“Mwaka uliopita, pia nilikuwa nimelaza mapato kwenye madema. Hata hivyo, taifa lilipofunguliwa nilipata nafuu,” Irungu anaelezea, akisema wanunuzi wake wengi hutoka eneo la Kati mwa Kenya.

Wakulima hususan wa mazao mbichi pia walikadiria hasara.

“Kipindi cha lockdown, wengi wetu tulipata hasara mazao kukosa wanunuzi na hata kuozea shambani,” Paul Mwangi, mkulima eneo la Nyandarua anasema, akikadiria hasara.

Mwangi hukuza viazimbatata, kabichi, karoti na maharagwe asilia ya kijani.

“Wakati wa amri ya ama kuingia au kutoka Nairobi, nilikuwa na kabichi 6,000 ila nilifanikiwa kuuza 300 pekee,” anafichua.

Anasema mazao yaliyosalia yaliozea shambani na mengine kulishwa mifugo.

Kwa Peter Irungu, tangazo la Rais Kenyatta, Sikukuu ya maadhimisho ya Leba Dei, Mei 1, 2021, kuondolewa kwa lockdown, anasema ni afueni akiwa mwingi wa matumaini ataweza kufufua biashara yake ya madema.

You can share this post!

Swansea City na Bournmouth zashinda mkondo wa kwanza wa...

Chipukizi asimulia machafuko ya 2007 yalivyomchochea...