• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
MWALIMU WA WIKI: Rashid Kisenya mwalimu dijitali

MWALIMU WA WIKI: Rashid Kisenya mwalimu dijitali

Na CHRIS ADUNGO

KUFAULU kwa mwanafunzi shuleni hutegemea mtazamo wake kwa mwalimu na masomo yote anayofundishwa darasani.

Kwa kuwa uwezo wa wanafunzi wa kumudu masomo hutofautiana, mwalimu ana ulazima wa kuelewa kiwango cha kila mwanafunzi na kubuni mbinu za ufundishaji zitakazomwezesha kila mmoja wao kufikia malengo yake.

Mwanafunzi aliye na uwezo wa chini kimasomo huvunjika moyo upesi iwapo mwalimu ataanza kumlinganisha na wenzake wanaoelewa mambo haraka.

Mwalimu Rashid Juma Kisenya katika Shule ya Msingi ya Central Girls, Kaunti ya Mombasa, anashikilia kuwa mbinu rahisi zaidi ya kuamsha ari ya kuthaminiwa kwa masomo miongoni mwa wanafunzi ni kuwaaminisha kwamba hakuna lisilowekezana.

Rashid alizaliwa Oktoba 18, 1981 katika mtaa wa Kaloleni, eneo la Migosi, Kaunti ya Kisumu. Ndiye mwanambee katika familia ya watoto sita wa Bi Saumu Rashid Ogutu na marehemu Bw Suleiman Kisenya aliyewahi kuhudumu katika Jeshi la Kenya (KDF).

Alianza masomo katika Shule ya Msingi ya Moi Barracks, Eldoret kabla ya kujiunga na Shule ya Msingi ya Ogango, Kisumu. Rashid alifanya Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) mnamo 1996 na kupata fursa ya kusomea katika Shule ya Upili ya Muslim Kisumu kuanzia 1997. Alihitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE) mnamo 2000.

Ingawa matamanio yake yalikuwa kusomea uanahabari na hatimaye kuwa mtangazaji wa habari runingani, alijiunga na Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Islamic Teachers Mikindani, Mombasa mnamo 2002. Mazingira alimokulia yalimweka katika ulazima wa kutumia Kiswahili mara kwa mara kwa minajili ya mawasiliano.

Aliyemchochea zaidi kusomea taaluma ya ualimu ni Bw Ustadh ‘Baba’ Opiyo aliyemfundisha Kiswahili katika shule ya upili.

Rashid alihitimu ualimu mnamo 2003 na akaanza kufundisha katika Shule ya Msingi ya Central Girls akiwa mwalimu wa kujitolea. Alihudumu huko kwa kipindi cha miaka mitatu kabla ya kuhamia Shule ya Msingi ya Arya Samaj, Mwembe Tayari, Mombasa mnamo 2006.

Aliajiriwa na Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) mnamo Februari 2009 na akatumwa kufundisha Kiswahili, Sayansi na Dini ya Kiislamu (IRE) katika Shule ya Msingi ya Central Girls. Amewahi pia kuwa kaimu mwalimu mwandamizi na kaimu naibu wa mwalimu mkuu shuleni humo kati ya 2015 na 2019.

Rashid kwa sasa ndiye mlezi wa wanaskauti, kocha wa handiboli, vikapu na riadha. Mbali na kuwa Mkuu wa Idara ya Sayansi, anashirikiana na Bi Afye Abdalla na Bi Sauda Shee kulisukuma gurudumu la Kiswahili shuleni Central Girls.

“Nashirikisha sana ubunifu wa kiteknolojia katika ufundishaji wangu. Pamoja na kutumia vifaa vya kidijitali ambavyo husisimua sana wanafunzi, matumizi ya video na picha ni namna nyingine ya kufanya masomo kuvutia.”

“Kuwahusisha wanafunzi moja kwa moja huwapa fursa ya kufanya mambo kwa kujiamini. Mawanda ya fikira zao hupanuka zaidi na huanza kuona kwamba vitu wanavyofundishwa ni vya kawaida mno,” anaeleza.

Kwa mujibu wa Rashid, mwanafunzi akipata umilisi ufaao, atakuwa wa manufaa katika jamii ya sasa inayoshuhudia mabadiliko ya kasi katika takriban nyanja zote.

“Kutokana na imani hii, ipo haja kwa mwalimu

kukumbatia matumizi ya mbinu zitakazompa mwanafunzi nafasi murua ya kushiriki masimulizi, usomaji na kufanya kazi katika vikundi. Matumizi ya vifaa vya kidijitali yatachochea ubongo wa mwanafunzi uanze kufanya kazi,” anashauri.

Haja ya kujiendeleza kitaaluma ilimpa Rashid msukumo wa kusomea diploma ya ualimu katika Coast Institute of Research & Teaching kati ya 2012 na 2013.

Alijiunga baadaye na Chuo Kikuu cha Kenya Methodist (KeMU) kusomea shahada ya ualimu kati ya 2015 na 2018. Analenga sasa kusomea shahada ya uzamili katika masuala ya usimamizi wa elimu.

Kubwa zaidi katika maazimio ya Rashid ni kumiliki shule yake binafsi pamoja na kuzamia kabisa masuala ya uandishi wa fasihi ili kuendeleza kipaji cha utunzi kilichoanza kujikuza ndani yake tangu utotoni.

Rashid ametunga idadi kubwa ya mashairi ambayo yamekuwa yakifana katika mashindano ya viwango mbalimbali. Baadhi ya mashairi hayo yamekuwa yakichapishwa katika gazeti hili la Taifa Leo chini ya lakabu ‘Malenga wa Auji’.

You can share this post!

Raila aahidi kuigeuza Lamu iwe ‘Dubai ya Afrika’

Mahasla njaa Ruto akigawa mamilioni

T L