• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
Mahasla njaa Ruto akigawa mamilioni

Mahasla njaa Ruto akigawa mamilioni

ALEX NJERU, BRIAN OJAMAA Na BENSON MATHEKA

WAHUDUMU wa Bodaboda na mama mboga, sasa wanalaumu wanasiasa kwa kuwatumia kupata mamilioni ya pesa kutoka kwa Naibu Rais William Ruto wakidai wanazitumia kuwainua kiuchumi.

Dkt Ruto amekuwa akiandaa vikao na wafanyabiashara wadogo katika maeneo tofauti na kuwapa pesa wagawane akidai ni juhudi zake za kuinua kiuchumi Wakenya wa mapato ya chini.

Hata hivyo wanasema kwamba hawapati pesa hizo.

Katika maeneo anayokutana na wafanyabiashara hao, huwa anaandamana na wanasiasa wanaomuunga mkono wakiwemo wabunge anaowatumia kuandaa mikutano hiyo.

Hata hivyo, vijana wengi wamelalamika kuwa huwa hawapati pesa anazotoa wagawane wakilaumu washirika wake kwa kuwapiga chenga.

Mnamo Jumamosi, wahudumu wa Bodaboda kaunti ya Tharaka Nithi walilaumu washirika wa Dkt Ruto kwa kuwatumia kupata pesa kutoka kwa naibu rais kujinufaisha.

Akizungumza na wanahabari mjini Chuka, mwenyekiti wa chama cha wanabodaboda eneo hilo Bw Lewis Mutwiri alimlaumu mbunge wa

Chuka/Igambang’ombe Patrick Munene kwa kupokea pesa kutoka kwa Dkt Ruto alipotembelea eneo hilo. Alimlaumu mbunge huyo kwa kukata kushirikiana na makundi yaliyosajiliwa ili kutimiza maslahi yake ya kibinafsi.

“Tunataka naibu rais aje kwetu moja kwa moja na sio kupitia wanasiasa kwa sababu wanataka kututumia na kisha kuunda makundi yao,” alisema Bw Mutwiri.

Afisa huyo alisema kwamba ombi lao kwa Dkt Ruto ni awasaidie kununua ambulensi ya kuokoa maisha yao na watu wengine wakihusika kwenye ajali.

Kundi jingine linaloongozwa na Bw Willis Mugambi linataka Dkt Ruto awape pesa lakini sio kuwanunulia ambulensi. Akizungumza na Taifa Leo jana Jumapili, Bw Munene alisema kundi analodaiwa kuunda ni la vijana walioshiriki mpango wa Kazi Mtaani ambao waliunda Meru South Cohorts Youth Sacco.

Alisema wanabodaboda hao watakutana na Dkt Ruto katika mji wa Kathwana na kisha akutane na Meru South Cohorts Youth Sacco mjini Chuka ulio umbali wa kilomita 30 ili kuepuka makabiliano.

Ghasia zilizozuka wakati wa ziara ya Dkt Ruto katika mtaa wa Kondele mjini Kisumu wiki jana, zilihusishwa na pesa anazodaiwa aliachia makundi ya vijana. Baadhi walisema kwamba pesa hizo zilitoweka.

Jumapili, mama mboga katika eneobunge la Kanduyi kaunti ya Bungoma waliungana na mama mboga kulalamika kuwa hawajapata pesa walizoachiwa na Dkt Ruto alipozuru eneo hilo wiki mbili zilizopita.

Mwenyekiti wa chama cha Bodaboda eneo hilo David Mulonja Simiyu alisema walipatiwa Sh1 milioni na Dkt Ruto alipozuru Tongaren, Webuye East, Kimilili, Kabuchai, Mt Elgon, Sirisia, Bumula, Webuye West na Kanduyi lakini hawakupata hata senti moja.

“Naibu Rais alipokuja hapa alitupatia Sh1 milioni na akapatia mama mboga Sh1 milioni lakini juhudi zetu za kupata pesa hizo zimegonga mwamba,” alisema.

Alisema kwamba walisikia ni mbunge wa eneo hilo John Waluke aliyepokea pesa hizo.

Kiongozi wa vijana eneo la Kanduyi Kelvin Sifuna alisema kwamba walikuwa na matumaini ya kutumia pesa hizo kuinua biashara zao.

Madai ya kutoweka kwa pesa ambazo Dkt Ruto anapatia vijana yameripotiwa kaunti za Kitui na Kongowea kaunti ya Mombasa.

Mnamo Septemba 25, vijana waliandamana mjini Kitui wakilalamika kuwa hawakupata walizoachiwa na Dkt Ruto wagawane kujiinua kiuchumi.

You can share this post!

MWALIMU WA WIKI: Rashid Kisenya mwalimu dijitali

Wezi wa mali ya umma tutawatia adabu – Moi

T L