• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:55 AM
MAKALA MAALUM: Awadh hajasoma ila anasifika kwa kuongoza hafla na utangazaji mpira

MAKALA MAALUM: Awadh hajasoma ila anasifika kwa kuongoza hafla na utangazaji mpira

Na KALUME KAZUNGU

SIFA zake za kutangaza mpira wa kandanda kwenye viwanja mbalimbali na pia uzoefu wake katika kuongoza sherehe mbalimbali zimemfanya kupendwa na wengi ndani na nje ya kisiwa cha Lamu.

Kutana na Awadh Hassan Awadh kwa jina la msimbo ‘Tajiri wa Mifupa, Maskini wa Nyama.’

Kila wakati jina ‘Tajiri wa Mifupa, Maskini wa Nyama’ linapopasua anga kwenye viwanja mbalimbali vya mpira, ikiwemo Twaif, Shella, Kashmir na sehemu zingine za kaunti ya Lamu, ikiwemo Mpeketoni, Witu, Kiunga, Pate na maeneo mengine, utakubaliana kuwa jamaa huyo kweli ni mjuzi aliyebobea kwenye tasnia ya utangazaji na uhafidhina.

Aghalabu huenda ukamfananisha na watangazaji mashuhuri kama vile Jack Oyoo Silvester ‘Kaka JOS’ au Ali Salim Manga.

Viwanja vingi ambapo ‘Tajiri wa Mifupa, Maskini wa Nyama’ huwepo mara nyingi hufurika kadamnasi ya watu, si kwa sababu wahudhuriaji hao ni mashabiki kindakindaki wa mpira ila huvutiwa tu na sauti nyororo na pia utumiaji mwafaka wa lugha ya Kiswahili kutoka kwa mtangazaji huyo wa kabumbu.

Usichokijua ni kwamba mtangazaji huyu hajasomea kazi hiyo wala kupata elimu yoyote, ikiwemo ile ya msingi, angaa darasa la kwanza.

Awadh Hassan Awadh alizaliwa Januari 1, 1984, kisiwani Kiwayu tarafa ya Kiunga, Kaunti Ndogo ya Lamu Mashariki katika familia ya watoto tisa, yeye akiwa ni mzaliwa wa tatu.

Kutokana na umasikini uliokumba familia yake, Awadh hakuweza kujiunga na shule ya msingi, upili au chuo kupata elimu.

Badala yake aliamua kufuata mafundisho ya dini, ambapo alijiunga na madrassa ya Swafaa yaliyoko kisiwani Lamu, alikofuzu mafundisho hayo hadi kuwa mwalimu wa dini.

Anasema changamoto za kimaisha ndizo zilizomfanya kukitambua na kukipalilia zaidi kipaji chake cha kutangaza kandanda na mfawidhi kwenye sherehe mbalimbali, ikiwemo makongamano ya kisiasa ambayo hufanyika Lamu kila mara.

Ni nadra sana kumkosa Awadh, kwenye majukwaa au viwanja mbalimbali wakati Lamu ikiadhimisha sherehe kama vile Tamasha za Utamaduni wa Lamu, Maulid ya Lamu na hafla zingine, zikiwemo zile za kisiasa.

“Nilifahamu kuwa niko na talanta ya kutangaza mpira na uhafidhina tangu nikiwa mtoto. Mimi hupenda kuongea. Nilikuwa kila mara ninapojitokeza kushika kipaza sauti, iwe ni kwenye sherehe au kwenye uga wa mpira, watu wengi walipenda sana kunisikiliza. Nilianzia hapo na kufikia sasa hakuna sherehe zozote zinazofanyika ndani na nje ya kisiwa cha Lamu nisizoalikwa kuongoza hafla hizo na hata kutangaza soka iwapo kilele cha sherehe husika hujumuisha michezo,” anasema Awadh.

Lakini je, jina ‘Tajiri wa Mifupa, Maskini wa Nyama’ alilipata vipi? Anaeleza kuwa yeye ni mtu wa mwili mdogo. Ukimuona kwa mara ya kwanza jinsi alivyokonda utadhami ni mgonjwa, japo ni maumbile tu lakini mwenyewe yu buheri wa afya.

Anasema katika harakati za kujitambulisha kwa urahisi kwa umma, aliamua kuibuka na nembo yake mwenyewe, ndivyo akaafikia kujipa jina hilo la msimbo linaloshabihiana na maumbile yake madogo.

“Kwa nini nijifanye mnene ilhali kakonda gaya ya kukonda? Nilijikubali jinsi nilivyo kwamba japo ni ‘Maskini wa Nyama’ kwa kukonda kwangu lakini pia kwa upande mwingine ni ‘Tajiri wa Mifupa.’ Hapo ndipo nikaibuka na jina hilo la ‘Tajiri wa Mifupa, Maskini wa Nyama’ kama nembo yangu,” anaeleza Awadh.

Anasema katika maisha ya kujaribu kusukuma kipaji chake, amewahi kutangamana na watu wenye haiba kubwa na hata kushiriki nao jukwaa moja, ikiwemo Rais Uhuru Kenyatta, Gavana wa Mombasa, Hassan Ali Joho na wengineo.

“Nimetangaza mpira kwenye nyanja mbalimbali za Lamu wakati wa sherehe zinazowaleta magavana kutoka sehemu mbalimbali za nchi eneo hili,” anasema.

Anaongeza, “Isitoshe, mojawapo ya sherehe nilizoongoza na kujihisi kuwa mwenye haiba kubwa ni wakati Rais Uhuru Kenyatta alipozuru mji wa Lamu kukutana na wananchi wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2017. Najivunia kwamba mimi ndiye niliyemkaribisha Rais Kenyatta alipokuwa akiingia kwenye eneo la Mkunguni kuhutubia umma.”

Awadh anaeleza kuwa safari yake ya kukuza kipaji cha utangazaji imekuwa ya mabonde, milima na changamoto za kila aina.

Kwanza anataja ukosefu wa elimu na vyeti vya kumwezesha kuajiriwa hapa nchini kuwa suala zito linalomkosesha lepe la usingizi kila kuchao.

“Talanta niko nayo lakini ukosefu wangu wa elimu na makaratasi ya kunifanya kupata ajira ndilo doa jeusi katika aushi yangu. Kuna wamiliki wa kampuni mbalimbali, ikiwemo wale wa vituo vya redio ambao wamenitafuta ili kuwa mtangazaji wao lakini wanapouliza kuhusu elimu yangu wanapata kuwa sina cheti chochote. Hii ndiyo sababu hadi wa leo nimebaki kuwa tu mtangazaji tajika, japo wa vichochoroni,” anasema Awadh.

Akiwa amejaaliwa mke na watoto wanne, anasema licha ya kukosa kuajiriwa kwenye vituo vya redio, kugaagaa kwake kimaisha, hasa kwenye anga za Lamu kumemwacha bila kula wali mkavu.

“Chambilecho ukikosa la mama, hata la mbwa huamwa. Licha ya kutopata ajira maalum kwa kukosa elimu, nimekuwa nikipokea mialiko mbalimbali ya kuongoza sherehe hapa Lamu na nje. Isitoshe, nimekuwa nikitangaza mpira, hasa katika ligi zinazoendelea hapa Lamu na mwisho wa siku napokea mtaji wa kukimu familia yangu.”

“Kutokana na uzoefu wangu wa kuongea, kwa miaka kadhaa nimekuwa ninahudumu kama mwenyekiti wa Muungano wa Wamiliki wa boti na mashua hapa Lamu, ambapo mwisho wa siku napata riziki. Isitoshe, mimi pia ni mjasiriamali mashuhuri katika kisiwa hiki cha Lamu. Najua ipo siku nitapata elimu na pia kufunguka zaidi kimaisha na kitalanta hadi kufikia kilele,” anasema.

Anawashauri vijana kuzingatia mambo matatu maishani.

Anasema vijana lazima wafahamu fika kwamba maisha ni mapambano, majaribu na yanayohitaji uamuzi.

“Sharti ukubali kupambana maishani ili uvuke upande mwingine na kufanikiwa. Mja lazima pia ajaribu. Heri kujaribu, ufanye kifaulu au kiharibike kuliko kukosa kufanya hivyo kabisa.

Ushauri wake wa mwisho kwa vijana ni kwamba lazima mtu afanye uamuzi akisisitiza kuwa maishani lazima uwe na lengo.

“Hilo haliwezi kuafikiwa bila kuamua kulifanyia bidii ili ulifikie. Ukiwa wampenda mtu, si vyema kuendelea kuumia moyo, lazima uamue kumfuata umweleze wazi kilichoko moyoni, akukatae ama akukubali,” anaongeza Awadh.

You can share this post!

Trump sasa apanga kuzindua mtandao

TAHARIRI: Wazazi wawachunge watoto na mitandao