• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
MAKALA MAALUM: Mahangaiko ya wananchi waliobomolewa makao na serikali

MAKALA MAALUM: Mahangaiko ya wananchi waliobomolewa makao na serikali

Na SAMMY WAWERU

UBOMOAJI wa majengo na makazi uliotekelezwa katika eneo la Kware, Kaunti Ndogo ya Njiru, kiungani mwa jiji la Nairobi umemwacha Jacinta Wanjiku Macharia na msururu wa mawazo mazito.

Alikuwa mmiliki wa ploti Nairobi aliyokuwa ameijenga, hivyo basi kumuondolea mzigo wa gharama ya kukodi nyumba.

Ubomozi huo uliofanyika usiku wa kuamkia Machi 26, 2021 na kuendelezwa kwa muda wa siku kadhaa, uligeuza mradi wa nyumba yake kuwa vipande vidogo vya saruji, changarawe na mawe yasiyo na maana.

Kulingana na masimulizi ya mama huyu wa mtoto mmoja, hakuna alichoweza kuokoa.

Akionekana kuzongwa na maswali chungu nzima atakavyoweza kuinua hali yake ya maisha na kukwea hadi alipokuwa, ni tukio analotaja kama “la kinyama kuharibu mapato na raslimali niliyojikakamua kuwekeza na mume wangu”.

“Tuliamshwa saa tisa alfajiri na mapema, shughuli za matingatinga kubomoa nyumba zilipoanza, maafisa wa polisi wakirusha gesi ya vitoa machozi kufurusha watu. Hakuna nilichookoa, ila mtoto na mavazi tuliyokuwa nayo mwilini. Nimerejeshwa chekechea kuanza upya safari ya maisha,” Wanjiku, 25, anasimulia.

Kinachomuuma zaidi, ni jitihada zake asubuhi hiyo kurai afisa mmoja wa polisi angalau aweze kunusuru vitu muhimu vya nyumba, lakini hazikuzaa matunda.

Jacinta Wanjiku katika eneo la Kware, Njiru, Kaunti ya Nairobi ambalo sasa ni mahame, akielezea jinsi walivyofurushwa bila notisi. Picha/ Sammy Waweru

“Aliniambia amri imetoka ‘juu’. Stakabadhi zote muhimu na simu zilipotelea humo. Mahandaki yalichimbwa kutoruhusu gari lolote kuingia tusibebe tunachomiliki,” anasema.

Kipande chake cha ploti chenye ukubwa wa mita 30 kwa 60 na alichokuwa anamiliki, sasa ni mahame.

Alikinunua 2018, ambapo ilimgharimu Sh330, 000 na kukipulizia zaidi ya Sh400, 000 kukifanya makao.

“Moyo unauma nikikumbuka jinsi tulivyojinyima ili kuondokea nyumba za kukodi Nairobi. Mume wangu huchuuza malimali kwa wilibaro, nami vibarua vya hapa na pale. Tuliweka akiba tukanunua ploti ambayo sasa haipo tena,” Wanjiku anafafanua, akilemewa kudhibiti machozi.

Hadithi yake si tofauti na ya Eunice Wachira Kiarie, 28, ambaye pia ni miongoni mwa mamia na maelfu ya walioathirika.

Eunice ni mama wa watoto wawili, wenye umri wa miaka 9 na mwaka mmoja.

Ploti ya mama huyo pia ni yenye ukubwa wa mita 30 kwa 60. Aidha, aliinunua miaka mitatu iliyopita kutoka kwa rafiki wa familia ambaye Eunice anahoji alienda ng’ambo.

“Kwa sababu tuliuziwa na mtu tunayejua na aliyekuwa humo kwa zaidi ya miaka 10, hatukuwa na wasiwasi. Isitoshe, tulihusisha wakili,” anadokeza.

Huku kipande hicho wakiuziwa Sh280, 000 anafichua iliwagharimu zaidi ya Sh800, 000 kufanya ujenzi.

“Wakati wa kununua mume wangu alikuwa dereva wa matrela ya masafa marefu. Kiwango kikubwa cha fedha tulizowekeza kilikuwa mkopo, ambao hatujakamilisha kulipa,” anaelezea.

Hakuna alichookoa, ila wanawe na mavazi waliyovalia.

Mwathiriwa mwingine wa ubomoaji wa makao Kware, Michael Mwangi anakadiria hasara ya mali yenye thamani ya Sh4 milioni. “Kando na nyumba yangu kubomolewa, nilikuwa na duka la vifaa vya ujenzi, ambalo sasa ni historia. Ninahisi uchungu nikikumbuka jasho langu lilivyoangushwa chini ya saa chache,” Mwangi analia.

Zaidi ya watu 5, 000 waliathirika, kufuatia ubomozi huo wanaolalamikia hawakuwa wamepewa notisi ya kuondoka.

Umiliki wa ardhi hiyo ukisalia kuwa kitendawili, maafisa wa polisi wametumwa kushika doria kuilinda.

Shughuli za saveya kuweka alama (land marking) zinaendelea chini ya ulinzi mkali, eneo hilo likiwa marufuku kuingia hususan kwa waliofurushwa.

Huku walioathirika wakiendelea kuhangaika, hasa baada ya kuondolewa kipindi hiki taifa limelemewa na makali ya janga la Covid-19, Chifu wa Kata ya Njiru, Teresia Wambui anadai hakupokea notisi yoyote kuhusu ubomoaji huo.

“Siku ya tukio nilipigiwa simu mwendo wa saa kumi alfajiri. Sikuwa nimearifiwa chochote na ubomoaji ulinifikia kwa mshangao,” akaambia Taifa Leo, kupitia mahojiano ya kipekee.

Kulingana na chifu huyo, ardhi hiyo yenye utata ni ya kibinafsi, akisema haihusishwi na serikali.

Hata hivyo, imebainika imekuwa na mzozo wa umiliki kwa zaidi ya miaka 20, kampuni ya Njiru Ageria ikitajwa kuwa mmiliki.

Kwa mujibu wa wahasiriwa tuliozungumza nao, wanahoji vyeti walivyokabidhiwa baada ya ununuzi vinaonyesha ardhi hiyo ni mradi wa maskwota, unaomilikiwa na Investors Settlement Field.

Wakilalamikia sheria kutofuatwa wakati wa kuondolewa, idara ya polisi inasema zoezi la kuwafurusha lilikuwa oparesheni iliyohusisha vikosi vya pamoja vya usalama.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo, Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Kayole na ambacho kinajukumika kuimarisha shughuli za usalama eneo la Njiru, Bw Paul Wambugu hakueleza bayana ikiwa kuna notisi iliyotolewa.

“Ilikuwa oparesheni ya vikosi vya pamoja, na hilo linapojiri halina jawabu,” Bw Wambugu akasema, akikwepa kueleza iwapo kulikuwa na amri ya korti.

Hali kadhalika, afisa huyo hakuweka wazi ikiwa ardhi hiyo yenye utata ilikuwa imenyakuliwa au la.

Bomoabomoa hiyo ilitekelezwa siku ambayo Rais Uhuru Kenyatta alitangaza marufuku ya ama kuingia au kutoka kaunti tano, ikiwemo Nairobi, hatua iliyoongeza chumvi kwenye kidonda kinachouguza majeraha kwa wahusika.

Walioathirika wasingeweza kusafiri mashambani wanakotoka, kilichosalia kikiwa kuelekeza macho yao kwa Mungu kutenda miujiza.

Ni tukio ambalo limezidisha mahangaiko, serikali ikinyooshewa kidole cha lawama na kutakiwa kueleza kwa nini ubomoaji huo usingesubiri makali ya corona yapungue.

Jacinta Wanjiku ni mjamzito, na chini ya mwezi mmoja kutoka sasa anatarajia kujifungua. Baada ya nyumba yake kubomolewa, anasema alilemewa na msongo wa mawazo.

“Tuliishia kukodi chumba katika mtaa wa mabanda, na ni kupitia msaada wa wasamaria wema,” anadokeza.

Katika mtaa wa mabanda wa Mukuru Kwa Reuben, Nairobi, Wanjiku, mume wake na mvulana wao mwenye umri wa miaka 3, hawana budi ila kusukuma gurudumu la maisha kwenye chumba cha mabati na kilicho pembezoni mwa mto wa majitaka.

Ni mazingira yanayomtia hofu, kutokana na hali yake. Alipohamia humo, aliugua na anaendelea kupata matibabu.

“Unachoona humu, ni msaada wa wasamaria wema. Mapato ya mume wangu kwa siku ni chini ya Sh200, na yanagharamia chakula pekee. Mvua inaponyesha, chumba kinafuja, ni hatari kuacha mtoto kuenda kusaka riziki,” anafafanua, akisema afya yake inaendelea kudhoofika kutokana na hali ya mazingira duni wanayoishi.

“Endapo ardhi tuliyonunua ilikuwa ya unyakuzi kama wanavyodai, kwa nini waliona ugumu kutupa notisi tuondoke kwa amani na utulivu? Maisha yamegeuka kuwa magumu, waliokuwa wakiishi kwao sasa wamekuwa ombaomba,” anaelezea.

Naye Eunice Wachira alikaribishwa na mmoja wa jamaa zake, anayeishi eneo la Kahawa West, kiungani mwa jiji la Nairobi, mazingira waliyoko yakiwa ni yaleyale ya kutesa.

“Kunapokucha, ninapata tabasamu. Usiku mawazo yanatawala,” anasema, akifichua mwanawe mdogo ana tatizo la shinikizo la damu na ambaye kila wiki huhudhuria kliniki.

Simulizi yao inaashiria mahangaiko ya mamia na maelfu ya walioathirika kufuatia ubomoaji huo.

Licha ya kujaribu kutafuta suluhu kupitia viongozi waliochaguliwa Nairobi, wanadai hakuna aliyejituma kuangazia changamoto zinazowakumba.

Baadhi wanauguza majeraha kufuatia vurugu zilizozuka wakati wa ubomozi, tetesi zikiibuka kuna mmoja alifariki kutokana na jeraha la risasi na kadha mshtuko, wakikadiria hasara waliyopata.

Kimsingi, wahasiriwa wanalalamikia haki za kibinadamu kukiukwa.

Bw Gerald Muchiri, Wakili kutoka Wangira Okoba & Company Advocates eneo la Viwandani, Nairobi anasema waathiriwa walipaswa kupokezwa notisi ya siku 30 kabla ya ubomoaji kutekelezwa. “Kisheria, notisi inaeleza kuhusu ardhi yenye utata, wanaolengwa na sababu za kutaka waondolewe,” Bw Muchiri anasisitiza.

“Endapo kulikuwa na ukiukaji wa haki za kibinadamu, wanaweza kukata rufaa ya ubomoaji katika Mahakama Kuu washinikize fidia ya hasara waliyokadiria,” Wakili huyo anashauri.

Mwaka 2020 bomoabomoa sawa na ya Kware – Njiru ilishuhudiwa katika kitongoji cha Kariobangi Sewage na Ruai. Waathiriwa kufikia sasa wanaendelea kuhangaika.

You can share this post!

Wakazi wa mitaa ya mabanda Nairobi wahangaika kupata maji

Klabu zote sita za EPL zilizokuwa zimejiunga na European...