• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
MAKALA MAALUM: Wanafunzi 700 Lugari hawana madarasa shule zikifunguliwa wiki ijayo

MAKALA MAALUM: Wanafunzi 700 Lugari hawana madarasa shule zikifunguliwa wiki ijayo

Na TITUS OMINDE

HUKU wanafunzi wakijandaa kwa ufunguzi wa shule mnamo Mei 10, hali duni ya miundo msingi katika shule ya msingi ya Panpaper katika kaunti ndogo ya Lugari inayumbisha hatima ya kufunguliwa kwa taasisi hiyo.

Shule hiyo ambayo ilianzishwa yapata miaka 20 iliyopita, haina madarasa ya kudumu licha ya kuwepo kwa hazina ya maendeleo katika maeneobunge N-G CDF.

Unapoingia katika shule hiyo unakutana na mijengo ya madarasa ambayo yanakaa kama magofu ya mahame

Madarasa ambayo wazazi walijenga kwa udongo yalibomolewa na upepo mkali yapata miezi miwili iliyopita.

Mbali na ukosefu wa madarasa shule hiyo pia haina vyoo kwa wanafunzi.

Ukosefu wa vyoo umefanya wanafunzi kutumia vichaka karibu na shule hiyo kama maeneo pa kwenda msalani.

Mwenyekiti wa kamati ya wazazi Shuleni humo (PA) Priscah Naliaka Mabonga alitoa wito kwa viongozi wa eneo hilo kuingilia kati na kusaidia shule hiyo kuwajengea watoto wao madarasa ya kisasa.

Akizungumza na Taifa Leo katika shule hiyo, Bi Mabonga alisema tangu madarasa hayo sita yaporomoshwe hakuna kiongozi kutoka eneo hilo ambaye amewapa msaada hitajika.

“Kama wazazi tuna wasiwasi sana wakati ufunguzi wa shule unakaribia, hatujui watoto wetu watasomea wapi ikizingatia kwamba tunaingia katika msimu wa mvua ya masika na mahali hapa ni eneo lenye maji mengi, ” alisema Bi Mabonga.

Bi Mabonga alitoa wito kwa wadau wote pamoja na Mbunge wa eneo hilo Ayub Savula kuingilia kati ili kuwasaidia wanafunzi kabla ya ufunguzi wa shule.

“Tunataka mbunge wa eneo letu Bw Savula aje kusaidia watoto wetu kupata madarasa mazuri kupitia CDF. Watoto wetu wanastahili mazingira bora ya masomo mazuri kama watoto wengine wowote katika eneo hili, ” Bi Mabonga alisema.

Bi Priscah Naliaka Mabonga ni mwenyekiti wa kamati ya wazazi (PA) Shule ya Msingi ya Panpaper, Lugari. Picha/ Titus Ominde

Kiongozi huyo alisema iwapo hali hiyo haitashughulikiwa kwa wakati, kuna uwezekanao wa kutokea mkurupuko wa maradhi kutokana na mazingira duni ambamo wanafunzi husomea.

“Msimu wa mvua ya masika umefika, hatuna madarasa wala mahala pa kwenda msalani maisha ya watoto wetu yamo hatarini,” aliongeza Bi Mabonga

Mbali na wanafunzi kukosa madarasa vile vile walimu hawana afisi ambapo imewalazimu kukaa chini ya miti wakati wa kusahisha kazi za wanafunzi.

Jengo ambalo awali walikuwa wakitumia kama afisi limebadilishwa na kuwa ghala mabali kuhifadhi stakabadhi muhimu za shule hiyo.

Kutokana na ukosefu wa afisi tunalazimika kuondoka shule mapema kwa kuhofia kunyeshewa kwa kukosa mahali pa kujikinga iwapo mvua itatupa shuleni,” alisema mmoja wa walimu wa shule hiyo.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo Roslyn Wabwire alisema anahitaji madarasa zaidi ya 10 kuhudumia zaidi ya wanafunzi 700 katika shule hiyo.

Darasa moja linakadiriwa kugharimu zaidi ya Sh1.2 milioni.

“Nina wanafunzi 710, ninahitaji zaidi ya madarasa 10, natumai viongozi wetu na wahisani watasikia kilio chetu na kutupa msaada hitajika, “alisema Bi Wabwire.

Bi Nabwire alisema hali duni ya mijengo katika shule hiyo imechangia katika matoeo duni katika mitihani ya kitaifa shuleni humo.

Katika matokeo ya mtihani wa KCPE mwaka wa 2020 mwanafunzi wa kwanza shuleni humo alipata alama 352 ambapo walimu walihisi kuwa iwapo shule hiyo ingekuwa na miundombinu bora matokeo hayo yangekuwa bora zaidi.

Mbali na kujengewa madarasa ya kisasa shule hiyo pia inahitaji ardhi zaidi ili kuwezesha wanafunzi kupata uwanja wa kuchezea.

Mwenyekiti wa CDF katika eneobunge hilo, Aggrey Jeremiah alisema hazina imeweza kujenga darasa moja shuleni humo na mipango ya kujenga madarasa zaidi inaendelea katika mwaka huu wa fedha.

“Kama CDF tunajaribu, tayari tumejenga darasa moja kwa shule hiyo na mwaka huu wa fedha tunakusudia kuweka madarasa zaidi shuleni humo,” akasema Bw Jeremiah.

Bw Jeremiah alikiri kuwa kuna shule kadhaa katika eneobunge hilo ambazo zingali na mijengo ya udongo.

Kwa mujibu wa Bw Jeremiah ni kwamba mikakati imewekwa ili kuona kuwa shule zote za matope katika eneobunge hilo zinapewa sura mpya kipindi cha mwaka mmoja ujao.

“Kuna shule ambazo tulizipata zikiwa katika hali duni, tunafanya kila juhuzi ili kuona kuwa tunabadilisha sura ya shule husika,” alisema Bw Jeremiah.

Kiongozi huyo alisema mbunge wa eneobunge hilo anashirikiana na wadau wengine kama vile shirika la kusambaza umeme maeneo ya mashambani REA na kuboresha miundo mbinu katika baadhi ya shule lengwa.

Alitoa wito kwa wihisani wa matabaka mbalimbali kujitolea ili kusaidia na mbunge wa eneo hilo kuimarisha hali ya shule zote.

Huku wazazi na wanafunzi kutoka shule hiyo wakililia utawala wa eneo hilo, majirani wao katika eneobunge la Likuyani ambalo lilibuniwa kutoka lilokuwa eneobunge pana la Lugari wanasherehekea madarasa safi ya kisasa chini ya mbunge wao Dkt Enock Kibunguchy.

Mwenyekiti wa kamati ya CDF katika eneobunge la Likuyani Bi Francisca Nakaya alisema eneobunge lake limetoa kipaumbele kwa ujenzi wa madarasa na miundo msingi katika shule za eneo hilo.

Mbali na ujenzi wa madarasa Bi Nakaya alisema eneo hilo linapania kutumia aslimia kubwa ya hazina hiyo kusaidia wanafunzi ambao walifanya mtihani wa KCPE kulipa karo ya shule za upili.

“Sisi katika eneobunge letu tumetoa kipaumbele kwa ujenzi wa shule na kusaidia wanafunzi kulipa karo tukifahamu fika kuwa masomo ndio mwanzo wa urithi kwa watoto siku kwa ajili ya maendeleo na ustawi,” alisema Bi Nakaya.

Usemi huo wa Bi Nakaya uliungwa mkono na baadhi ya wazazi katika shule za misingi eno hilo ambao walisema madarasa ya shule za misingi katika eneo hilo ni ya hadhi ya juu kutokana na mchango wa hazina ya CDF.

“Madarasa katika shule yetu ni safi na ya kisasa hata wanafunzi kutoka shule za maeneobunge jirani kama vile Lugari wameanza kuhamia hapa,” alisema Bi Nakaya

Bi Florence Nasimiyu ambaye ni mzazi katika shule ya msingi ya Mufutu alisifia hazina ya CDF ya Likuyani kwa kudhamini miundo msingi katika shule za eneo hilo huku akitaka eneobunge jirani la Lugari kuiga mfano wa Likuyani katika ujenzi wa taasisi za elimu.

Kutokana na uwepo wa miundomsingi bora shuleni matokeo ya wanafunzi katika shule za eneobunge la Likuyani yanazidi kuimairka ikilinganishwa na eneobunge jirani la Lugari.

Dkt Kibunguchy aliahidi kufadhili masomo ya wanafunzi 600 bora kutoka eneo bunge hilo ambao hawana uwezo wa kulipa karo ya shule za upili.

“Ajenda yangu kubwa ya kufanikisha masomo katika eneobunge hili, masomo ndiyo kigezo kikuu katika vita dhidi ya umaskini,” alisema Dkt Kibunguchy.

Hata hivyo, Dkt Kibunguchy alitaka kamati za shule zote katika eneobunge lake kutunza miundo msingi shuleni mwao ili watoto wapate manufaa inayostahili kutoka kwa miundomsingi ya shule zao.

  • Tags

You can share this post!

Hofu ya viongozi yazamisha vijana kwa ugaidi – Jaji...

TAHARIRI: Uhuru wa habari ulindwe kikamilifu