• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 5:50 AM
Hofu ya viongozi yazamisha vijana kwa ugaidi – Jaji Said

Hofu ya viongozi yazamisha vijana kwa ugaidi – Jaji Said

Na RICHARD MUNGUTI

JAJI Said Juma Chitembwe, amesema hofu ya viongozi wakiwemo makadhi kujadili masuala kuhusu itikadi kali za kigaidi ni miongoni mwa sababu zinazofanya vijana kuendelea kuvutiwa kwa makundi ya kigaidi maeneo ya Pwani.

Akihojiwa na tume ya huduma za mahakama (JSC) katika mchakato wa kumsaka Jaji wa Mahakama ya Juu, Jaji Chitembwe alisema utafiti aliofanya katika eneo la Lamu na maeneo mengine ya Pwani, ulibainisha kuwa vijana wengi walienda nchini Somalia kupokea mafunzo hayo ya itikadi kali za ugaidi na kurejea nchini baadaye.

“Niliwasiliana na makamishna wa kaunti mbalimbali eneo la Pwani na wakanieleza viongozi wanahofia maisha yao. Hawawezi kuzungumzia jambo hilo la mafundisho hayo yenye itikadi kali kwa kuogopa kuuawa,” akasema.

Hata hivyo, alieleza JSC kuwa ametoa mapendekezo ya kuwafikia vijana waliopokea mafunzo hayo kwa lengo la kuwabadili tabia wawe wananchi wema.

Kando na suala hilo, Jaji Chitembwe alisema majaji wote wanahitaji kuwapa wananchi uhuru wao wa kikatiba.

“Nilifutilia mbali kafyu iliyokuwa imetangazwa katika kaunti za Lamu na Tana River kwa vile ilikuwa inawatesa watu sana. Wavuvi walikuwa hawaendi kuvua samaki wakiwa huru.Watu wakichelewa walikuwa wanateswa na vyombo vya usalama. Katika kila uamuzi wa mahakama lazima jaji awe na fikra za kuwapa wananchi uhuru wao,” akaeleza.

Jaji Mohammed Warsame alimwuliza Jaji Chitembwe ikiwa kati ya maamuzi ya Mahakama ya Juu kuna ule ambao anatofautiana nao.

Akijibu alisema kuwa uamuzi wa Jaji Njoki Ndung’u aliotofautiana na majaji wengine katika kesi ya kupinga ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta 2017 na ule wa Gavana wa Wajir Mohamed Abdi Mohamud kuhusu cheti chake cha Digrii.

Mahakama ilisema suala la Digrii lingeamuliwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Jaji Chitembwe aliyehojiwa pamoja na Jaji David Marete alisema majaji wanatakiwa kuwa mstari wa mbele katika utekelezaji wa haki na si kutawala.

Pia alikiri kuwa ufisadi umekithiri katika idara ya mahakama.

“Hata utafiti ukifanywa katika sekta yoyote ya mahakama itabainika kuwa ufisadi umeenea,” alisema Jaji Chitembwe.

Alisema suluhu ya kupunguza ufisadi katika idara ya mahakama ni “kuamua kesi kwa haraka.”

Jaji huyo alisema “itachukua muda mrefu kuangamiza ufisadi.”

“Umesema idara ya mahakama imelowa kwa ufisadi na kamwe hautaisha ama kupungua,” Kamishna Everlyne Olwande alimwuliza.

“Nilisema ufisadi ni mwingi na utaweza kupunguzwa,” akajibu.

Jaji Marete alifadhaika wakati Jaji Warsame alipokataa kumwuliza maswali na badala yake, kusema tu kwamba anamtakia mema.

Jaji Marete alimjibu na kusema kutomwuliza maswali kumewanyima makamishna na wananchi uhondo wa majadiliano yao.

Jaji Warsame hakueleza sababu ya kutomwuliza maswali. Mahojiano yanaendelea leo Jumanne.

  • Tags

You can share this post!

Rais Samia Suluhu wa TZ atua Kenya kwa ziara ya siku mbili

MAKALA MAALUM: Wanafunzi 700 Lugari hawana madarasa shule...