• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
MAPISHI: Jinsi ya kuandaa mlo mtamu wa pilau ya kuku na njegere

MAPISHI: Jinsi ya kuandaa mlo mtamu wa pilau ya kuku na njegere

Na MARY WANGARI

Utahitaji viungo vifuatavyo

  • ½ kilo mchele aina ya Basmati
  • ½ kilo nyama ya kuku
  • mafuta ya kupikia
  • chumvi
  • 1 kikombe cha njegere
  • 4 viazi mbatata
  • zabibu kavu kiasi upendacho
  • 3 vitunguu maji vikubwa
  • 2 karoti kubwa
  • 8 punje kubwa za thomu
  • 2 mbili kubwa aina ya tungule
  • 1 kijiko cha mdalasini uliosagwa
  • 1 kijiko kidogo cha pilipili manga
  • 1 kijiko cha binzari au kiasi upendacho
  • tangawizi kiasi cha haja

Jinsi ya kuandaa

Katakata kuku vipandevipande kiasi unachopenda kisha uvioshe katika karai safi.

Menya vipande vitatu vya thomu, tangawizi, vitie kwenye kifaa cha kiutwangia weka chumvi na kisha uvitwange.

Chambua na uoshe mchele kwa maji mengi kisha uweke kando.

Chambua viazi na uvimenye mara mbili au unavyopenda.

Twanga kitunguu maji pamoja na punje za thomu zilizosalia na uchanganye na chumvi.

Katakata vitunguu maji vilivyosalia pamoja na pilipili hoho.

Para karoti kisha para nyanya na uziweke kando tayari kwa kupika.

Loweka viungo vya pilau vizima kwenye maji Kiasi.

Osha njegere zako ziwe tayari.

Katika sufuria safi, tia vipande vya kuku pamoja na viungo ulivyotwanga, tia maji kiasi, bandika kwenye moto na uviache vichemke.

Ikiwa ni kuku wa kisasa, mchemshe kwa dakika tano kisha umuache na supu yake.

Iwapo ni kuku wa kienyeji, mchemshe hadi atakapoiva kisha umuache na supu yake vile.

Kwenye sufuria safi mimina mafuta ya kupikia, bandika kwenye moto na usubiri yapate moto.

Kaanga vitunguu hadi vigeuke rangi ya dhahabu.

Tia pilipili hoho koroga na kisha ongeza karoti kisha nyanya na ukoroge mchanganyiko wako vyema.

Ongeza viazi na usubiri vikaangike kidogo.

Weka mchanganyiko wa vitunguu thomu na vitunguu Maji ulivyovitwanga kwenye Mchanganyiko wako.

Ongeza viungo vya pilau vilivyosagwa kwenye mchanganyiko huo.

Kisha weka viungo vya pilau vizima ulivyokuwa umeloweka.

Ongeza njegere na ukoroge vyema kisha mimina kuku na supu yake kwenye mchanganyiko huo.

Ongeza maji kiasi ili uendane na kiasi cha mchele kisha weka punje za zabibu kavu.

Hakikisha mchanganyiko wako una kiasi cha chumvi unachopenda ikiwa ni kidogo ongeza.

Subiri vichemke kisha ongeza mchele kwenye mchanganyiko huo, koroga kiasi na ufunike.

Iwapo unatumia gesi kupika, tumia moto wa wastan ili pilau lako lisije likaungua.

Maji yakikauka funua, changanya pilau lako vizuri kisha funika tena.

Subiri kama dakika tano na kisha ufunue kuangalia kama mchele wako umeiva.

Wali ukiwa umeiva basi pishi lako la pilau litakuwa tayari kwa kuliwa ukiambatisha kwa kachumbari ili linoge zaidi.

Vidokezo

Ili pishi lako la pilau linoge na linukie hakikisha viungo vya pilau vya unga umevitengeneza mwenyewe.

Unaweza pia ukatumia Pilau Masala kama hauna mchanganyiko wa viungo vya unga.

Unaweza ukatumia viungo zaidi upendavyo kuungia vipande vya kuku.

  • Tags

You can share this post!

Mwanamume akamatwa kwa tuhuma za kuua baba na kumzika...

Sitagura Liverpool hata tukishindwa kufuzu UEFA muhula ujao...