• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
MAPISHI KIKWETU: Jinsi ya kuandaa mahamri

MAPISHI KIKWETU: Jinsi ya kuandaa mahamri

NA MARGARET MAINA

[email protected]

KIMSINGI mahamri ni kama donati lakini huwa na ladha ya nazi na unga wa iliki.

Donati zina umbo la pete na tamu zaidi lakini mahamri huwa na umbo la pembe tatu au wakati mwingine pande zote. Kwa ujumla mahamri hufurahiwa kama kiamsha kinywa peke yake kwa chai au kahawa au kwa mbaazi.

Ingawa mahamri ni maarufu kama chaguo la staftahi, pia hutolewa pamoja na kitoweo na kari kama sehemu ya chakula kikuu.

Muda wa kuandaa: Dakika 10

Muda wa mapishi: Dakika 20

Walaji: 4

Vinavyohitajika

  • vikombe 3 vya unga wa ngano
  • kijiko 1 cha iliki
  • kijiko 1 cha hamira
  • kikombe ½ cha sukari
  • kikombe ¼ cha maziwa ya moto
  • kikombe 1 cha tui nzito la nazi
  • vijiko 2 vya siagi
  • mafuta ya kukaangia

Maelekezo

Mimina unga kwenye bakuli kubwa na uchanganye unga wa iliki na sukari.

Ongeza hamira na uchanganye vizuri. Ongeza kijiko kimoja cha siagi uchanganye ndani ya unga.

Changanya maziwa ya moto na tui la nazi.

Ukitumia mchanganyiko wa maziwa, tengeneza unga laini.

Ukitumia siagi iliyobaki, kanda unga kwa muda wa dakika tano hadi uwe laini.

Paka bakuli mafuta kidogo. Weka unga ndani yake. Funika na filamu ya kushikilia na acha unga uumuke kwa karibu muda wa saa mbili.

Gawanya unga katika sehemu nane ili utengeneze maumbo shepu ya mpira.

Yasukume maumbo hayo ukitumia mpini yawe duara halafu kata katika sehemu nne kwa kutumia kisu chenye makali.

Yasukume maumbo ya unga na mchanganyiko wa vitu vingine vinavyohitajika ukitumia mpini upate duara halafu kata katika sehemu nne kwa kutumia kisu chenye makali. PICHA | MARGARET MAINA

Weka pembetatu kando, rudia na unga uliobaki.

Pasha mafuta kwenye kikaangio kilicho katika chanzo cha moto wa wastani. Jaribu kwa kutumbukiza kipande kidogo cha unga kwenye mafuta ya moto. Ikiwa kinakauka na kuja juu mara moja, basi mafuta yamechemka vizuri na yako tayari.

Weka pembetatu (3 hadi 4 kwa wakati mmoja) ndani yake kwa upole na kaanga hadi mahamri yawe na rangi ya dhahabu. Kumbuka usiandae mahamri moto ukiwa mwingi sana kwani yatabadilika rangi haraka na ndani kubaki yakiwa mabichi.

Epua na upakue kisha ufurahie pamoja na familia au wageni.

  • Tags

You can share this post!

Sonko amalizika kisiasa

Michezo ya Jumuiya ya Madola: McGrath asema Shujaa imeiva...

T L