• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Michezo ya Jumuiya ya Madola: McGrath asema Shujaa imeiva kuhangaisha Uganda, Jamaica katika Kundi D

Michezo ya Jumuiya ya Madola: McGrath asema Shujaa imeiva kuhangaisha Uganda, Jamaica katika Kundi D

AYUMBA AYODI na GAKENIA MWIGE

KOCHA mkuu wa Kenya Shujaa, Damian McGrath atasikitika ikiwa vijana wake hawatafika awamu ya muondoano kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola mnamo Julai 29-31 ugani Coventry nchini Uingereza.

Mwingereza huyo alisema kuwa kazi kubwa ambayo wamefanya kwa majuma matano inatosha kuingiza Shujaa katika hatua ya muondoano kutoka Kundi D linalowakutanisha dhidi ya Australia, Uganda na Jamaica.

Alisema kuwa kwa miezi miwili amekuwa na timu hiyo, mtazamo wa wachezaji umeimarika.

“Kilichonipendeza ni kuwa wanachocheana kupata mafanikio,” alisema McGrath.

“Hatutaki kujigamba, lakini nahisi tuna uwezo wa kuwazidi Uganda na Jamaica na pia kutatiza Australia,” alisema na kuongeza kuwa awamu ya muondoano itakuwa mchezo tofauti kabisa ambapo chochote chaweza kufanyika.

“Unaweza kufanya mengi unapokuwa mzuri siku hiyo. Kenya imeonyesha ina uwezo baada ya kutawala Singapore Sevens mwaka 2016,” alieleza McGrath.

Alisema kuwa alipochukua usukani mwezi Mei, timu hiyo ilionekana kuwa na uchovu na isiyo na ari ambayo aliona kwenye Raga za Dunia.

“Nawafahamu wachezaji wa Shujaa kuwa na furaha, wakicheza densi na kutabasamu sana. Wakati huu, walikosa hivyo vitu, mambo hayakuenda vyema kila wakati,” alisema McGrath, akiongeza kuwa kiwango cha ufundi cha timu kilikuwa kibovu na makosa ya kijinga.

McGrath alisema benchi la kiufundi limefanya kazi nzuri katika kupiga msasa masuala ya kimsingi, huku kocha Geoffrey Kimani akisaidia pakubwa.

“Kimani amewaweka katika hali nzuri anayoweza. Tuko katika hali nzuri kimwili, ingawa kuna kazi bado inayoendelea. Tuko asilimia 50 bora kuliko tulipokuwa. Tuna mwili, kasi na nguvu,” alieleza McGrath akitaja kikosi cha mwisho kuwa mchanganyiko wa wazoefu na chipukizi.

Ingawa Wakenya wanafaa kuwa tayari kushuhudia mtindo tofauti wa uchezaji, McGrath alionya kuwa haihitaji miujiza na kuwa Roma haikujengwa kwa siku moja. Itachukua muda, lakini utaona timu ikiimarika na Wakenya watakuwa na furaha,” alisema.

Nahodha Nelson Oyoo alisema utelekezaji wa ikabu na ushikaji wa mpira zimeimarika kwa wiki tano wamekuwa kambini Kasarani. “Tunasubiri kwa hamu kubwa kuingia katika droo kubwa na hatimaye katika mduara wa medali,” alisema Oyoo.

TAFSIRI: GEOFFREY ANENE

  • Tags

You can share this post!

MAPISHI KIKWETU: Jinsi ya kuandaa mahamri

KASHESHE: ‘Walinitilia sumu’

T L