• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:50 AM
MAWAIDHA YA KIISLAMU: Zakatul Fitr ni amri yake Mungu kwa waumini

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Zakatul Fitr ni amri yake Mungu kwa waumini

NA HAWA ALI

SIFA zote njema anastahiki Mwenyezi Mungu, Muumba wa mbingu na ardhi na vilivyomo.

Swala na salamu zimwendee Mtume Muhammad Swallallahu ‘Alayhi Wasallam. Inshallah tunaelekea kumaliza mfungo wa Saumu na ningependa tujifunze machache kuhusu Zakat-ul-Fitr au Sadaqat-ul-Fitr.

Nayo ni ‘Sadaqa ya utakaso wa kufungua saumu. Na ni kiwango fulani cha chakula kinachotolewa na waislamu katika siku chache za mwisho wa Ramadhan au siku ya ‘Idd asubuhi, kabla ya kuswaliwa Swala ya ‘Idd.

Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala) ametuamrisha kutoa zakat-ul-fitr kwa sababu mbili.

– Kuwatakasa wale waliofunga, kuzisafisha saumu zao kutokamana na mambo ya upuzi, kama vile mazungumzo yasiofaa na madhambi madogo.

– Kuwalisha Waislamu masikini ili nao wawe na chakula cha kuwatosha siku ya ‘Idd.

Zakat-ul-fitr ni faradhi (wajib) kwa wale wenye uwezo wa kutoa.

Imeelezwa hii waziwazi kwenye Hadith ya Ibn ‘Umar (Radhiya Llahu anhu): ‘Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) ameamrisha zakat-ul-fitr itolewe kwa kiwango cha Sa’a moja ya tende au Sa’ moja ya shayiri (Barley), kwa Waislamu (Mtumwa au aliye huru mume au mke, mdogo au mkubwa). Na akaamrisha itolewe kabla ya watu kwenda kuswali swala ya ‘Idd’Hadithi hii inazidi kudhihirisha ya kwamba ni wajib juu ya kila muislamu (mwenye uwezo) bila ya kujali umri wala hali ya kijamii.

Jukumu la kutoa zakat ul-fitr ni juu ya kiongozi wa nyumba; inampasa kutoa kwa niaba yake mwenyewe na wale walio chini ya usimamizi wake: wadogo kwa wakubwa, waume na wake, watumwa na waungwana. Ibn Umar (Radhiya Llahu anhu) akasema: ‘Ameamrisha Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) sadaqat ul-fitr itolewe kwa walio chini ya usimamizi wako: wadogo na wakubwa, waungwana na watumwa.’

Ama kwa yule asokuwa na uwezo wa kifedha, huyo amesamehewa kwa sababu ya Nas’ kutoka kwenye Qur’ani na Sunna, kama vile maneno ya Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala) alivyosema: ‘Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi yoyote illa yaliyo sawa na uwezo wake…’

Baadhi ya wanavyuoni waonelea kuwa hata kijusu (mtoto kabla ya kuzaliwa) nae alipiwe kwa niaba yake. Hata hivyo, hapana ushahidi wa hayo; na huyo kijusu hachukuliwi kuwa ni kijana – si katika lugha wala kawaida za watu.

AINA ZA ZAKAT-UL-FITR

Alivyokuwa akifanya Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) na Maswahaba zake ni kutoa zakat-ul-fitr kwa njia ya chakula. Akapokea Abu Sa’id al-Khudri (r.a): ‘(Katika wakati wa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) tulikuwa tukitoa zakat-ul-fitr kama Sa’ moja ya twa’am (chakula), Sa’ moja ya shayiri, Sa’ moja ya tende, Sa’ moja ya Aqit, au Sa’ moja ya zabibu kavu.

Wakati huo chakula chetu cha kawaida kilikuwa ni shayiri, zabibu kavu na tende.

Mtu anaweza kukadiria kiwango cha fedha cha gharama ya mali alokusudia kutoa, na akampa mtu au chama ambacho anakiamini kuwa watanunuwa aina (ya chakula) inayofaa. Ni muhimu ya kwamba itakapomfikia anaepasa kupokea hiyo zakat ul-fitr, iwe katika hali inayoruhusiwa kwenye Sunna.

Inaruhusiwa kuchagua watu kukusanya zakat-ul-fitr miongoni mwao.

Vile vile inaruhusiwa kuwapa (hiyo zaka) hao wakusanyaji iwapo wanahitaji na wanastahiki. Zakat-ul-fitr inapasa kugawanyiwa masikini (wanaohitaji) kama ilivyosemwa kwenye hadithi ya Ibn ‘Abbas.

Haistahiki kupewa miongoni mwa aina nane za watu wanaopewa Zaka ya kawaida. Mtu maskini si mtu alie kwenye hali ya ufukara wa hali ya mwisho, lakini ni mtu ambaye hali yake ya kifedha ni kiasi cha haja.

You can share this post!

Wakenya kubaki bila kazi hoteli ya Hilton ikifungwa

Rais Suluhu atangaza siku mbili za maombolezo ya Kibaki

T L