• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 5:04 PM
Mazingira: Malalamishi ya mipira ya kondomu kusambaa

Mazingira: Malalamishi ya mipira ya kondomu kusambaa

NA MWANGI MUIRURI 

UTAWALA wa Gavana Irungu Kang’ata wa Murang’a umekosolewa kuhusu uwezo wake wa kutekeleza sheria za kimazingira.

Huku watoto wa shule wakiwa katika likizo ndefu ya miezi miwili, baadhi ya wazazi wameteta kwamba vichochoro vya miji kadha ni vichafu nyumba zingine za upangaji zikiwa chafu.

“Tunaomba utawala wa Kang’ata uwaandame wanaochafua mazingira kiasi hata cha kutupa ovyo ovyo mipira ya kondomu iliyotumika na ambayo watoto wetu wanachukua na kucheza nayo kama baluni,” akasema Bi Sarah Njahira mkazi wa Murang’a.

Bw Charles Ngigi ambaye ni mpangaji katika mji wa Murang’a aliteta kwamba ukaguzi wa nyumba za upangaji umetelekezwa huku wamiliki wengi wakikosa kuzingatia usafi wa kimsingi.

“Nyumba nyingi za kukodisha hazijapakwa rangi huku miundo mbinu ya baadhi ya zingine ya kutupa majitaka ikiwa katika hali duni. Hali hii inafanya afya ya wapangaji kuwa hatarini, huku ugonjwa hatari wa Kipindupindu ukituvizia,” akasema.

Mwenyekiti wa muungano wa uzingatiaji usalama wa kimazingira kupitia kilimoasili, Bw Martin Ndirangu aliteta kwamba “tumekuwa tukilalamika kuhusu uchafuzi kiholela wa kimazingira lakini tunaambiwa kuwa kaunti haina maafisa wa kutosha kuzingatia utekelezaji sheria”.

Mkazi wa Murang’a atembea katika barabara moja ya Murang’a ambayo imegeuzwa kuwa jaa la taka. PICHA|MWANGI MUIRURI

Bw Ndirangu alisema kwamba mabwanyenye katika sekta ya ujenzi na ukodishaji nyumba ni watu walio na ushawishi mkuu na ambapo maafisa wa kaunti hulemewa kuwadhibiti.

“Kuna tetesi zingine hata ukizileta kwa Serikali ya Kaunti haziwezi zikafuatiliwa kwa kuwa zinahusu mabwanyenye, wanasiasa na washirika wa utawala. Siasa nyingi katika vitengo vya Serikali ya Kaunti zinawaacha wengi wa maafisa wakijiepusha na kutekeleza sheria ipasavyo,” akasema mmoja wa mfanyakazi katika baraza la manispaa ambalo huratibiwa na Serikali ya Kaunti.

Bw Ndirangu alisema kwamba kaunti inajizatiti tu kudumisha usafi katika uso wa miji lakini kwa vichochoro kukiwa na miundombinu ya taka iliyopasuka na kuvuja, nyumba zikiendelea kudumu kando mwa viini vya maji na hata sheria za kelele kutoka kwa vilabu na viwanda vikikosa wa kutekeleza.

Waziri wa Mazingira Bi Mary Magochi alisema kwamba amekuwa akipata tetesi hizo kutoka kwa baadhi ya wakazi “lakini huwa natuma maafisa kuwajibika”.

Alisema atafuatilia visa ambapo malalamishi hayajashughulikiwa.

“Kuna baadhi ya mambo tumefanya ya kudumisha usafi na tumepata ufanisi mkuu. Sehemu ambazo tumerekodi upungufu tutatatua pia,” akaahidi.

Njia ya maji taka yakiwemo ya choo iliyoko katikati mwa vyumba vya makazi ya wapangaji Mjini Murang’a. PICHA|MWANGI MUIRURI

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Tamasha za Utamaduni: Mafuriko yarefusha muda wa wageni...

Raila na Kalonzo washauriwa wasitengane 

T L